Dk Nshala: Nchi inaongozwa kwa matamko ya wanasiasa

Sunday April 14 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Rais mpya wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk Lugemeleza Nshala amesema nchi imekumbwa na tatizo la kuongozwa kwa matamko ya viongozi wa Serikali badala ya kufuata utawala wa sheria.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi jijini Dar es Salaam, Dk Nshala aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni katika mkutano mkuu wa TLS uliofanyikia Arusha hivi karibuni alitoa mfano wa wakuu wa mikoa na wilaya akisema wamekuwa wakiingilia hata uamuzi wa mahakama, jambo alilosema ni kinyume cha Katiba.

“Nchi yetu ni ya kidemokrasia, inaongozwa na sheria na Katiba na viongozi wote kuanzia Rais hadi viongozi wa chini wamekuwa wakiapa kuwa wataitii kuhifadhi na kutetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Sasa kumekuwa na mtindo kwamba matamko ndiyo yanaongoza nchi. Unajiuliza kiongozi anatamka kwa sheria gani? Mkuu wa wilaya anaweka mtu ndani, sawa tunajua kuna sheria ya wakuu wa wilaya, lakini kwa kosa gani?” alihoji Dk Nshala.

Aliendelea, “Kwa sababu tunajua ni lazima mtu atende kosa la kushitakiwa ndipo awekwe ndani, lakini mtu anakuweka ndani saa 24 au saa 48 ili umtambue au ujue yeye ni mkubwa wako.”

Huku akisisitiza utawala wa sheria, Dk Nshala alisema kumekuwa na tabia ya viongozi wa Serikali kuingilia migogoro iliyofikishwa mahakamani na kuitolea matamko.

“Kiongozi hata kama una nia njema kiasi gani, huna mamlaka ya kuamua mgogoro ulioko mahakamani. Kama haujafika mahakamani, mtu yoyote anaweza kusuluhisha. Lakini ukisha kwenda mahakamani, acha taratibu zifuatwe,” alisema.

Suala la wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu mahabusu hovyo limeshakemewa na mawaziri kama Selemani Jafo (Tamisemi), Ummy Mwalimu (Afya) na George Mkuchika (Utumishi na Utawala Bora) wakisema tabia hiyo ni kukiuka misingi ya utawala bora.

Huku akitoa mfano wa tathmini za mazingira, Dk Nshala alisema viongozi wamekuwa wakitoa matamko bila kujali ushauri wa kitaalamu na sheria husika.

“Kama Sheria inaagiza ifanyike tathmini ya athari za mazingira lazima ifuatwe, kwa sababu athari yake ni kubwa sana, inaweza kuhatarisha maisha ya watu,” alisema na kuongeza:

“Sasa tukiamka tu tukasema huu mradi lazima uwepo, msimkwamishe, maana yake kuna sheria ya mazingira ya 2004 bado ipo, nani ametoa madaraka?”

Alisema tathmini ya mazingira hailengi kukwamisha miradi bali inalenga kuhakikisha mradi umefikiriwa kwa makini.

Kuhusu uhuru wa Mahakama, Dk Nshala alisema kumekuwa na ukaribu kati ya viongozi wa Mahakama na viongozi wa Serikali jambo alilosema linaondoa imani ya wananchi kwa mhimili huo.

“Mahakama ndiyo chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kuamua migogoro ya watu na kutoa haki kati ya jamii, hiyo ni ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Sasa ukianza kukipa amri au maelekezo basi unaondoa imani ya wananchi. Au chombo hicho kikionekana kuwa karibu au watu wake kama majaji au Jaji Mkuu wanaonekana kuwa karibu na Dola unaanza kupunguza imani bila kujijua,” alisema Dk Nshala.

Alisema licha ya Rais kuwateua majaji wa mahakama, lakini akishawateua hatakiwi kuwaingilia katika utendaji wao.

“Lakini, sasa kumekuwa na tabia tunayoiona pengine viongozi hawa amekuwa karibu na sherehe za Serikali unashindwa kutofautisha kama hii ni shughuli ya Serikali kama Serikali au ni shughuli ya mahakama,” alisema.

Aliendelea, “Ikiwa ni sherehe za uhuru haina shida, kuzinduliwa Bunge haina shida, siku ya sheria haina shida, kuapisha majaji haina shida, lakini ndege zinapokelewa, sijui kuna mradi gani unafunguliwa, kunakuwepo Jaji Mkuu pale wanakuwepo majaji kule Ikulu wakati mawaziri wanaapishwa.

“Inaonekana kana kwamba mahakama na majaji wetu ambao kwa kweli wanatenda kazi zao kwa uadilifu. Lakini, mwananchi wa kawaida anaweza kusema hawa watu mbona wako karibu na aliyewateua? Kuna msemo usemao ‘Perception trumps reality’ kwamba haki siyo tu itendeke, bali pia ionekane ikitendeka.”

Miongoni mwa matukio yaliyohudhuriwa na kiongozi wa Mahakama ni pamoja na tukio la kuapishwa kwa mawaziri baada ya Rais John Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Wizara za Kilimo, Viwanda na Biashara, Tamisemi na Utumishi, Novemba 12, 2018.

Katika tukio hilo, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alisema mabadiliko yanaigusa Mahakama.

“Ushauri ni kwamba karne ya 21 ni shindani, kwa hiyo shughuli zote ni shughuli zenye ushindani mkubwa sana. Kilimo kinahitaji ushindani, wananchi wana matarajio makubwa sana kwa hivyo watahitaji ushindaji wa hali ya juu,” alisema Jaji Mkuu Profesa Juma.

Kuhusu mabadiliko ya Sheria ya madini ya mwaka 2017, Dk Nshala ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria watetezi wa mazingira (Leat) alisema licha ya ubora wa sheria hiyo, bado imeshindwa kutoa suluhisho la mikataba iliyoingia na kampuni kubwa za madini.

“Hakujawahi kuwa na mchakato mzuri wa kutunga sheria ya madini na sisi kujua kama nchi tunataka kujua tupate nini katika madini na kuongozwa na falsafa gani” alisema.

“Mwaka 2017 tulikuja na sheria nzuri, lakini yale mambo ya nyuma tunaondokana nayo vipi? Kwamba ile mikataba tuliyosaini ya kugawa rasilimali tunaondokana nayo vipi?” alihoji.

Alisema mikataba hiyo iliweka masharti ya kutovunjwa, hivyo ameshauri Serikali ikae na kampuni za madini ili kujadiliana jinsi ya kuachana nayo salama.

Hata hivyo, alisema sheria hiyo mpya ni nzuri kwa kuwa sasa imezuia kusaini mikataba mingine na imeweka masharti ya uchimbaji wa madini kwenye leseni na ikiwa utatokea mgogoro. Utaamuliwa nchini badala ya kwenda kwenye mahakama za kimataifa.

Wasifu

Dk Lugemeleza Nshala, Wakili wa kujitegemea

Umri: Miaka 53

Historia. Alizaliwa Juni 19, 1966 wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera.

Elimu. Mei 2005 hadi Mei 2012 alisomea shahada ya uzamivu (PhD) Chuo Kikuu cha Havard Cambridge, Massachusetts nchini Marekani. 2004-2005 na 2006- 2007 shahada ya uzamivu New Haven, Connecticut nchini Marekani. Shahada ya uzamivu Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani. Shahada ya kwanza 1989-1993 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uzoefu wa kazi. Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wanasheria watetezi wa Mazingira (Leat) tangu Desemba 2012. Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha watetezi wa Ardhi (TALA) na anayo kampuni ya uwakili ya Rugemeleza Nshala Advocates. Mhadhiri wa vyuo mbalimbali duniani akifundisha masuala ya sheria ma mazingira.

Advertisement