NDANI YA BOKSI: Familia ya Ruge nje ya Mutahaba

Saturday February 23 2019
pic ruge

“Kuna kipindi nilifanya kazi na kupata Sh50 milioni. Nikaja kwa Ruge. Nikaweka mezani hela zote na kumwambia sina gari na msanii bila gari unaambiwa umefulia. Akaniambia maisha siyo gari, kanunue shamba. Nikamuitikia na kuondoka. Nikiwa nje akapigia simu na kusisitiza kanunue shamba, ukinunua gari hautapanda tena kwenye fursa.”

“Leo hii nisipokuwa na nyimbo au kuonekana kimuziki bado naishi kwa sababu ya shamba. Wauza matunda mnaokutana nao mitaa ya Posta wote ni wasambazaji wangu. Benki nyingi zimenifuata kunishawishi nichukue mkopo, wengine wameniambia naweza kuchukua mpaka Sh500 milioni. Lakini sijawa tayari.”

Hayo ni maneno ya Mrisho Mpoto. Alipokuwa anahojiwa na washikaji wa kipindi cha 360, kinachorushwa asubuhi pale Clouds Tv. Kuna kina Mpoto kama wote wasio na idadi wanaoweza kuongea mengi mema juu ya Ruge Mutahaba. Siyo wasanii na watangazaji tu. Jamaa kasaidia mamia ya watu kifursa.

Pesa ya burudani ipo shingoni mwake. Ukubwa wa jina tofauti na mavazi yake. ‘Braza’ Joe akiwa busy na tarakimu za kibenki. Yeye anabaki kama injini ya Clouds. Akijua hii ni pesa anageuka mnyenyekevu. Uzeni unga. Uzeni pembe za faru. Yeye anauza burudani. Akili nyingi sana. Msikilize na ufanye anachokueleza. Hakika utaweza.

Huyu mwamba wa burudani. Kalala sehemu. Kwenye kuta zenye vifaa na wataalamu wa tiba. Anayapigania maisha. Anapigania pumzi yake. Anapigania afya. Tanzania inam-miss. Burudani inapwaya. Kiti chake kinaota kutu pale mjengoni ghorofani Mikocheni. Maisha ya burudani bila Ruge yanakosa mvuto na maana halisi.

Juhudi zinafanywa na familia na wadau ikiwemo kuundwa kwa kamati ya kusaidia matibabu yake. Gharama ni kubwa sana. Ni muda mrefu mshikaji yupo kwenye matibabu. Anahitaji msaada wa faraja, maombi na pesa za kutosha ili kumudu matibabu. Milioni 5 kwa siku siyo jambo jepesi. Ni wakati wa kumfungulia dunia ya upendo wetu kwake.

Advertisement

Sikilizeni madogo. Hangaikeni kunyoa viduku. Kunyanyua vyuma kutafuta six packs. Totozi mtazitazama kwenye foleni ‘zikidraivu’ ndinga za mamilioni. Huku mkiishia kuwaita shemeji. Viduku waachieni madansa wa Dai na Kiba. Kubeba nondo mtaishia kulinda watu kwenye kumbi za starehe usiku. Saka mahela.

Tafuteni, zilindeni na kuheshimu pesa. Acha kujiumiza kutaka mtelezo kwa totozi. Pesa ni zaidi ya kukata viuno kwenye sita kwa sita. Siyo wajinga mademu kuolewa na vibabu huko Tabora. Maisha bana, tafsiri unavyoweza. Lakini elewa kuwa ni zaidi ya vile unavyoishi. Tajiri kwa masikini inakubidi uwe mbishi.

Hili ni tatizo tena ni kubwa kuliko watu wanavyofikiria. Kwa hatua tuliofikia ya usugu wa tatizo ni vigumu kupata tiba. Bahati mbaya hata mangariba wanakaa kando na sanaa kwa sababu tofauti tofauti. Yaani sanaa na wasanii wa Tanzania wanahitaji kuzaliwa na kubatizwa upya, tena ule ubatizo wa Kisabato kuzamishwa kwenye maji.

Nafuu pekee tuliyonayo ni kuwekeza katika kizazi kijacho. Watoto wetu! Wafundishwe tulipotoka! Wafundishwe tulipokosea! Wafundishwe na wajue kwa uwazi na ukweli wa kwa nini sisi hatuwezi na tumeshindwa kuchukua hatua kuifanya sanaa ya Tanzania iwe yenye neema. Wasanii hawana uhakika wa afya na baadaye yao kutokana na sanaa kukosa mfumo rasmi.

Watoto tukiwaambia ukweli wa makosa watafanya mapinduzi ya fikra. Sisi hatuwezi kuubadili mfumo unaotutengezea umasikini kwenye sanaa kila siku. Hatuwezi kutofautisha sanaa na dawa za kulevya. Ulevi na kushindwa kujisimamia kiafya. Hata ulinzi wa mifuko na akaunti zetu pindi tunapopata pesa nyingi na kuacha zitoweke.

Wale wa kike wanatumia muda mwingi kuwaza ‘smart phone’ na ‘ku-drive’ mjini. Wanajikuta wanazeeka bila mali wala ndoa. Wakiona hakuna dalili wanalazimika kujiweka kwa mtu yeyote mradi ana nafuu ya kulea mtoto. Sanaa usiwe ukuta wa kukutenga na jamii na kujikuta unaishi maisha ‘feki’ tofauti na kipato chako.

Wanamuziki na waigizaji kitambo tu wanapiga pesa. Tena pesa ndefu. Lakini kuna vitu wanavijali bila kujua kuwa ni hatari kwao. Mojawapo ni ‘ku-meintaini statasi’ zao za ‘usupastaa’. Wanapambana kufanya vitu ambavyo haviendani na uhalisia wa vipato vyao. Wakitaka kuwa tofauti kabisa na watu wa kawaida na kutaka kuishi kimalaika katikati ya bwawa la kishetani.

Mwanamuziki anavyozidi kuongeza pesa kwenye akaunti. Ndivyo anavyozidi kuongeza ‘stress’ kichwani. Presha ya kuumiza vichwa anunue gari gani ili awe kama fulani. Ndiyo akili ya Mpoto aliyokwenda nayo kwa Ruge. Mwishowe akaondoka na akili mpya inayomsaidia mpaka hii leo.

Kwa wasanii wanaoibukia ‘stress’ ndo tatizo zaidi. Wengi wanadiriki kukodisha magari ya watu na kulipa kila mwezi. Mradi asionekane kwenye daladala. Matokeo yake kile anachopata kinaishia kwenue usafiri na shughuli zote za kukwepa macho ya watu. Si kila msanii Bongo anaweza kumiliki gari.

Hata ‘andagraundi’ aliyetoka na ‘kuhiti’ na wimbo mmoja. Naye anahangaika na muonekano wake kwa watu. Hizi ndo akili tope zilizojaa kwenye ‘gemu’. Ambazo zinahitaji uponyaji wa haraka kama Mpoto kwa Ruge. Maana naye angebaki kwenye kumbukumbu tu ya kuwahi kukimbiza kisanaa na ngonjera zake.

Hawa wenye akili za ‘kisimbilisi pori’ hata nguo wanaazimana. Kwa kipindi hiki siyo kila ‘staa’ hapa Bongo anaweza kubadili pamba kila siku. Wapo wale wanaovaa kwa matangazo. Wapo wakopaji wakubwa na wale wa kuazima kupigia picha. Kinachowavuruga zaidi ni ‘stress’ za instagram. Kutupia picha ‘deile’ na pamba mpya.

Mitandao ya kijamii inafanya kila ‘staa’ ajitahidi kutupia picha bila ya kuonekana kama amerudia pamba. Kwa kuhofia eti kurasa za wanoko wa ‘town’ na mashabiki ambao lazima waliongelee hilo. Kurudia pamba mtandaoni kwa ‘staa’ lazima atengeneze stori mpya ambayo ‘itatrend’.

Siku hizi tunaona wana kibao kwenye ‘gemu’ wanaokimbiza wakionyesha mijengo yao. Wapo wanaoponda maonyesho hayo. Lakini hili linatokana na ‘stress’ zao walizozipata baada ya kuona wengine wanalijenga kabla yao. Pia na imani potofu ya kuamini kuwa mafanikio ya kweli ni ndinga na mjengo.

Wasanii wengi wameonyesha mijengo yao. Hasa wanamuziki maana muziki hivi sasa unalipa kuliko filamu. ‘Stress’ za mijengo zitazidi maana wengi wapangaji. Na kuna ‘stress’ ya muonekano wa maumbo na rangi. Pesa nyingi zinaishia ‘jimu’, kuongeza bando la rangi na kusimika nyama bandia kwenye maungo yao.

Kama ambavyo Mpoto alipewa akili badala ya shairi. Ikafanya milioni 50 awekeze kwenye kilimo badala ya ndinga na pamba. Kuna milioni 50 nyingi sana kwenye miili ya wasanii wetu, wanachokosa ni akili iliyolala hapo ‘Sauzi’ ikilipigania afya. Tusifanye maombi tu bali na msaada wa kipesa. Familia kubwa ya Ruge iko nje ya ukoo wa Mutahaba.

Advertisement