Fahamu maana halisi ya malezi na ulinzi wa mtoto wako

Tafsiri ya kitaalamu inaelezea malezi kuwa ni mchakato wa maandalizi ya mtoto utakaomwezesha kukua, kukubalika na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni kwa kumlinda, kumjamiisha na kumpatia mahitaji na huduma za msingi.

Iwapo malezi ni mchakato wa maandalizi ya mtoto basi shurti iwepo mipango toka kwa wazazi ili kufanikisha hili. Zama za ‘kujipatia’ watoto na ‘kuwaacha’ wakue zinajongea ukingoni. Sasa tunaishi katika wakati wa kuzaa. Kulea. Kulea ni pamoja na kuwekeza katika mahitaji muhimu kama vile lishe bora, afya, elimu, ulinzi na hata maji safi na salama.

Ili kumwezesha mtoto kukua mathalani kiakili ili kimo na weledi wa mambo vikue sambamba basi wazazi hawana budi kuwekeza muda wao kuandaa mtoto mdogo, kitaalamu ikijulikana kama uchangamshi wa awali. Hapa mzazi anafanya vitendo vya makusudi vinavyolenga kumpa mtoto fursa ya kushiriki kikamilifu katika kutenda, kuhusiana na watu au vitu katika mazingira. Mfano hata akiwa bado tumboni unaanza kumuongelesha apate kuifahamu sauti yako na mara tu anapozaliwa unaanza mazungumzo kamili ili kumjengea msingi wa msamiati.

Yaani hata kabla ya mtoto kwenda shule anahitaji maandalizi kwa kitaalamu tunayaita ‘maandalizi ya utayari wa shule.’ Hapa unamfunda stadi muhimu za maisha kama vile kuvijua viungo muhimu vya mwili; macho, mdomo, meno, nk. Hutaki akifika shule akiagizwa kukaa yeye hajui kukaa ina maana gani. Unataka mtoto akiingia shule tayari anao ‘ujanja’ na utayari wa kuipokea elimu.

Ulinzi wa mtoto ni dhana pana mno. Kimsingi, mzazi mlinzi wa mtoto ni yule anayeratibu mienendo ya mtoto wake kila inapoitwa leo.

Mathalani mtoto atavaa nini, atakula nini, ataenda vipi shuleni, atarudishwa na nani nyumbani, atapumzika muda gani, analala wapi na saa ngapi n.k. Bila shaka wahenga waliponena ya kwamba “uchungu wa mwana aujuae mzazi” hawakukosea, walilenga maana pana inayoukilia mahusiano endelevu kati ya mzazi na mtoto katika kipindi chote cha maisha yake.

Kwa bahati mbaya sana idadi kubwa ya wazazi tumesahau wajibu wetu kwa watoto wetu na hivyo majukumu yaliyo mengi yanayohusu maswala ya watoto huachwa kwa watu baki.

Inasikitisha kuwa hoja ya watu kutingwa na shughuli za kimaisha imeteka wazazi wengi jambo ambalo husababisha idadi kubwa ya watoto kukosa ulinzi huku usalama wao ukiwa mashakani.

Ieleweke kuwa watoto huweza kukutana na ukatili katika hatua zote za ukuaji wao kwenye mazingira wanayoishi. Aidha, katika maeneo mengi ukatili dhidi yao huweza kufanywa na watu ambao wanawaona kila siku (wanao wazunguka).

Pindi watoto wanapokosa ulinzi na usalama kutoka kwa wazazi wao kama wawajibikaji wakubwa wakati wote hii huchangia uwezekano vitendo vya unyanyasaji dhidi yao.

Huu ni wasaa wetu kujitathmini na kuhakikisha kuwa watoto wetu wanakua salama wakati wote. Tutekeleze wajibu.

wetu wa kuwaongoza watoto ili wafikie ndoto zao. Watoto ni sehemu muhimu ya jamii, ndiyo tegemeo la uendelevu wa Taifa lolote hivyo hatuna budi kuwalinda, kuwalea vizuri na kuwaendeleza.