ELIMU &MALEZI : Mbinu za kumjenga mwanao ajiamini

Tuesday January 22 2019

 

By Christian Bwaya

Maisha yanahitaji ujasiri. Mtu asiyejiamini ni vigumu kufanya jambo kubwa na likafanikiwa. Ni hivyo kwa sababu ukishakosa hali ya kujiamini wewe mwenyewe hata wengine wanaokuzunguka wataanza kuwa na wasiwasi na uwezo wako.

Lazima ujiamini ili watu wengine wawe na mahala pa kuanzia wanapofikiria kufanya kazi na wewe.

Mtoto jasiri, kwa mfano, huwa na uthubutu wa kufanya vitu vipya bila hofu ya kukosea. Unapompa nafasi ya kufanya kitu, anakifanya bila wasiwasi tofauti na mtoto mnyonge asiye na imani na kile anachojaribu kukifanya.

Ingawa imejengeka dhana kuwa wapo watu huzaliwa wakijiamini, watalaam wa tabia wanasema kujiamini ni matokeo ya malezi. Sote, bila kujali jinsia, kabila wala kiwango cha elimu tunaweza kukuzwa kwa namna inayojenga ujasiri wetu. Mahali pa kuanzia ni malezi. Lazima kuanza mapema kujenga ujasiri wa wanetu.

Ili mtoto ajiamini lazima kwanza ajenge mtazamo chanya na maisha. Hapa tuna maana ya kuamini kuwa yuko kwenye mazingira salama, anaishi na watu wanaoaminika na kwamba hana sababu ya kuwa na wasiwasi na maisha yake. Bila mtazamo huu chanya, ni dhahiri mtoto atakosa ujasiri na mazingira anamoishi na matokeo yake hatoweza kuwa na uthubutu wa kudadisi na kutafuta majibu ya changamoto zinazomkabili.

Mtazamo chanya, kwa bahati nzuri, unajengwa na wazazi kwa ushirikiano na watu wengine wanaoishi na mtoto. Wazazi, kwa mfano, wanahitaji kuyaelewa mahitaji aliyonayo mtoto na kuhakikisha kuwa mahitaji hayo yanapatikana. Mtoto asiye na wasiwasi na mahitaji yake ni rahisi kujiamini.

Lakini pia, ni muhimu wazazi kumshirikisha mtoto kwenye shughuli ndogo ndogo zinazolingana na umri wake. Shughuli hizi, hata hivyo, ni muhimu zimsaidie mtoto kutatua vikwazo vinavyomkabili. Katika mazingira ambayo mtoto anapewa nafasi ya kushiriki kufanya vitu bila kukosolewa, wazazi wanakuza hali ya mtoto kujiamini.

Aidha, maneno anayoambiwa mtoto nayo yana nguvu kubwa ya kujenga kujiamini kwake. Mzazi, mathalani, anahitaji kuonyesha kuwa ana imani na uwezo alionao mtoto.

Kisaikolojia unapomwamini mtu unamfanya apambane kuwa vile unavyoamini. Mtamkie mtoto maneno chanya yatakayoumba msisimko wa kuamini anaweza. Mwambie ana uwezo wa kufika mbali badala ya kumkatisha tamaa. Neno baya, hata pale linapotamkwa kiutani linaweza kumnyong’onyeza mtoto na kujenga hali ya kutojiamini.

Walimu, nao kwa upande mwingine, lazima waangalie namna gani wanawafundisha watoto. Kazi ya ualimu ni zaidi ya kuhakikisha watoto wanapata alama za juu darasani.

Mwalimu mzuri hufanya kazi ya kumjenga mtoto kisaikolojia aamini anaweza. Je, kazi ambazo walimu wanawapa watoto darasani zinawajengea kujiamini? Vipi watoto wanapokosea? Hatua zinazochukuliwa kwa watoto wasiofanya vizuri darasani zinawasaidia? Je, walimu wanawasaidia watoto kujikosoa bila kuwafanya wakose imani na uwezo wao?

Advertisement