Dhima ya tahajia katika uandishi

Tuesday August 21 2018

 

Inawezekana istilahi hii ‘tahajia’ ni ngeni kwa baadhi yetu ingawa kimatumizi inatumika mara nyingi.

Wengi wamezoea kutumia neno la Kiingereza ‘spelling’ badala ya neno la Kiswahili ‘tahajia’. Tahajia ni uwakilishaji wa sauti kwa herufi katika maandishi kufuatana na mwendelezo wa maneno uolikubalika.

Kila neno katika lugha lina tahajia sahihi zilizokubalika. Kwa mfano, neno ‘sayansi’ linaundwa na tahajia ‘s-a-y-a-n-s-i’. Kila herufi hapo ni tahajia ya neno hilo. Maneno ya lugha hupatikana katika kamusi.

Aidha, ili kuweza kuwa na uhakika kuhusu kamusi yenye maneno sanifu ya lugha, ni vizuri kutumia kamusi zenye ithibati kutoka mamlaka husika za lugha.

Katika uandishi au mitindo ya uzungumzaji rasmi, maneno yatumiwayo hayana budi kuwa na tahajia sahihi. Endapo tahajia hizo zitakuwa tofauti, basi mwandishi au mzungumzaji anaweza kupata changamoto kubwa ya kutoeleweka kwa hadhira yake.

Jambo la msingi kabla ya kuandika, mwandishi ahakiki msamiati anaotaka kuutumia. Akiwa na shaka kuhusu tahajia za baadhi ya maneno au msamiati huo, arejelee kamusi kwa ajili ya kufanya uhakiki.

Kila mwandishi hana budi kukumbuka kuwa, ingawa wazungumzaji wa Kiswahili wanaweza kutamka maneno kwa lafudhi na matamshi tofauti na inavyotakiwa kulingana na taratibu za lugha ya Kiswahili, kasoro hiyo haitakiwi kujitokea katika maandishi.

Hii ni kwa sababu kwa kiasi fulani, athari za lugha mama katika lugha ya mazungumzo kwa upande wa lafudhi haziepukiki. Hata hivyo, ni vyema kuandika kwa kufuata taratibu za lugha ili ujumbe uweze kuwafikia walengwa.

Ikiwa msamiati uliotumika katika uandishi una makosa ya kitahajia, ni wazi kwamba ujumbe wa kazi hiyo hautawafikia walengwa vile ipasavyo na kazi hiyo haitakuwa na mvuto wa kusomwa na walengwa.

Kama tulivyokwishaeleza hapo awali, kipimo kizuri cha kujua tahajia za maneno katika lugha ni kutumia kamusi ya lugha husika iliyothibitishwa na mamlaka husika za lugha.

Tusisitize kuwa kila mwandishi ana wajibu wa kuhariri tahajia za msamiati alioutumia katika andiko lake kabla ya kuitoa rasmi kazi hiyo isomwe na walengwa. Tahajia ya msamiati uliotumika ikiwa na kasoro, ujumbe uliokusudiwa hautowafikia walengwa kwa kuwa tahajia ina tabia ya kuathiri uelewekaji wa kazi iliyoandikwa kwa wasomaji. Matumizi ya msamiati ndiyo yanayomwelekeza msomaji kuelewa kusudio la mwandishi.

Baadhi ya maneno ambayo tahajia zake hubanangwa na baadhi ya waandishi ni kama vile: mrabaha (mrahaba), mstari (msitari), teremka (telemka), thibitisha (dhibitisha), thamani (dhamani/samani), dhibiti (thibiti) na kadhalika. Maneno kwenye mabano yanapotumiwa na waandishi wakati wanapokuwa na lengo la kutumia maneno yasiyo kwenye mabano, utumiaji huwakanganya wasomaji na kuwafanya wasielewe ujumbe uliokusudiwa na waandishi.

Tahajia kwa yenyewe ni ndogo sana lakini inapoachwa kutumiwa au kukosewa katika uandishi wa neno, athari yake ni hasi na kubwa katika uelewekaji wa ujumbe huo. Mathalani, mwandishi anapokusudia kuandika neno ‘shinda’ halafu akaandika ‘shida’ tayari atakuwa amebadili ujumbe aliokusudia kuuwasilisha, au atakapoandika ‘Samani ya mali zote ni shilingi milioni kumi,’ badala ya kutumia neno ‘thamani,’ hadhira yake haitomwelewa.

Ikumbukwe kwamba, lengo la andiko lolote ni kutoa ujumbe fulani unaoeleweka. Ili ujumbe huo uweze kuwafikia walengwa, mwandishi hana budi kuandika kwa umakini mkubwa. Anapaswa kuzingatia taratibu zote za uandishi na usahihi wa maneno, huku akimakinikia tahajia za maneno yote aliyoyatumia.

Advertisement