DK Bashiru ampinga RC Chalamila kuhusu Tanzania kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja cha siasa

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewashangaa baadhi ya wanachama wa chama hicho wanaompigia chapuo Rais John Magufuli kuendelea kuongoza hata baada ya kipindi chake kuisha.

Dk Bashiru, aliyekuwa anazungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dodoma wiki iliyopita, alisema kukubali jambo hilo litokee ni kuvunja utaratibu wa chama uliokuwapo tangu enzi za muasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere.

“Rais Magufuli atafanya kazi ya miaka mitano na ataomba ridhaa nyingine afikishe miaka 10, tuache kuwa wanajimu,” alisema msomi huyo aliyebobea katika sayansi ya siasa.

Katika hoja hiyo, alitoa mfano wa kauli tata ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila aliyesema anatamani kibaki chama kimoja cha siasa kitakachoitwa “Magufuli Ruling Party”.

Pamoja na kwamba Rais Magufuli alimjibu Chalamila palepale kwamba angependa viwepo vyama vingi, lakini CCM ndiyo iwe inashinda, Bashiru anasisitiza kuwa kauli hiyo ya mkuu wa mkoa si msimamo wa chama.

“Hata Tume ya Nyalali wakati ya kupata maoni juu ya mfumo wa kisiasa, ilikusanya maoni asilimia 80 walitaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja, lakini asilimia 20 walitaka vyama vingi, lakini CCM ikaamuliwaa viwepo vyama vingi,” alisema.

Dk Bashiru anasema kwa kauli hiyo Chalamila, ambaye alikuwa mwanafunzi wake katika masomo ya sayansi ya siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anapaswa kurudishwa tena darasani kufundishwa siasa.

“CCM tuna mkakati wa kuanzisha vyuo vya siasa kwa ajili ya kuwapika vijana ambao watasaidia katika masuala ya uongozi. Tayari nimeshawasilisha jina la mkuu huyu wa mkoa awe miongoni mwa wanafunzi wa kwanza watakaofaidika na elimu hiyo,” alisema.

Mbali na kauli hiyo, baadhi ya wanasiasa, hasa wabunge wa CCM wamekuwa wakipendekeza Rais Magufuli ama aongezewe muda au uchaguzi wa 2020 usifanyike ili aendelee.

Wabunge ambao wamewahi kutoa kauli hiyo ni Juma Nkamia (Chemba) na Livingstone Lusinde wa Mtera.

Akizungumzia siasa za ushindani, Dk Bashiru alisema bado CCM inaheshimu mfumo wa vyama vingi kwa kuwa unapanua uwezo wa kufikiri.

“CCM hatutatamani wala kupanga siku moja kuua upinzani,” aliongeza Dk Bashiru ambaye hivi karibuni atatimiza mwaka mmoja tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

Mali za CCM

Dk Bashiru, ambaye mwaka 2017 aliongoza kamati ya kufuatilia na kuhakiki mali za CCM kote nchini, alisema walibaini wizi, ubadhirifu, rushwa na ufisadi mkubwa katika mikataba ya majengo, likiwamo Jengo la Umoja wa Vijana (UVCC) na lililokuwa jengo la Umoja wa Wanawake (UWT) ambalo sasa limejengwa jengo la Airtel.

“Hakuna mkataba ambao utaachwa, tumebaini upotevu mkubwa wa mali za CCM uliosababishwa na mikataba mibovu,” alisema.

Kumuenzi Nyerere

Dk Bashiru pia alizungumzia Mwalimu Nyerere ambaye mwaka huu anatimiza miaka 20 tangu afariki dunia akisema Watanzania wanapaswa kumuenzi kwa staha na kuyafanya yale yote mazuri ambayo aliyaanzisha.

“Nawaombeni mtumieni taaluma yenu mwaka 2019 kutangaza, kuchambua na kueneza kazi za Mwalimu Julius Nyerere, maisha yake na fikra zake,” anasisitiza.

Hata hivyo, Dk Bashiru anasema si vyema kuandika kama kasuku na kumtaja Baba wa Taifa kama mtukufu kwa kuwa alikuwa ni binadamu, hivyo anaweza kuwa na mapungufu yake.

“Mumtangaze kwa mazuri yake kwa heshima, kuna vijana wengi wataandikishwa kupiga kura lakini hawajui historia ya Taifa hili,” anasisitiza.

Uhuru wa kiuchumi

Dk Bashiru pia alizungumzia changamoto na vikwazo vya maendeleo na kueleza uhuru wa nchi hauwezi kukamilika bila kupambana na uhuru wa kiuchumi.

Anasema mapambano ya uhuru wa nchi ni ya kudumu na yanahusu uhuru wa nchi na watu wake.

“Katika umasikini tulitoa michango kutafuta uhuru wa watu wengine kwa kufahamu binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja,” anasema

Hata hivyo, anasema bado kuna watu wachache wanufaika lakini lazima uhuru utafutwe ili kutafuta usawa

CCM na uchaguzi mkuu

Akizunguzia CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, Dk Bashiru anasema CCM itaendelea kuwa imara ili kuweza kuwa na serikali imara.

“Tuliambiwa chama legelege huzaa Serikali legelege hivyo ni lazima CCM iendelee kujenga utamaduni wa kujiimarisha,” anasema.

Anasema mtu yoyote ambaye anajiandaa kununua kura kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao ajue anajiandaa na vita kali.

“Mimi sihongeki, mwenyekiti wetu haongeki,” anasema.

Vilevile, alisema “Hakuna mtu yoyote ambaye akiondoka CCM itakufa, kwani ingekuwa kufa CCM ingekufa wakati ameondoka Nyerere.

Nafasi yake kisiasa

Dk Bashiru, anasema akiondoka katika nafasi hiyo hatashika cheo chochote cha kuteuliwa, atarudi kushika chaki.

“Hiki cheo changu cha mwanzo na mwisho, sikubebwa na sitambeba mtu,” anasema.

Anasema kazi iliyopo mbele yake na viongozi wengine ni kuendelea kujenga umoja ndani ya chama na kuondoa wanaotafuna nchi kwa maslahi yao.

“Mimi sijaingia CCM na fikra mpya, CCM ina ilani yake na hakuna mgongano kati ya Bashiru na historia ya CCM,” anasema.

Anasema kuna minong’ono mingi kuhusu yeye, lakini ijulikane kwamba yeye ni mtumishi tu, tena wa kuteuliwa na ataondoka kama alivyoingia.

“Kazi yangu ni kusimamia chama kikubalike kwa umma,” anasema.

Wagombea Zanzibar

Akizungumzia wanaojipitisha kugombea wa urais, Zanzibar, anasema hivi sasa kuna mpasuko Zanzibar, wanaotaka Rais wa Unguja Kaskazini, Unguja kusini, urais wa Pemba na Zanzibar Bara

Hata hivyo, anasema chama hicho kina taratibu zake za kupata viongozi.