Fanya haya utafutapo ajira

Friday September 21 2018

 

By Christian Bwaya, Mwananchi

Kutafuta kazi ni kuingia kwenye soko la ajira ambalo kimsingi ni uwanja unaowakutanisha watu wenye mahitaji makubwa ya aina mbili.

Upande mmoja, wapo watu wenye ‘bidhaa’ ya ujuzi na weledi, lakini wanataka kujipatia kipato kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyonayo. Hawa wanaitwa watafuta kazi.

Upande wa pili, wapo watu wanaohitaji ujuzi huo ili uwasaidie kuongeza ufanisi wa huduma wanazotoa kwa kutumia rasilimali na fedha za kuulipia ujuzi huo.Hawa wanaitwa waajiri.

Pande hizi mbili zinahitajiana na kutegemeana, kwa maana ya mahitaji ya upande mmoja, hutoa jawabu la tatizo la upande wa pili.

Ili uajirike, unalazimika kumridhisha mwajiri kuwa unao ujuzi na uwezo wa kutumia maarifa uliyonayo katika kuongeza ufanisi wa huduma anazozitoa.

Kutokana na ukweli kwamba waajiriwa hutofautiana ujuzi na uwezo huo; na kwa sababu uwezo wa waajiri pia hutofautiana; na kwa kuwa haiwezekani kila mwenye ujuzi kukidhi mahitaji ya mwajiri, hapa ndipo dhana ya ushindani wa soko la ajira inapojitokeza.

Ili ushindane vyema katika soko la ajira ni jukumu la mtafuta kazi kujiandaa ipasavyo kiujuzi na kiweledi. Tuangalie mambo kadhaa muhimu ya kufanya unapoingia kwenye soko la ajira ili kuongeza uwezekano wa kuajirika.

Jenga utambulisho wako

Utambulisho wako ni kama kutangaza bidhaa uliyonayo sokoni. Kwa wewe unayetafuta kazi, bidhaa yako ni ujuzi ulionao, maarifa na fikra zinazokutambulisha kwa wengine. Ni muhimu kutafuta mazingira ya kutangaza bidhaa yako.

Bahati mbaya vijana wengi huwa hawatumii muda wa kutosha kujitambua wana kitu gani ndani yao. Kutojua wao ni kina nani kunawafanya watumie muda mwingi kusikiliza maoni ya watu, kujua nini kinalipa vyuoni, soko linataka nini na matarajio ya jumla ya jamii.

Sababu hizi ni muhimu lakini haziwezi kukusaidia. Ingawa kwa sasa unaweza kuwa na msisimko wa kusoma fani unayofikiri itakuletea heshima kwa jamii, baada ya muda hutaona faida yake. Sababu kubwa ni kwamba elimu isipokuza kile kilichomo ndani yao, haiwezi kukusaidia.

Unataka kufanya nini baadaye?

Sambamba na kujua kuna nini ndani yako, ni muhimu kujua kwa nini unataka kusoma. Usisome tu kwa sababu na wewe unataka uonekane msomi. Fahamu kwa yakini lengo lako la kwenda chuo. Je, unataka kuajiriwa baada ya masomo au unalenga kujiajiri?

Ukweli ni kwamba tunatofautiana. Ni makosa kufikiri watu wote wanaweza kujiajiri. Kwa wakati wowote, kokote, bado watakuwepo watu ambao mafanikio yao yatapatikana kwenye ajira.

Hawa, hata ungewawekea mazingira ya kujiajiri, bado furaha yao inatimilika kwa kufanya kazi chini ya watu wengine. Hakuna ubaya kutaka kuajiriwa na usikatishwe tamaa na watu.

Advertisement