Dawa za kulevya bado tatizo kubwa Zanzibar

Wednesday October 3 2018

 

By Salim Said Salim

Tatizo la dawa za kulevya bado limeendelea kuwa sugu bara na visiwani, na hata hatua zinazochukuliwa hazionekani kulimaliza mojakwamoja. Ndio maana unahitajika ushirikiano wa dhati kati ya taasisi za serikali na watu binafsi katika kulitokomeza.

Kwa mara nyingine tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya na ukahaba uliokithiri katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar, mjini na vijijini, liliibua hisia kubwa za masikitiko katika Baraza la Wawakilishi.

Wajumbe walisema mbali ya kutafuta njia zitakazowasaidia waliotumbukia katika janga hili pamoja na familia zao, mkazo zaidi uwekwe wa kuwasaka wanaoingiza dawa hizi na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Wakijadili ripoti za utekelezaji wa kazi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ambayo inashughulikia masuala ya dawa za kulevya wawakilishi walisema baadhi ya watumiaji wa dawa hizi sasa ni tishio kwa maisha ya raia wema.

Kwa hiyo, walisema, ni vizuri wakakamatwa na kupatiwa matibabu na pia kupatiwa elimu itakayowarekebisha katika nyumba poa (sober hose) ili waweze kujirekebisha na hatimaye kurudia hali ya maisha inayokubalika katika jamii.

Mwakilishi mmoja alisema kama kweli wajumbe wa haki chombo cha kutunga sheria Zanzibar wanataka jamii ielewe kwamba wanapozungumzia suala la dawa za kulevya kauli zao ni za kweli basi ni vizuri kufanyika zoezi la kuwapima wajumbe wote wa Baraza kuhakikisha hakuna anayetumia dawa hizi hatari.

Hapo ndipo Baraza litapata imani ya wananchi kwamba wawakilishi hawafanyi utani wanapolaani matumizi ya dawa hizi hatari zenye kuleta athari kubwa kwa maisha ya jamii na nchi.

Mjadala huu mkali umekuja mwaka mmoja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, kueleza katika Baraza mkakati wa kuhakikisha watu wote wanaouza dawa za kulevya Zanzibar wanakamatwa.

Wakati ilipotolewa kauli ile palioonekana kufanyika juhudi kubwa ya kuwasaka watumiaji na wauzaji dawa za kulevya na kwa kiasi fulani hali ilibadilika na hata idadi ya vijana waliokuwa wakionekana wanasinzia ovyo katika vijiwe kupungua.

Muda mfupi baada ya kuanza kampeni tulipatiwa takwimu za watu waliokamatwa na idadi ya kesi zilizofunguliwa. Kwa bahati mbaya hili zoezi hivi sasa linaonekana limepwaya na hali kuonekana kurudia kama si kuzidi ile iliyokuwepo mwaka jana.

Hata upatikanaji wa hizi dawa ulikuwa wa taabu kubwa na zilikuwapo taarifa kwamba kutokana na upungufu mkubwa uliokuwepo bei yake nayo ilipanda.Wasiwasi ulioonyeshwa na wawakilishi unapaswa kuzingatiwa na kufanyiwa kazi na wananchi hawataki kusikia si kuambiwa kuwapo mkakati wa kuwakamata wanaoingiza na wanaouza hizi dawa hatari, bali kuona wanakamatwa, wanafunguliwa mashtaka na wanaoonekana na hatua wanawajibishwa kisheria.

Kwa kweli Wazanzibari wamechoka kuona maisha ya vijana wao wengi yanaharibiwa na matumizi ya dawa za kulevya na hao wanaoitwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao kwa kweli ni wauzaji wa dawa za mauaji na sio za kulevya ndio kwanza wanajitanua na kujitajirisha kwa kuharibu maisha ya watu, hasa vijana.

Ni vizuri kwa serikali kwanza kutoa mchanganuo wa kesi ziliofunguliwa, idadi ya kesi zilizomalizika na matokeo yake na maelezo ya kipi hasa kinakwamisha kukomesha biashara hii haramu kwa sehemu ndogo kama Zanzibar ambapo watu wake wanajiona vizuri na si taabu kama inavyokuwa kwa nchi kubwa kuwasaka wahalifu.

Hapana anayeweza kubisha kwamba katika kila mtaa na kijiji cha Unguja na Pemba watu wanazijua nyumba zinazouzwa dawa hizi na hao wanaoziuza.

Maeneo maarufu ya vijana wanaotumia dawa hizi ambayo yana majina ya nchi zilizokubuhu kwa kilimo na matumizi ya dawa hizi kama Peshawar au Colombia katika mji wa Unguja yanafahamika hata na vizee.

Ni kawaida kwa watoto hasa wa kike kukatazwa na wazee kupita baadhi ya sehemu hata nyakati za mchana kwa sababu ni maeneo hatarishi yenye vigenge vya watumiaji wa dawa za kulevya.

Ipo pia taarifa kwamba hata baadhi ya vilabu vyenye leseni ya kuuza pombe zilizoruhusiwa kisheria hutumiwa na wauzaji wa dawa za kulevya kama vituo vyao vya biashara hii haramu na hatari kwa maisha.

Waziri Aboud aliliambia Baraza mwaka jana kwamba serikali ilikuwa inafuatilia kwa siri wanaohusika na biashara hii haramu. Sasa umetimia mwaka mmoja tangu kutoa kauli yake ile katika Baraza la Wawakilishi.

Ni vizuri sasa akatueleza ule ufuatiliaji umepata mafanikio gani na watu wangapi waliokuwa wakifuatiliwa walibainika kuhusika na biashara hii haramu, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka na kesi zao zimefikia hatua gani.

Kinachoshangaza ni ipo shida gani ya kuwabana hata vijana wanaouza hizi dawa hatari ili waeleze wanazipata wapi na hatimaye kuwapata hao wanaowapa kuziuza?

Tatizo kubwa lazima tukubali ni kuwepo muhali na sababu za kila aina Visiwani zinazopelekea wanaofanya biashara hii haramu kuendelea kutanua misuli huku mamia ya vijana na hata baadhi ya wenye umri mkubwa kuendelea kuathiriwa na matumizi ya dawa hizi hatari.

Kikubwa kinachoonekana ni kunyoosheana vidole vya lawama na mara nyingi unaposikia wapo watu waliokamatwa kwa kuingiza nchini hizi dawa hatari haichukui muda mrefu utawaona watu hao wanatamba mitaani na kesi zao kumalizika kimyakimya.

Siku za nyuma ulisikia heka ya zisizoingia akilini za kueleza ati pipi walizokuwa nazo tumboni ni unga kama wa saruji.

Advertisement