Faida na hasara za majungu kazini

Muktasari:

  • Mara nyingi tunaamini majungu hayafai. Tunaposikia kuna watu wanatusema tunajisikia vibaya na kujenga uadui nao. Lakini, kwa upande mwingine, majungu yanaweza kuwa na faida kama nitakavyoonyesha kwenye makala haya.

Fikiria ulitoka kidogo ofisini na umerudi ghafla wenzako wananyamaza. Unajiuliza kulikoni? Mara mada inabadilika. Unajisikiaje unapofahamu kuwa mjadala wenyewe ulikuwa na lengo la kuzungumzia upungufu wako? Kama wewe ni kama wengine, uwezekano ni mkubwa utajisikia vibaya kwa sababu usingependa watu wakuseme vibaya hasa usipokuwepo.

Majungu ni sehemu ya maisha ya kazi. Ingawa hatupendi kusemwa, ukweli ni kwamba haiwezekani kukwepa majungu kwenye eneo la kazi. Hata usiposikia, watu watakusema usipokuwepo na wakati mwingine wewe mwenyewe unaweza kushiriki majungu kuhusu maisha ya wengine.

Katika mipaka ya makala haya, majungu ni mazungumzo yanayofanywa na watu wengine kumhusu mtu mwingine asiyekuwepo, mara nyingi kujadili mapungufu ambayo wasingeweza kuyajadili mtu huyo akiwepo.

Mara nyingi tumeshauriwa tuache tabia ya majungu. Tunafahamu majungu yanaweza kuharibu mahusiano ya watu kazini; majungu yanaweza kupunguza ari ya mfanyakazi kujituma kazini; majungu yanaweza kupunguza hali ya kujiamini anayokuwa nayo mfanyakazi; hata hivyo upo upande mwingine wa majungu ambao ningependa tuutazame kwenye makala haya.

Kukusaidia kuwafahamu watu

Ukweli ni kwamba uhalisia wa maisha ya watu unaofanya nao kazi ni fumbo. Huwezi kumfahamu mtu kwa kusikiliza maelezo yake mwenyewe. Sababu ni kwamba, mara nyingi, binadamu tunapenda kujisema vizuri ili taswira yetu kwenye jamii isiharibike.

Kadhalika, mara nyingi, maisha yetu ya hadharani hutofautiana sana na maisha yetu tunapokuwa faraghani. Kwa lugha nyingine, tunapokuwa na aina fulani ya watu, maisha yetu yanabadilika ili kukidhi mahitaji husika. Sababu ni ile ile kwamba tusingependa mapungufu yetu yafahamike. tusingependa kujielezea kwa namna ambayo ile kubwa.

Hapa ndipo majungu yanapokuwa na nafasi yake. Ukitaka kumfahamu mtu, sikiliza vile watu wanaofanya nae kazi wanavyomzungumzia. Ingawa ni kweli kuna uwezekano wa mazungumzo haya kuwa na nia ya kutangaza mapungufu yake zaidi, bado yatakusaidia kupata mtazamo wa jumla wa watu kuhusu mtu unayetaka kumfahamu.

Ikiwa, kwa mfano, mtu fulani hutuhumiwa kwa upendeleo na watu wengi, hayo si maneno ya kupuuza. Pamoja na uwezekano wa habari mbaya kusikika zaidi kuliko habari njema, usichukulie kirahisi.

Kukusaidia kujitambua

Moja ya udhaifu mkubwa wa binadamu ni kutokujua mapungufu yetu. Tungependa kuamini hatuna udhaifu walionao wengine. Hata katika mazingira ambayo tunayafahamu mapungufu tuliyonayo, mara nyingi hatukubali kusikia yakizungumzwa hadharani kwa hofu ya kuharibu heshima yetu.

Unaposikia watu wanakujadili kwa mabaya, fahamu kuwa wanasaidiana kufikia muafaka wa kukufahamu vizuri. Kwa kuwa wanaogopa kukukwaza, wanaona ni muhimu kukujadili kwa uhuru zaidi wakati haupo.

Kwa upande mwingine, majungu yanakusaidia wewe mwenyewe kujifahamu. Habari za mambo yaliyokuwa yakijadiliwa yatakapokukufikia, yatakusaidia kujitazama kama mtu anayejiangalia kwenye kioo kinachomwonyesha mapungufu yake.

Ndio kusema unaposikia watu wanakusema vibaya usihamaki. Hata kama usingependa kusemwa vibaya, bado unaweza kuyatumia maneno hayo kama fursa chungu ya kujifahamu.

Chanzo cha taarifa muhimu

Majukumu ya kazi yanaweza kukuondoa kwenye mfumo wa kupata taarifa muhimu kabla hazijawa rasmi. Wakati mwingine, shauri ya kusubiri kupata taarifa pale tu zinapokuwa rasmi, habari hizo zinaweza kukufikia kwa kuchelewa. Kumbe ungezipata taarifa hizo mapema kabla zikiwa kwenye hatua ya majungu, huenda zingekusaidia kujipanga na kuchukua tahadhari mapema.

Nikupe mfano. Umesikia watu wakizungumza kuhusu mpango wa mfanyakazi mwenzako kukuhujumu. Ingawa haya kwa haraka yanaweza kuchukuliwa kuwa majungu, bado yanaweza kukusaidia kubaini mpango huo na kujihami kabla utekelezaji wake haujafanyika.

Hivyo, majungu yanayoendelea kwenye eneo la kazi, yanaweza kukusaidia kupata uvumi wa tuhuma ambazo ukiwa makini utakusaidia kuchukua hatua mapema zaidi.

Wakati gani majungu ni hatari?

Si wakati wote majungu yanaweza kuwa na faida. Kuna nyakati majungu haya yanaweza kuwa chanzo cha kubomoa mahusiano mazuri baina ya wafanyakazi. Unawezaje kufahamu kuwa majungu unayoyasikia yanaweza hatari?

Mosi, ni pale majungu yanapolenga kumharibia mwenzako. Maeneo ya kazi hujaa ushindani rasmi na usio rasmi. Ushindani huu, wakati mwingine, ndio unaowafanya watu wapende kukuza mapungufu ya watu wengine kwa lengo la kuharibu taswira yao.

Lakini pia, unapoona majungu yanahusu taarifa za uzushi zisizo na ushahidi, hapo ni muhimu kuchukua tahadhari. Watu wenye nia ovu hutumia uzushi kama mbinu ya kupambana na wabaya wao.

Vilevile, majungu yanaweza kutumika kama sehemu ya jitihada za kutengeneza makundi maslahi katika eneo la kazi. Kuwa makini na maneno yanayoenezwa kwa kasi kwa sababu wakati mwingine lengo ni kujenga matabaka ya kimaslahi kazini.

Hivyo, maneno unayoyasikia, wakati mwingine ni propaganda za kukuza siasa za makundi kwenye maeneo ya kazi. Usipende kuwa sehemu ya propaganda hizi.

Christian Bwaya ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Kwa ushauri wasiliana naye kwa 0754870815