Chiku Masanja na siri ya kuwapaisha wanawake

Kati ya mambo yaliyompa sifa Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Iringa, Chiku Masanja ni uwezo wa kuandaa viongozi wa kike kushikilia nafasi za uongozi za ndani na nje ya CCM.

Vijana wengi wamezoea kumuita mama, si kwa sababu ya umri wake hapana ila ni kwa namna anavyowalea na kuishi nao wakati anapowaandaa kuongoza.

“Ukiwa katibu lazima uwatambue wasichana wenye vipaji vya uongozi. Wakati mwingine unakutana na binti hajawahi kufikiria kuwa mwanasiasa ila ukihisi ana kipaji cha kuongoza unamshawishi na kumuonyesha njia mwisho anagombea na hata kufikia ngazi ya waziri,” anasema Masanja.

Mwenyewe anasema uvumilivu, upole na ucheshi ndivyo vilivyomfikisha mahali alipo.

“Nilikotoka mpaka nilipo ni mafanikio makubwa kwangu kisiasa, nilikuwa katibu wa tawi, lakini namshukuru Mungu kwamba naongoza wanawake wenzangu kwenye mkoa,” anasema.

Mara ya kwanza kukutana na Masanja alikuwa katibu wa UWT Manispaa ya Iringa.

Licha ya kuwepo kwa makundi ya uchaguzi yenye nguvu ya kumvutia mtendaji wa chama kwenda upande fulani, hakuwahi kuyumba zaidi ya kusimamia haki.

“Kuna wakati ukiongea na huyu, mwingine atachukia na ukiongea na yule, huyu atachukia. Hii ndiyo changamoto kikubwa, cha msingi ni kusimamia kanuni na katiba,” anasema.

Masanja alianzaje?

Mwanamama huyo awali alikuwa mtumishi wa umma akifanya kazi Ofisi ya maliasili na utalii mkoani Singida na wakati huo alikuwa katibu wa tawi wa CCM.

Anasema baada ya kuolewa mwaka 1996 aliamua kuacha kazi ili alee na kuitunza familia yake.

“Nikaona ndoa na mambo mengine ya kibiashara yaliingiliana, nikawa mama wa nyumbani lakini katika kuwa mama wa nyumbani niliendelea na siasa,” anasema.

Masanja aliwania ujumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa akapata na baadaye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Singida.

Anaeleza kuwa wakati akiwa mwenyekiti wa UWT wilaya aliomba kuwa diwani wa viti maalumu nafasi ambayo pi alipenya. Wakati huo ilikuwa ruksa mwana CCM kuongoza nafasi mbili.

“Niliongoza nafasi ya udiwani kwa vipindi viwili na nikiwa kwenye udiwani nilifanikiwa kuwa kwenye kamati mbalimbali kuhakikisha maendeleo kwenye wilaya yetu,” anasisitiza.

Akiwa bado diwani aliteuliwa kuwa Katibu wa UWT wa wilaya huku kituo chake cha kwanza cha kazi kikiwa Iramba (Singida). Baadaye alikwenda Urambo mkoani Tabora na Ulanga Mkoa wa Morogoro kabla ya kuhamia Wilaya ya Iringa Mjini. Alipanda na kuwa Katibu wa UWT Mkoa wa Iringa, akahamia Ruvuma kabla kurejeshwa tena Iringa aliko sasa.

Siri ya mafanikio

Anasema siri ya mafanikio ni kuwafanya anaowaongoza kuwa rafiki zake wakiwamo wasichana wenye ndoto za kuwa viongozi.

Anasema anajivunia kuwanoa na kuwapika viongozi wengi wanawake ambao kwa sasa wameshikilia nafasi mbalimbali za nchini.

Miongoni mwa wanawake hao ni Pendo Ngonyani ambaye amekuwa katibu tawala wa wilaya.

“Mwanamke hutakiwa kuwa mchoyo kwamba huyu nikimsaidia atafaidika. Usimzibie mtoto wa mwenzako kama ana uwezo, kwa hiyo binafsi naamini siri ya mafanikio ni kuwabeba wengine,” anasisitiza.

Atoa ushauri

“Kwenye dunia hii jambo kubwa ni mahusiano, uadilifu na nidhamu. Waheshimu watu wote mkubwa na mdogo na ukishafanya hivyo watu watakusaidia,” anasema.

Anasema ukikosa nidhamu na kudharau watu itakuwa rahisi kupotea na mwisho mtu asipate kile anachokusudia.

Mkakati wake

Masanja anasema mwanamke ni katibu wa familia, hivyo lazima awe na uchumi imara.

Anasema uchumi imara unaweza kumjengea mwanamke ujasiri na kumuepusha kwenye vishawishi hivyo kupata kile anachotaka. “Hata kwenye siasa ukija na uchumi imara rahisi kufanikiwa kwa sababu hauna wa kukuyumbisha, kwa hiyo mkoa wetu naamini utasonga mbele,” anasema.

Anawaasa wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.