Chukua tahadhari unapoweka mboni za urembo

Saturday February 15 2020

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Wasichana wengi hasa wa mjini hukimbizana na fasheni inayoenda na wakati, ikiwamo ya uwekaji mboni bandia.

Rehema Sultan, mkazi wa jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa watumiaji mahiri wa mboni hizo. Anasema huwa anaziweka mara kwa mara kadri anavyotaka aonekane.

Tofauti na ushauri unaotolewa na madaktari kwamba watumiaji wa mboni hizi wanatakiwa kufuata ushauri wa kitabibu, yeye anasema hajawahi kupimwa chochote kwa lengo la kuona kama anastahili kuwekwa au la.

“Mara ya kwanza nilijiweka mwenyewe, niliponunua tu nikaweka...bahati nzuri ukishaiweka jichoni yenyewe inaenda kutafuta eneo inayopaswa kukaa,” anasema rehema.

Hata hivyo, anasema anafahamu hatakiwi kulala nazo kwani kufanya hivyo si salama, lakini huwa inanitokea anafanya hivyo mpaka kwa siku mbili mfululizo ila anasisitiza kuwa hamshauri mtu afanye hivyo kwa kuwa ni hatari.

Tahadhari nyingine anayochukua Rehema ni kuepuka kuusogelea moto. Ukiwa na mboni hizo anasema haitakiwi kuwa jirani na moto kwa sababu inayeyuka, hivyo ikikutokea unaweza kuwa kipofu.

Advertisement

Licha ya kuujua ukweli huo, Rehema anasema anapenda kubadilisha mwonekano wa macho yake kila wakati ndiyo amekuwa mpenzi wa mboni za rangi tofauti.

Daktari ashauri

Wataalamu wa afya ya macho wanatahadharisha kuhusu tabia ya wanawake wanaopenda kubadili muonekano wa macho yao kwa kuweka urembo huo, wakisema usipofanywa kwa umakini unaweza kusababisha athari kiafya.

Dk Nestory Massawe, mtaalamu wa macho katika Hospitali ya Mloganzila, anasema mboni zinapaswa kumsaidia mtu mwenye matatizo ya macho, kinyume na hapo si salama sana kuwekwa mwilini.

Ingawa urembo huu unapendwa sana na wanawake, Dk Massawe anasema kwenye matibabu ya macho, mboni za kubandika hutumika kuwasaidia watu wenye uoni hafifu.

Vilevile, anasema hutumika kufunika mboni halisi ya jicho ambayo imetoboka kiasi cha kuvujisha ute uliomo ndani yake. Kadiri kimiminika hicho kinavyoendelea kutoka hulifanya jicho kuwa kavu.

“Mboni ya jicho inapotoboka tunaiziba kuliondoa kwenye ukavu uliopitiliza ambao kitaalamu si salama,” anasema.

Massawe anasema matibabu ya kuweka mboni jichoni yanahitaji utaalamu mkubwa ili isilete madhara kwa mgonjwa.

Wakati imewekwa anasema mboni haitakiwi kuingia maji, hivyo haishauriwi kuoga wala kuogelea nazo.

“Kabla ya kulala zinatakiwa ziondolewe kwani si salama kulala nazo, ni hatari kwa macho. Mgonjwa anatakiwa azitoe na kuzihifadhi kwenye kontena lake ambalo huwa na kimiminika maalumu cha kuzisafishia. Mboni zinatakiwa kukaa humo kwa saa sita kabla ya kuvaliwa tena,” anasema Dk Massawe.

Kwa kawaida, mboni hutunzwa na kuangaliwa kwa uangalifu na mtaalamu huyo wa macho anasema hizi za kubandika uangalifu wake unapaswa kuongezeka maradufu kwani haitakiwi kwa namna yoyote ile kuwa na uchafu.

Anasema ubandikapo mboni, hakikisha umekata kucha zako za mkononi ili kupunguza uwezekano wa kukwangua au kuzichubua wakati unazibandika.

Vilevile anasema hakikisha unasafisha mikono kwa usahihi kabla ya kugusa mboni unazotaka kuweka jichoni na kabla hujazibandika mhusika ahakikishae hashiki mafuta wala kipodozi kingine chochote.

“Mboni zinahitaji usafi wa hali ya juu, unapoiweka kwenye jicho unaongeza joto na ifahamike kuwa bakteria wanapenda mazingira yenye joto sasa hapo unawakaribisha wazaliane na wakiwa wengi wanahatarisha usalama wa jicho lako,” anasema.

Dk Massawe anasema ikitokea jicho linawasha au lina wekundu wa aina yoyote mwekaji hatakiwi kuweka mboni, hata kama anaitumia kwa matibabu ya macho, hadi pale atakapoangaliwa na mtaalamu na kupewa matibabu stahiki.

Mtaalamu huyo anaongeza kuwa umakini mkubwa unahitajika kwenye kimiminika kinachotumika kusafisha mboni bandia na namna ya kuzisafisha.

“Ni kimiminika maalumu kwa ajili ya kusafisha ambacho kimetengenezwa kwa kemikali. Ikitokea mboni imewekwa kwenye kiminika tofauti na kinachohitajika upo uwezekano wa kung’ang’ania jichoni na hivyo kuitoa kwake kukahitaji utaalamu zaidi,” anasema.

Mambo ya kuzingatia

Wataalamu wanashauri kwamba anayeweka mboni bandia ni lazima apimwe na daktari kujua mambo kadhaa ikiwamo wingi wa machozi kwani mtu mwenye macho makavu hatakiwi kutumia mboni hizi.

Kabla ya kuwekwa mhusika pia ni lazima afundishwe kwa kina kuhusu mboni, matumizi yake, jinsi ya kuziweka, kuzitoa na kuzitunza kwa usafi.

“Mtu anayewekewa kwa mara ya kwanza hatakiwi kukaa nazo kwa zaidi ya saa tatu,” anasema Dk Massawe.

Ni muhimu kufahamu tarehe ya mwisho ya kutumika kwa mboni husika kabla ya kuwekwa jichoni.

“Ukitumia mboni iliyokwisha muda wake ni lazima italeta madhara jichoni,” anasema.

Kimiminika kinachotumika kusafishia mboni ni lazima kiendane na aina ya mboni yenhyewe, kinyume na hapo inaweza kuleta madhara kwenye jicho la mtumiaji.

Athari za kubandika mboni

Jarida la Firstcry Parenting linaeleza kuwa kuna athari nyingi kwa mtu anayeweka mboni kwa saa 24 wiki nzima.

Athari hizo ni pamoja na jicho kukosa hewa safi ya oksijeni kwani mboni huzuia hewa kuingia jichoni wakati kiafya hewa hiyo inahitajika ili kuyafanya macho kuwa salama.

Mboni pia zinaweza kusababisha macho kuwa makavu na kutengeneza wekundu. Matokeo ya hali hiyo ni mboni halisia kupata majeraha.

Kwa mujibu wa jarida hilo mboni za kubandika zinavuta machozi mengi kuzifanya zilainike, kitendo kinachoyafanya macho kuwa makavu wakati yanatakiwa kuwa na majimaji muda wote.

Athari nyingine ni uwezekano wa kutokea kidonda kwenye mboni halisi ya jicho. Hii inatokea pale bakteria, fangasi au virusi vinapotokea kwenye mboni bila kuondolewa, hivyo kuchangia kutengeneza kidonda ambacho kinaweza kusababisha upofu wa kudumu.

Tatizo jingine linalowakuta wanaovaa mboni kwa muda mrefu ni kuhisi maumivu ya macho. Hii inatokana na mboni kuzuia kusambazwa kwa hewa ya oksjeni kwenye macho, jambo linalosababisha yaume au kupoteza nguvu.

Kuna uwezekano wa kupata mzio (allergy) pia iwapo mtu anavaa mboni kwa muda mrefu kwa siku za baadaye.

Advertisement