Dk Bashiru: Kura za maoni hazitashirikisha wengi CCM

Msimamo alioutangaza Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ally wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kegara, kwamba kura za maoni hazitashirikisha watu wengi, ni vizuri ukapewa tafakari ya kutosha na wanachama ili wachukue mapema hatua kwa kujiandaa kisaikolojia.

Msomi huyo wa Sayansi ya Siasa alisisitiza kwamba mfumo wa uteuzi ndani ya chama umebadilika na kuwa sasa hautashirikisha watu wengi kama ilivyokuwa zamani.

Anasema utakuwepo “utaratibu mzuri” utakaowezesha kuwapata wagombea wenye sifa kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama.

Kwamba “chama kitahakikisha mchujo unasimamiwa vizuri ili kuwapata wanachama safi wa CCM,” anaongeza.

Dk Bashiru anaukosoa mfumo uliopita akisema ulihusisha matumizi ya fedha, kununua kadi na siasa za upendeleo kwa baadhi ya wagombea.

Kama hivi ndivyo, wanachama wanaotarajia kutetea nafasi za uteuzi kupitia chama hicho wakati huo wakiwa zao la mfumo unaolalamikiwa bila shaka hatima yao kisiasa iko njia panda.

Kupitia utaratibu mpya ambao hautahusisha wanachama wengi kama sauti ya mwisho ya kupitisha mgombea, vigogo wengi kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, udiwani na ubunge wajiandae kupukutishwa.

Nguvu kubwa ya CCM inatarajiwa kuwekezwa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaopangwa kufanyika baadaye mwaka huu ili kujenga msingi wa kufanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Pamoja na kuwapo mambo mazito namna hiyo haikushangaza kwamba kuna wanachama wa CCM waliosafiri hadi Kijiji cha Kanazi Wilaya ya Bukoba kumuona katibu mkuu na kutumia nafasi hiyo kumwambia mambo mepesi.

Baada ya siku chache za mapumziko na ziara Dk Bashiru alikuwa amepata taarifa za uongo na kweli kuhusu wanachama na mienendo yao, ingawa kimsingi siasa za majungu hazikuwa sehemu ya ziara yake.

Tahadhari Bukoba Vijijini

Tangu kung’olewa kwa Nazir Karamagi kupitia kura za maoni na Jasson Rweikiza kuchukua nafasi yake Jimbo la Bukoba Vijijini halikuwahi kutulia baada ya kuibuka migogoro ya kisiasa yenye mtazamo tofauti kuhusu vigogo hao.

Baada ya Karamagi kuonekana kama amejiweka kando na siasa, vita ya kisiasa imehamia kwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Murshid Ngeze na hivyo kusababisha mpasuko miongoni mwa madiwani.

Pamoja na mambo mengine, msuguano wa Mbunge na Mwenyekiti hauwezi kutenganishwa na vita ya kuwania sehemu ya kujenga makao makuu ya Wilaya ya Bukoba na hospitali ya Wilaya hiyo kongwe.

Ni nadra madiwani wa CCM kuwa na kauli moja na wale wa upinzani na kusaini barua moja ya kuonyesha kutokuwa na imani na mwenyekiti wa halmashauri, lakini hawa walifanya hivyo na kupeleka malalamiko hayo kwa mkurugenzi kama hatua ya kudai mchakato mpya.

Dk Bashiru wakati wa kuhitimisha ziara yake mkoani Kagera alionyesha kuufahamu vema mgogoro unaoendelea katika wilaya hiyo anayotoka na kulazimika kufanya upatanisho.

Mbele ya Katibu Mkuu, viongozi hao walitangaza kumaliza tofauti zao na alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kujitenga na mchakato wowote unaohusisha barua iliyosainiwa na madiwani na kuwa kama kuna ulazima, suala hilo lipelekwe kwenye chama.

Wote wawili walishikana mikono kama ushahidi wa kumaliza tofauti zao. Hata hivyo hakuna mwenye uhakika kama makundi yanayounga mkono viongozi hao kama nayo yamekufa au yataendelea kuparurana kimyakimya.

Utata soko la kahawa

Wakati zao la kahawa lina ushawishi mkubwa katika siasa za Kagera, Dk Bashiru Ally alisema ana taarifa kuwa kahawa bado ipo kuwa kwa wakulima na wengine waliouza hawajapata malipo yao.

Hata wakulima hawajui nini hasa kinachoendelea kuhusu malipo yao kwa kuwa viongozi wamekuwa wakitoa kauli zinazotofautiana.

Kiongozi huyo anasema kuna utekelezaji mzuri wa ilani kwenye mazao ya biashara ingawa soko la kahawa lina changamoto.

Kwamba makosa ya sasa ambayo kimsingi yanamgharimu mkulima yatumiwe na viongozi kufanya maandalizi ya ununuzi wa kahawa kwa msimu ujao na kushauri pia nguvu zielekezwe katika utafiti wa masoko.

Aruka mashimo

Pamoja na mengi aliyofanya, kuna mengine muhimu yanayoifanya ziara yake isikamilike kwa kuwa hakuyatolea msimamo hadharani labda kama alifanya hivyo kwenye vikao vya ndani.

Vyovyote iwavyo kukwama kwa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi ambao ni mradi mkubwa wa kiuchumi, ambao mkwamo wake unahusisha viongozi wa ndani na nje ya chama, litaendelea kuwa tatizo.

Pia ujenzi wa soko la Bukoba ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kiuchumi iliyoibuliwa na chama hicho miaka michache iliyopita ingawa utekelezaji wake umekuwa mgumu zaidi hasa baada ya chama hicho kupoteza kiti cha umeya Manispaa ya Bukoba na ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini.

Vikwazo vya utekelezaji wa miradi hii vimesimikwa kwenye maslahi ya wanasiasa kuliko mahitaji ya wananchi ambao wamechoka kupata huduma za usafiri kwenye stendi ya tope.

Utekelezaji wa ilani kwa maana ya Mkoa wa Kagera hautakiwi kuzungumzwa kwa ujumla, bali wananchi wanatakiwa waelezwe jitihada zilizopo katika kufanikisha vipaumbele vyao.

Pengine kwa kujua aibu iliyopo Dk Bashiru hakupitishwa katika kituo cha mabasi cha Bukoba na soko kuu badala yake alitembelea shule ya Sekondari ya Ihungo alikosomea ambayo imejengwa upya baada ya tetemeko la ardhi na akasifia miundombinu yake.

Mapokezi ya katibu mkuu yaliambatana na tukio la kumsimika kuwa mtemi, kazi waliyokabidhiwa wazee watatu ambao walimvika nguo ya gome la mti (olubugu) na kumkabidhi silaha za jadi tayari kwa mapambano.

Matukio ya kuwasimika viongozi kimila katika majukwaa ya kisiasa yameshika kasi katika maeneo mengi na mara nyingi wanaosimikwa huwa hawajishughulishi kwa lolote na masuala yanayoendana na majoho waliyobebeshwa.

Viongozi hao hupewa majukumu bandia ya kusimamia mila na tamaduni na mara nyingi wanapoondoka kwenye nafasi zao husahau kila kitu kuwa wamewahi kupewa utemi na suala hili linatakiwa lifanyike kwa uzito wake badala ya msukumo wa siasa.

Ziara ya Dk Bashiru mkoani Kagera inatoa fursa ya wanachama kujitathimini kama waliwasilisha ajenda zao kwa maslahi ya wengi au mambo mepesi yenye hila na ajenda binafsi.