Christina na Regina; Mapacha wanaotikisa tamthilia ya Huba

Ni rahisi kuamini kuwa waigizaji Rucky na Rani wanaocheza katika tamthilia ya Huba ni mtu mmoja, lakini ukweli ni kwamba hawa ni Christina na Regina.

Hili linawezekana kutokana na ukweli kwamba kwa vipaji waliojaliwa navyo huweza kuigiza hata watatu watatu tofauti katika filamu moja, lakini unakuta mtu ni yuleyule.

Hata hivyo, watayarishaji wa tamthilia hiyo inayorushwa katika kituo cha Maisha Magic Bongo walihitaji pacha halisi na ndipo bahati ikawaangukia Regina na Christina.

Filamu iliyowapa umaarufu ni Siri ya Mama. Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, mmoja wa pacha hao, Christina, anasema safari yao ya sanaa ilianzia mjini Morogoro baada ya Regina kushinda shindano la Miss Morogoro 2006 lililompa tiketi pia ya kushiriki Miss Tanzania.

Mwenzake, Regina, hakushiriki katika mashindano hayo kwa sababu alikuwa na mwili mkubwa yaani kibonge.

Mbali na kuwa Miss Morogoro, Christina amewahi kushinda mataji ya Miss Ukonga, Miss Utalii Morogoro na Miss Singida.

Kati ya watu waliokuwa wakimtembelea Regina baada ya kutwaa taji hilo ni pamoja na kikundi kimoja cha sanaa ya maigizo cha mjini humo ambapo baadaye walimshawishi aingie kwenye uigizaji.

“Kikundi hicho kilikuwa kikirusha tamthilia yake katika kituo cha televisheni cha Abood na kwa kuwa wote tumejikuta tukipenda vitu kwa pamoja, tuliingia wote katika kundi hilo na hapo ndio safari ya uigizaji ilipoanzia kwetu,” anasema Christina.

Hata hivyo mwishoni mwa 2004 Christina anasema walihamia mkoani Dar es Salaam katika kutafuta maisha na kuamua kusimamisha shughuli za sanaa.

Anasema ilipofika mwaka 2008 walirudi tena kwenye ‘gemu’ na hii ni baada ya pacha wake Regina kukutana na msanii Jacob Steven ‘JB’ aliyekuwa akirekodi filamu ya ‘Regina’ wakati huo ambako aliamua kuwashirikisha kucheza kama mwigizaji wa ziada japokuwa Regina hakufanikiwa kurekodi kutokana na kupata dharura.

“Katika harakati hizo za kujitanua kisanaa, pacha wangu akakutana tena na msanii Cloud aliyecheza naye filamu ya Kaburi la Mapenzi na baadaye akakutana na msanii Shija ambaye alimchezesha filamu ya Aisha - filamu iliyompa umaarufu hadi leo kupachikwa jina la Aisha.”

Haikuishia hapo, Shija baadaye aliamua kuwachezesha filamu ya Siri ya Mama kwa pamoja na hapo ndipo baadhi ya watu wakashtuka kwamba ni watu wawili tofauti na wakaanza kupata kazi za kucheza filamu mbalimbali hadi leo kuwa mojawapo wa wasanii wa kike wanaofanya vizuri katika tasnia hiyo.

Christina na Regina walizaliwa miaka kadhaa mkoani Mara na kusoma shule ya msingi Nyamongo na baadaye kujiunga na Sekondari ya Nyamongo kisha wakaanza kusaka maisha sehemu mbalimbali japokuwa kwa sasa makazi yao ni Dar es Salaam.

Pacha hao pia ni wazazi wa watoto wawili kila mmoja.