Dawa za nguvu za kiume bila ushauri wa daktari ni hatari

Sunday June 10 2018Dk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Siku chache zilizopita, nikiwa kwenye idara ya wagonjwa wa dharura katika hospitali ninayofanyia kazi, ghafla tulipokea mgonjwa akiwa na hali mbaya kiafya.

Hakuonekana na majeraha yoyote hivyo hali yake haikusababishwa na ajali na ndugu waliomleta walisema alikuwa mzima lakini hali hiyo ilibadilika ghafla tu.

Moja kwa moja nikaanza kumchunguza mapigo ya moyo, kwa wakati ule yalionekana kuwa na kasi iliyozidi kawaida, na hata shinikizo lake la damu pia lilikua limepanda sana huku akihema kwa kasi japo alikuwa hajapoteza fahamu. Tukaendelea na jitihada za kuokoa maisha yake huku tukimuuliza nini hasa anadhani kilichomsababishia hali ile na kwa sauti ya upole alisema, “kwa kweli sina uhakika ni nini kimenisababishia hali hii japo nakumbuka muda mfupi uliopita nilikunywa vidonge kadhaa vya kuongeza nguvu za kiume sijajua kama hicho ndiyo chanzo au la.”

Kwa bahati mbaya jitihada za kuokoa maisha yake ziligonga mwamba, alipoteza maisha wakati tukiendelea kumpatia huduma ya dharura ya matibabu.

Awali ya yote, naomba ieleweke kuwa, dawa yoyote ile ikitumika kinyume au pasipo kufuata ushauri wa mtaalamu wa afya inaweza kuwa hatari kwa afya na hata kusababisha kifo na tunapokuja kwenye suala la dawa za kuongeza nguvu za kiume, dhana hii huthibitika zaidi.

Tatizo la kukosa nguvu za kiume kwa ujumla wake linakuja na sura tofauti lakini sura iliyozoeleka ya tatizo ni pale mwanaume anaposhindwa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu kwa sababu tu uume unashindwa kusimama na kudumu kwa muda mrefu na hatimaye kusinyaa kabla ya kumaliza kushiriki tendo la ndoa.

Jambo hili husababishwa na vihatarishi na matatizo mbalimbali ya kiafya kwa ujumla wake, lakini kwa ujumla, kusinyaa au kutosimama kikamilifu kwa uume wakati wa kushiriki tendo la ndoa kunatokana hasa na msukumo hafifu wa damu kwenye via vya uzazi.

Hivyo naomba ieleweke kuwa dawa hizi hazileti tiba ya kudumu kama wengi wanavyodhani, bali zinafanya kazi ya kuongeza kazi ya msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu iliyopo kwenye uume ili mwanaume aweze kushiriki tendo la ndio kwa wakati ule na utendaji kazi wa dawa hii huwa ni wa muda mfupi tu, hivyo mtumiaji atalazimika kutumia kila anapohitaji kushiriki tendo la ndoa.

Dawa hizi zimewekewa kiambata chenye kemikali aina ya sildenafil na hiki kina kiwango maalumu kinachotakiwa kuingia mwilini kutokana na hali ya kiafya ya mtumiaji husika na madhara kiafya ya dawa hii ndipo yanapoanza.

Kama nilivyoeleza awali, dawa hii inafanya kazi ya kuongeza kasi ya msukumo wa damu mwilini ili kulazimisha damu ifike kwenye uume na hatimaye uweze kusimama na kama tunavyofahamu, kazi ya kusukuma damu inafanywa na moyo hivyo dawa hii huulazimisha moyo kufanya kazi ya ziada na hivyo kuupa moyo hatari ya kupata matatizo kama vile kwenda kasi na hata kusababisha moyo kusimama, na kwa mwenye matatizo mengine ya kiafya kama shinikizo la damu, mtumiaji anakua hatarini, dawa hizi zinaweza kumsababishia kifo.

Watu wengi wamekuwa wakitumia dawa hizi kiholela bila ushauri wa wataalamu wa afya na hii ni hatari kwa kuwa wengi wamekuwa wakizitumia kiasi kikubwa kuliko afya zao zinavyoweza kuhimili na hii ni hatari.

Ni vyema kwanza kupatiwa vipimo vya afya kama kupima kasi ya mapigo ya moyo na shinikizo la damu ili kushauriwa kiwango stahiki cha dawa kulingana na hali ya kiafya. Nashauri pia kama una tatizo la kukosa nguvu za kushiriki tendo la ndoa ni vyema kwanza kuwaona wahudumu wa afya ili kupata msaada wa utatuzi wa tatizo kuliko kuvamia dawa hizi bila ushauri wa daktari.

Advertisement