TIBA MBADALA: Dawa za asili za vidonda vya tumbo zipo nyingi

Watu wengi hawajui kuwa vidonda vya tumbo husababishwa na mienendo mibaya ya maisha yetu na mfumo wa chakula cha kila siku.

Dawa kama Omeprazole, Tagament, Cimetidine na nyingine nyingi za hospitali huwa zinapunguza maumivu kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo.

Dawa hizi hupunguza asidi (tindikali) ambayo huharibu kuta za mfuko wa chakula.

Zinazuia asidi tu, bila kushugulika na chanzo cha kuongezeka kwa hiyo tindikali.

Kwa hiyo, bila kuondoa chanzo kinachosababisha kuongezeka kwa asidi hiyo, huwezi kupona.

Dawa za vidonda vya tumbo zinatakiwa zitumike pale panapohitajika tu, siyo maisha yako yote.

Kwa kawaida dawa za hospitali mara nyingi huja na maudhi mbalimbali kwa kuwa ni dawa ambazo zimetengenezwa kwa kemikali.

Dawa pekee ambazo ni rahisi na za uhakika na hazina madhara ni dawa asili.

Changamoto kubwa kwa hapa nchini ni kuwa huduma hii ya tiba asili bado haijapata wataalamu wengi waliobobea wa kutoa bidhaa bora na zenye kufanyiwa utafiti wa kutosha na zenye kiwango cha kimataifa.

Vidonda vya tumbo ni nini?

Ni kuharibika kwa ukuta wa tumbo la chakula na sehemu ya mwanzo ya utumbo mwembamba. Kuna aina kuu mbili za vidonda vya tumbo

1. Gastric ulcers-hivi hutokea kwenye mfuko wa tumbo la chakula.

2. Duodenal ulcers-hivi hutokea sehemu ya mwanzo ya utumbo mwembamba.

Chanzo cha vidonda vya tumbo ni kuongezeka kwa asidi kwenye tumbo la chakula.

Dalili za vidonda

Baadhi ya dalili za vidonda vya tumbo njaa kupita kiasi hasa usiku, tumbo kuwaka moto sehemu ya juu kwenye chembe, tumbo kujaa gesi, kuhisi kichefu chefu na kuharisha kutokana na kubagua vyakula.

Tiba asili ya vidonda vya tumbo

Kuna aina nyingi za dawa za vidonda vya tumbo tena zinazosababisha kupona kabisa.

Changanya mdarasini, khurinjani, tangawizi, habasoda na manjano. Vyote viwe na ujazo sawa kisha changanya.

Kisha chota kijiko kimoja na asali vijiko vitatu kisha weka kwenye glasi ya maziwa au uji na unywe kutwa mara tatu. Hakikisha hizo dawa unazipata zikiwa mpya.

Epuka dawa zilizokaa dukani miaka mingi, kwa kuwa hazina nguvu.

Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa tiba mbadala.