UCHAMBUZI: Dini nyingi ni sawa, vyama vingi hapana

Haijawahi kutokea. Viongozi wa dini mbalimbali kutinga Ikulu kwa pamoja. Imetokea wiki iliyopita mbele ya chuma Rais John Magufuli. Akitaka wawe huru kusema lolote juu ya Taifa. Bonge moja la fursa na huenda imetokea Bongo tu tangu dunia iumbwe.

Ni wazi kwamba chanzo cha uvunjifu wa amani kwa Afrika, ni siasa na dini. Sababu ikiwa maslahi binafsi au ya kikundi cha watu badala ya kitaifa. Fuatilia vita zilizopiganwa. Sasa viongozi wa dini zote kubwa na ndogo kukutana pamoja kwetu ni jambo la pekee.

Linatokea hili kipindi ambacho baadhi ya Watanzania, kuanza kupandikiza chuki miongoni mwetu. Kama mazuzu tunazoea misemo ya sisi na wao. Sisi Waislam wale Wakristu. Wale Wasukuma sisi Wachaga. Tangu izaliwe nchi yetu neno ‘sisi na wao’ limekemewa sana na wazee wetu.

Tokea Julius akiwa Magogoni pale. Ilikuwa vigumu kufanya Wabongo wararuane kwa ukabila au siasa. Kitu chepesi ambacho kingewatenganisha hata kufanya watandikane ni udini. Lakini, kikao cha juzi Ikulu kinakupa picha kwamba mambo yamebadilika. Dini siyo tatizo tena.

Kama viongozi wake wanaweza kukutana sehemu moja na mambo yakaenda vizuri. Tatizo hivi sasa linabaki kwenye siasa, kwani huku ndio rahisi sana kuwatenganisha Wabongo hata wakaweza kuvunjana. Fuatilia mihemko ya kisiasa mitaani na mitandaoni.

Tuna kabila kibao. Lakini lugha ni moja. Tuna dini nyingi. Bado upendo wetu umetamalaki. Tuna vyama vingi, lakini chuki ina nafasi kubwa mbele ya itikadi sera na ilani ya vyama husika. Kuna chuki inatengenezwa waziwazi na viongozi au wafuasi.

Kama taifa hatuwezi ongozwa na kabila moja. Wala kuendeshwa na dini moja. Inawezekana vipi tuongozwe na chama kimoja? Yaani chama kimoja kibebe ajenda zote za kitaifa bila uwepo wa vyama vingine? Hata katiba yetu inakataa.

Ulikuwepo ubaguzi wa kidini kabla ingawa haukuwa wazi. Sasa kuna ubaguzi au chuki ya wazi kwenye siasa zetu. Kukaa bila kusema ni kulisaliti taifa lako. Chuki ya kisiasa inamea kwa kasi zaidi kuliko ukuaji wa uchumi kwa taifa. Chuki ndani na nje ya vyama.

Ukweli ni kwamba waliopo madarakani hawajakubali kwa dhati uwepo wa upinzani. Tofauti ya fikra, mtazamo, maono na sera zimeifikisha dunia katika maendeleo haya tuyaonayo. Kuamini katika akili na mtazamo wa aina moja tu tutakuwa binadamu mfu.

Kama viongozi wa dini zote wamekutana sehemu moja. Licha ya tofauti za kimtazamo kidini. Lakini, wameongea matatizo ya kijamii kwa pamoja. Kiroho safi. Inakuaje ishindikane kwa wabunge kuisemea jamii bungeni badala ya itikadi chuki na kusutana kivyama?