Fahamu faida za mazoezi mepesi

Friday May 10 2019

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa ili kuwa na afya njema na kujenga mwili imara unahitajika kufanya mazoezi mepesi kwa dakika 150 kwa wiki yaani kwa siku dakika 30 katika siku tano za wiki.

Lakini je, ni wafanya mazoezi wangapi wanaojua faida za kiafya za kufanya mazoezi? Mara kadhaa nimekuwa nikiandika aina za mazoezi mepesi ambayo unaweza kufanya mahali popote iwe kazini au wakati unakwenda nyumbani.

Zifuatazo ni faida 25 za kiafya unazoweza kuzipata endapo utayafanya mazoezi kwa kuweka ratiba.

Kukukinga na magonjwa yasiyoambukiza

Kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na kisukari kwa sababu mazoezi yanasaidia kuwa na mfumo wa moyo na damu wenye afya njema.

Kudhibiti unene na uzito uliokithiri

Unene ni kihatarishi cha kupata magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza, hivyo kufanya mazoezi kunashughulisha viungo vya mwili na kuchoma mafuta yaliyorundikana hatimaye kudhibiti uzito uliokithiri na kuwa na afya njema.

Kushusha shinikizo la juu

Mazoezi yanasababisha kuwa na moyo na mishipa ya damu yenye afya njema kuchangia kushusha shinikizo la juu la damu ambalo ni muuwaji wa kimya kimya.

Kuimarisha mfumo wa hewa

Kufanya mazoezi kama kutembea, kukimbia na kuogelea kunasaidia misuli ya mwili kuwa na ufanisi wa juu kusafirisha na kutumia oksijeni katika mapafu pamoja na kutoa hewa chafu nje ya mwili. Kwa hivyo ni vizuri kutembea kila siku ili kuimarisha mfumo wa hewa.

Kuboresha mfumo wa chakula

Mazoezi yanakufanya kuwa na hamu ya chakula na maji, husaidia chakula kusagwa, kunyonywa na kutolewa kwa ufanisi mwilini na kukuepusha na tatizo gesi na ukosefu wa haja kubwa.

Kupunguza hatari ya kupata saratani

Tafiti zinaonyesha kuwa wanaofanya mazoezi hawapo katika hatari ya kupata saratani za ziwa, utumbo mpana na mapafu ni ndogo ukilinganisha na wasiofanya.

Kudhibiti lehemu mbaya

Lehemu (cholestrol) ni mafuta ndani ya mishipa ya damu, mazoezi yanapunguza kiwango cha lehemu mbaya na kuongeza kiwango cha lehemu nzuri ambayo ina faida mwilini.

Lehemu mbaya, ndiyo inaharibu mishipa ya damu ikiwamo ya moyo hivyo kuidhibiti hupunguza hatari ya shambulizi la moyo (heart attack) na kiharusi (stroke).

Kinga dhidi ya magonjwa

Kadiri unavyofanya mazoezi mara kwa mara ndivyo hatari ya kuumwa na magonjwa mbalimbali inavyopungua hii ni kutokana na mazoezi kukufanya kuwa na kinga madhubuti dhidi ya vimelea.

Misuli imara

Kuimarisha misuli na kukupa ukakamavu wa mwili kwasababu mazoezi yanaifanya misuli kujengeka yenye kudumu hivyo kuweza kukabiliana na mazingira magumu.

Maungio kuwa mepesi

Kusaidia maungio na viungo vya mwili kuwa mepesi hivyo kufanya matendo mbalimbali ya kimwili kwa haraka na ufanisi pasipo kupata majeraha kirahisi.

Mifupa imara

Mazoezi mepesi husaidia kuwa na mifupa imara iliyojengeka hivyo kupunguza hatari ya kupata tatizo la kumomonyoka mifupa lijulikanalo kitabibu kama Osteoporosis.

Itaendelea

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu=

Advertisement