Dar es salaam ndiyo kwenye uamuzi wa mafanikio au kuangushwa

Wahenga walisema “siri ya mtungi aijuaye kata.” Mtungi hutumika kwa kuwekea maji, na hakika maji ya kwenye mtungi huwa ya baridi. Lakini mtungi huonekana kwa sura yake ya nje tu ambayo mara nyingine hupambwa na rangi na kuonekana maridadi.

Kata ndicho chombo ambacho hutumika kuteka maji toka mtungini, na ndicho chombo ambacho huingizwa mtungini na kujua hali iliyomo mle ndani, kama mtungi mchafu au msafi au una nyufa na kadhalika, kata ndio huwa na siri hiyo.

Kuna hadithi ambayo mimi na wadogo zangu wawili huwa tunacheka kila tukikumbushana, inafanana sana na mambo haya ya kata na siri za mtungi. Enzi ya ujana wetu ilifikia wakati tukawa wote tunavaa viatu saizi moja.

Siku moja mmoja wetu alikwenda kununua viatu vilivyokuwa vizuri sana, viatu vile vilikuwa ni vya aina iliyoitwa ‘bitoz’, kwani vilikuwa aina ya viatu ambavyo vilikuwa vikivaliwa na wanamuziki wa kundi la Beatles wakati ule. Viatu vile vilikuwa vyembamba mbele kwa staili iliyoitwa wakati huo ‘mkuki moyoni’.

Hakika tulipendeza sana kila tulipovaa nguo nzuri na chini tukawa tumevaa viatu vile. Katika safari zetu za kupishana kwenda kujipitisha mbele za nyumba ambapo pengine palikuwa na msichana tuliyempenda, au kuhudhuria mialiko ya sherehe mbalimbali tuligombea kuvaa viatu vile maana kulikuwa na uhakika kuwa lazima angetokea mtu na kuvisifia.

Lakini kulikuwa na siri kubwa sana kuhusu viatu vile. Vilikuwa ni vidogo kwa miguu yetu hivyo vilikuwa vinabana sana na kwa kweli muda wote ambapo watu walikuwa wakisifu utanashati wetu, miguuni ilikuwa maumivu makali, kila hatua ilikuwa ni maumivu makubwa sana. Tulivipa jina vile viatu tuliviita ‘adhabu’.

Nimekumbuka yote haya baada ya kuona video moja fupi ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa akihutubia katika mkutano mmojawapo nchini na katika mkutano huo, alitoa pongezi kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwa imeendeleza kuimarisha sekta zote.

Kutokana na maendeleo hayo, wasanii wa Tanzania wameanza kuwa maarufu Bara la Afrika, na filamu za Kitanzania zinaonekana kila mahali, baada ya hapo Mheshimiwa akatoa hongera kwa wasanii. Video hiyo ndio ikanikumbusha viatu vile tulivyoita adhabu, kila tulipopita tulisifiwa kumbe kila sekunde ni maumivu makali.

Hebu tuanze kuongelea sifa alizotupa mheshimiwa za kuanza kujulikana Bara la Afrika. Takwimu za mwaka 2008 zilizotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa zilionyesha kuwa wakati huo kulikuwa na wasanii milioni 6 nchini.

Hii ilikuwa ikijumlisha wasanii wa fani zote sanaa za ufundi, sanaa za maonyesho, muziki na filamu. Bila shaka idadi hiyo imeongezeka sana kwa sasa, sasa tujiulize ni wasanii wangapi wanajulikana nje ya Tanzania, wangapi wanajulikana kiasi cha kuweza kualikwa kwenye maonyesho katika nchi nyingine Afrika?

Ni nchi ngapi Afrika zimewahi kualika wasanii kutoka Tanzania? Wakifika wasanii hamsini waliowahi kualikwa kwa ajili ya maonyesho ya kibiashara katika nchi nyingine Afrika nitashangaa sana.

Na hao walioalikwa je, kujulikana kwao kuna tija kwao na kwa nchi yetu? Japo si mfano mzuri kulinganisha Uingereza na Tanzania, lakini tuangalie ripoti ya tarehe Aprili 29, 2019 iliyotolewa na chama cha Hakimiliki cha PRS cha Uingereza kuhusu fedha ambazo wanamuziki wa Uingereza wameingiza nchini mwao kutokana na mirabaha kutoka kazi zao nje ya Uingereza. Mirabaha iliingiza Pauni za Kiingereza milioni 281 sawa na Sh814 bilioni.

Tanzania ina chama cha Hakimiliki, Cosota, kila mtu anakilaumu hakifanyi kazi, wakati chama hicho hakijawahi kupewa fedha za kutekeleza kanuni yake inayoipa nguvu kudhibiti wizi wa kazi za sanaa, chama hicho hakijawahi kupewa fedha za kutosha hata kukusanya mirabaha katika jiji la Dar es Salaam tu, sembuse kuanza kupata makusanyo kutoka nje ya nchi?

Filamu zisizo halali zimezagaa nchi nzima, hivyo kwanza kulinyima Taifa pato na kwa kuwa zinauzwa kwa bei ndogo kutokana kuwa ni za wizi, pia zimeharibu kabisa soko la filamu za ndani, hali kadhalika soko la CD na DVD za muziki wa ndani liko hoi kutokana na mazingira mabovu ya biashara hiyo. Kweli siri ya mtungi aijuaye kata.

Ukipita Kariakoo utakuta maduka mengi yanayouza vifaa vya muziki ambavyo ndivyo vitendea kazi za wanamuziki, vifaa vyenye majina makubwa Yamaha, Roland, Behlinger na kadhalika vinapatikana katika maduka haya, ila jambo la ajabu bei ya vifaa hivyo unaweza kukuta ni ndogo kuliko bei ya vyombo hivyohivyo nchi ambako vinatoka, hii ni kwa kuwa asilimia kubwa ya vyombo hivi ni feki, wasanii tunaviita mafafa, hivyo ukinunua chombo kama hicho uhai wake ni kwa kudra ya Mungu. Sasa jaribu kufanya mbinu zako na kuagiza chombo original, ushuru wake unategemea anae kukadiria ameamkaje siku hiyo.

Microphone uliyonunua kwa dola mia mbili, unaweza kuambiwa ulipie ushuru wa dola mia nne. Kilio cha kurekebisha ushuru wa vifaa ambavyo ni vitendea kazi vya wasanii ni habari ya muda mrefu imeanza toka miaka ya 80.

Wasanii wachoraji wanalia ushuru wa karatasi, rangi, brashi na vifaa vingine vya kutekeleza kazi zao, tasnia ya filamu vifaa vyao. Lakini mkuu amesema mambo safi. Nakumbuka sana vile viatu tulivyoviita ‘adhabu’

Dar es salaam ndio kwenye uamuzi wa mafanikio au kuangushwa kwa wasanii. Ni kama vile nje ya Dar es Salaam hakuna wasanii, hata takwimu za awali za mwaka 2008 zinaonyesha kuwa wasanii ni wengi kuliko watu wote wa Dar es Salaam wakijumlishwa pamoja, sasa kwa nini msanii ili ufanikiwe lazima uwe ni wa Dar es Salaam au uje kutolea kazi zako Dar es Salaam.

Ni jambo la ajabu sana, angalia hata Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi huwa hawaongelei wasanii katika majimbo yao, wanakuwa wepesi kutetea haki za wasanii wenye majina tayari walioko Dar es salaam, ni kama vile majimboni kwao hakuna wasanii.

Ni miji mingapi ina maeneo maalumu kwa ajili ya sanaa, ni shule ngapi zinafuata syllabus iliyoko ya sanaa? Wakati wenzetu duniani kote wana shule za sanaa na hivyo kujenga tasnia zao tunataka tushindane nao kwenye soko la dunia kwa kudra za Mungu. Pamoja na sura nzuri na mavazi nadhifu kumbe wamevaa viatu vimebana

Kuwa na maendeleo pekee si kigezo cha kupata kura nyingi. Maendeleo yanatakiwa yalete furaha siyo yawe kwa gharama ya furaha.