Fainali Miss World leo, mrembo wa Tanzania ang’aa bila ya taji

Pamoja na kura kumwangusha katika mashindano ya Head to Head, mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, Queen Elizabeth Makune ameendelea kung’ara katika shughuli mbalimbali za fainali hizo zinazokoma leo mjini Sanya, China.

Pamoja na Elizabeth kutarajiwa kupanda jukwaa la Miss World leo, hatarajiwi kuwa miongoni mwa washindi baada ya washindani 30 kufahamika mapema, lakini hadi sasa amekuwa kivutio kwa wafuatiliaji.

Ingawa kura zimemwangusha katika mashindano ya Head to Head yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, binti huyo aliyetwaa taji la Miss Tanzania akitokea Kanda ya Dar es Salaam ameendelea kung’ara kutokana na kujiamini kwake.

Mapema wiki hii video ya mlimbwende huyo kutoka Kinondoni ilienea mtandaoni ikimwonyesha akizungumza kwa kujiamini katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni.

Alisema huenda angekuwa mrembo wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa taji la Miss World.

Alisema jukwaa la Miss World limempa nafasi ya kujitambua na kujipambanua kama mwanamke mwenye ndoto ya kubadilisha maisha.

Mahojiano hayo yalionyesha kuwakuna watu wengi mitandaoni na kumshangilia kwamba hata asiposhinda, hali yake ya kujiamini na uwezo wa kupambanua hoja ni ushindi tosha.

Muandaaji wa mashindano hayo nchini, Basilla Mwanukuzi amesisitiza Watanzania kuendelea kumpigia kura mrembo huyo ili kumuweka katika nafasi nzuri katika mashindano hayo.

Mtandao wa GoPageant ambao huelezea na kuchambua mashindano mbalimbali ya urembo duniani, ulimtaja Queen Elizabeth kuwa ni miongoni mwa warembo 15 kati ya 113 wanaoshiriki shindano hilo waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji.