DC Mbogho: Magufuli amenisaidia

Saturday February 9 2019

 

By Daniel Mjema

Swali: Umekuwa mkuu wa Wilaya ya Mwanga kwa miaka mitatu hadi Rais alipotengua uteuzi wako, hivi mtu akitaka kukufahamu unaweza kumwelezaje wewe ni nani?

Jibu: Nilizaliwa miaka 49 iliyopita mkoani Singida, sehemu moja inaitwa Mtinko. Nilihitimu elimu ya msingi mwaka 1986 katika Shule ya Msingi Malolo. Kidato cha nne mwaka 1990 na cha Sita mwaka 1993 katika Sekondari ya Mwenge iliyopo mjini Singida.

Nilisoma shahada ya kwanza ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro. Na shahada ya uzamili ya wadudu ya Chuo Kikuu cha Missouri, Kampasi ya Columbia nchini Marekani. Katika fani hii niligundua wadudu wawili wa mazao hapa Tanzania ambao walikuwa hawajatambuliwa, nikawapa majina ya kisayansi. Mmoja ni Neomacrocris vuga, na Neomacrocoris bondelaufa.

Kwa sasa naendelea na utafiti wangu kwenye visumbufu vya mazao na namna ya kuwadhibiti shambani kwa kuzingatia wingi wao.

Utafiti huu ni sehemu ya kozi ya Shahada ya Uzamivu ya viumbe hai (PhD in Applied Zoology) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Swali: Ulipoteuliwa kuwa DC Mwanga, uliikuta wilaya ya katika hali gani na umeichia nini cha kujivunia?

Aaron Mbogho: Nilifika Mwanga Julai 2016, nilikuta wilaya inakusanya si zaidi ya Sh1 bilioni kwa mwaka kama mapato yake ya ndani. Kwa kutumia vyanzo vilevile vya mapato kwa kiwango kilekile cha tozo/ushuru, niliweza kusimamia na kuifanya halmashauri ifikie zaidi ya Sh2 bilioni. Mwaka huu nilikuwa natarajia waripoti zaidi ya Sh3 bilioni. Cha kujivunia hapa ni usimamizi kwa kuwa hakuna jipya kwenye vyanzo vya mapato.

Kingine ni kuweka nidhamu katika kazi kwa watendaji. Nilikuta si jambo la ajabu mtumishi kudaiwa rushwa na wahasibu ili hundi yake ya malipo halali ishughulikiwe. Nilianza na mweka hazina wa wakati huo, nikahakikisha huo uonevu unapungua kama si kuisha kabisa. Mweka hazina wa wakati huo na timu yake ilikoma kukalia madai ya watu kwenye ofisi ya malipo. Hapa nilikuwa napingana na ukweli kwamba samaki hukunjwa angali mbichi. Mimi nilikuta wamekauka ila nikawa nawaloweka na kuwataka wanipe ushirikiano wakati nawarekebisha. Hapo ndipo palikuwa patamu kwani mbinu zote zilikuwa zinahitajika kukunja samaki wakavu.

Nakumbuka nilikuta injinia aliyesoma shahada ya biashara na uchumi. Watumishi wa aina hii hawakuwa wepesi kuelewa na walioshindwa kunielewa walijiondoa wenyewe kwa hiari. Nilikuta idara ya maji ina changamoto nyingi sana, lakini hadi naondoka naicha wilaya ikiwa inaweza kufikisha maji safi kwa zaidi ya asilimia 80 ya watu wake.

Pia, mamlaka ya maji ya mji mdogo ikiwa ina uwezo wa kujiendesha bila ruzuku ya serikali. Udanganyifu kwenye mitihani ilikuwa ni nyenzo kwa baadhi ya shule kujitangaza; sasa udanganyifu huo umepungua sana. Matumizi ya walimu wasio Watanzania kwa njia ya mkato yalikuwa yamekithiri kwa kuwatumia watumishi wa idara ya uhamiaji wasio waaminifu, sasa wanayohofu kwani nililiangalia suala hili kwa umakini ili kulinda ajira za wazawa.

Halmashauri kwa mara ya kwanza ilinunua gari jipya kwa mapato ya ndani. Kisiasa, niliwafanya wanamwanga waiamini serikali yao hadi chama changu (CCM) kushinda chaguzi ndogo zote za nafasi mbalimbali zipatazo 60 huku vyama vya upinzani havikiambulia hata nafasi moja kwenye uongozi. Mambo ni mengi nimefanikiwa na sijutii kuiacha wilaya kwenye hali hii kulinganisha na nilivyoikuta.

Swali: Wewe ni miongoni mwa wakuu wa wilaya waliotumia sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ya mwaka 1998, kuwaweka watu ndani akiwamo DED, DAS, mwenyekiti wa CCM wa wilaya na wengine, nini kilikusukuma kuchukua hatua hizi?

Aaron Mbogho: Watu wa kwanza kuwaweka ndani kwa amri yangu walikuwa wavuvi haramu wanne kutoka eneo la Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Ilikuwa ni mapema kabisa baada ya kuapishwa Julai 2016. Nakumbuka nilipigiwa simu na msamaria mmoja akaniambia kuwa hao watu ni wanachama wa vyama fulani vya siasa. Nilimjibu kuwa sikuwauliza watu vyama vyao bali nilitizama walitenda kosa gani.

Huwa siulizi asili ama ubini hata wadhifa wa mtu kama anachofanya ni kinyume cha sheria na kanuni. Ni kweli, niliwahi kuweka ndani watu wengi lakini kila wakati nilikuwa nalazimishwa na matendo yao kufanya hivyo.

Wengine niliwapeleka kwa amri yangu na hao walikaa ndani sio chini ya saa 24 na wengine niliamru wapelekwe polisi kwa sheria zingine kama ambavyo raia mwingine angeweza kuwapeleka kwa ajili ya hayo waliyoyafanya. Hao utawatambua kwa muda waliokaa polisi ambako hawakufikisha saa 24.

Walifika wakatoa maelezo na kuachiwa huru ama kwa dhamana baada ya jalada la uchunguzi kufunguliwa. Kwa kifupi, wote nilioamuru waende polisi ama wawekwe rumande walikuwa na makosa yaliyowapelekea kufikishwa huko, hakuna mtu ambaye niliamrisha apelekwe kisa ameniudhi mimi binafsi kwenye mambo yasiyo ya kikazi ama yasiyo na public interest.

Natoa mifano michache bila kutaja wahusika hasa viongozi na watumishi. Utakuta kiongozi anatoa amri wananchi washambulie askari wanaofanya kazi yao ama wahalifu wasilipishwe faini za makosa yao. Au kiongozi anamwandikia mtumshi malipo ya masurufu (perdiem) wakati mtumishi hajasafiri tena kukiwa na makubaliano ya kumrejeshea hizo pesa zote ama sehemu kwa matumizi ambayo hayakuombewa. Ama kiongozi anaomba kuuziwa gari la sekakali halafu akishaona kakubaliwa kulinunua, anapanga kulifanyia matengenezo makubwa kwa pesa ya serikali, hayo ni matumizi mabaya ya pesa za umma na mbaya zaidi ukimkatalia anakuwa mbogo ( sio mbogho). Ama mtumishi anafanya matumizi yasiyoidhinishwa na kamati husika na bila taratibu za manunuzi kufuatwa.

Ama unakuta mtumishi amegushi majina hewa na sahihi hewa kuonyesha amefanya malipo kwa fedha ya umma. Kwa taarifa yako haya hayafanyiki bila ya kuwepo na ushawishi usiohalali. Labda tujiulize kwanini wengi hawakuwa wanafikishwa mahakamani.

Moja ni wao wenyewe kuomba radhi na kukiri kuwa hawatarudia, pili hasa watumishi wa umma, RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) amekuwa akiingilia na kuniambia atawashughulikia kwa taratibu zao za kinidhamu hivyo niwaachie. Tatu ni wanasiasa kuingilia kati kuwa kaeni mzungumze na kuonyana kuliko kwenda mahakamani.

Swali: Rais ametengua uteuzi wako, unazungumziaje hatua hiyo?

Aaron Mbogho: Mimi namshukuru mheshimiwa Rais kwa maamuzi haya kwa sababu amenisaidia kutokutenda dhambi ya kudhalilisha mamlaka ya uteuzi kwa kujiuzulu. Nilikokuwa nimefikia nilikuwa navumilia sana taabu ya kufanyakazi na watu ambao wana mitazamo kinzani.

Ninachokiona ni sita wao wanakiona ni tisa kwa sababu wamesimama ambapo hawatakiwi kusimama ili kuisoma hiyo namba kwa sababu ya kujali masilahi binafsi wakati mimi naangalia masilahi mapana kwa ajili ya manufaa ya Taifa.

Wengi wao wanapenda kwa kila wafanyalo watafaidikaje leo wakati mimi nafikiria jamii itanufaikaje leo na kesho na hata kizazi kikacho. Hivyo, msuguano usingeisha kati ya mitizamo hii miwili.

Mheshimiwa Rais amenisaidia sana kunitenganisha na watu wenye mitazamo kinzani na wangu.Ingekuwa ni fedheha kwa mteule wa Rais kujiuzulu kwa hiari yake bila hata ya ushauri wa mamlaka iliyomteua na tena bila ya kuwa na kashfa ambayo machoni pa wengi inaonekana wazi ni kuidhalilisha serikali. Ningeweza kujiuzulu kwa manufaa ya serikali kama ningekutwa na kashfa ya wizi, ubadhirifu na rushwa ili serikali isitukanwe lakini sio kwa kukosa huruma kwa wahalifu na wakwamishaji wa shughuli za maendeleo. Kuitwa mkali ama mnoko kwa masilahi ya taifa ni jambo jema kuliko kuitwa mkarimu na mpole kwa upendeleo na woga wa kuchukua maamuzi ili kuilinda nafasi yangu.

Swali: Tumeambiwa wewe ni mtaalamu uliyebobea katika masuala ya wadudu, unazungumziaje ukweli huu na kwanini unaonekana pengine wewe ni mtaalamu pekee au mko wachache nchini. Unaweza kufafanua hili?

Aaron Mbogho: Kama nilivyojitambulisha kwenye swali lako la kwanza, fani yangu ya wadudu inaonekana ya pekee kwa ajili ya uchache wa wenye fani hii. Upekee wangu labda unakuja kwa kuangalia idadi ya wataalam wa wadudu kwenye wizara ya kilimo ambapo waliwahi kukiri kuwa wataalam wa wadudu ni wachache na pengine watambuzi wa wadudu ndiyo kabisa haba mno.

Hii iliaminishwa na mvutano uliotokea mwaka 2015 kati ya idara ya utafiti na idara yangu wakati huo ya maendeleo ya mazao kunigombania. Utafiti wanamuomba katibu mkuu nihamie kwenye utafiti wakati huo idara yangu inakatalia huo uhamisho kwa madai kuwa na wao hawana mtaalam wa aina yangu. Kesi hiyo ilimalizwa na katibu mkuu Sophia Kaduma kwa kuniuliza maoni yangu na nikachagua kwenda utafiti. Sina ikama ya sasa huenda wameshasomeshwa wengine wa fani hii ya utambuzi wa wadudu. Watu wengi wanasomea udhibiti wa visumbufu (insect pest management) ama matumizi na madhara ya wadudu (applied entomology) sio insect systematics niliyofanyia shahada ya uzamili japo sasa ninafanya shahada ya uzamivu kwenye udhibiti wa visumbufu yaani insect pest management.

Swali: Wewe ni miongoni mwa makada wa CCM uliyewahi kugombea Ubunge Singida, Je unaweza kuwaambia watanzania ni jimbo gani na hali ilikuwaje katika kura hizo za maoni?

Aaron Mbogho: Mwaka 2015 niliingia kwenye kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea kupitia chama changu pekee cha maisha yangu yote ya siasa yaani Chama cha Mapinduzi. Kwenye mbio hizo nilimaliza kwa kushindwa ama kwa kura za maoni kutokutosha na sikuteuliwa kugombea. Niligombea jimbo la nyumbani kwetu la Singida Kaskazini.

Swali: Umekaa Mwanga kwa zaidi ya miaka mitatu na umekutana na changamoto mbalimbali ikiwamo uvuvi haramu Bwawa la Nyumba ya Mungu, una ushauri gani kwa mrithi wako?

Aaron Mbogho: Bwawa la Nyumba ya Mungu lipo Manyara na Kilimanjaro, lakini asishangae kusikia kuwa bwawa hili ni la Mwanga. Kupambana na uvuvi haramu ni kazi ambayo mtu asipokuwa jasiri ataamua kuikwepa (kuipotezea) kwani ina wapinzani wengi; wengine watakuwa ni watumishi na hata viongozi wenye masilahi binafsi; kisiasa, kiuchumi ama hata kiharakati (watetezi wa watu bila kujali watu hao wamefanya nini). Namshauri asije akatumia ile mbinu ya kuungana kwa kushindwa ama kuona ugumu kupingana. Namwachia akiwa na boti ya kufanyia doria ambayo tumeikarabati na kuifufua siku ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka huu. Apambane kupata raslimali fedha kuendeleza vita dhidi ya Uvuvi haramu.

Advertisement