Genevieve Nnaji: Bilionea wa filamu barani Afrika

Saturday February 9 2019

 

Miezi michache iliyopita kampuni inayojihusisha na usambazaji wa kazi za sanaa, Netflix ilitangaza kuinunua filamu ya Genevieve Nnaji, Lion Heart. Imekuwa filamu ya kwanza kutoka Afrika kununuliwa na kampuni hiyo.

Kabla ya kununuliwa na Netflix, filamu hiyo ilipokelewa vizuri katika soko nchini Nigeria hasa baada ya kuonyeshwa katika majumba ya sinema.

Mataifa mbalimbali nchini Afrika yalimtumia mwaliko maalumu yakitaka filamu hiyo ikaonyeshwe katika majumba ya sinema.

Tangu kutoka kwake, filamu ya Lion Heart imekuwa ikisifiwa na mmoja wa waigizaji maarufu duniani, Kerry Washington, kupitia mtandao wa Twitter alimpongeza Genevieve.

Kwa filamu hiyo, Netflix imemlipa dola za Marekani milioni 3.5 ambazo ni wastani wa Sh8.05 bilioni huku akiendelea kubaki kuwa mmiliki wa haki zote za sanaa.

Baada ya kuuza filamu hiyo, Genevieve amepata zali jingine la kusajili na kampuni ya Universal Talent Agency ambayo pia inawasimamia DJ Khalid, Johnny Depp, Lady Gaga na Angelina Jolie.

Aendelea kuijenga himaya yake

Tunapozungumzia uwezekezaji na maendeleo ndiyo anayoyafanya nyota wa filamu mwenye umri wa miaka 39.

Licha ya uwezo wake mkubwa kwenye uigizaji, nyota huyu anatajwa kuwa miongoni mwa wasanii wa Nigeria waliowekeza na kujijengea utajiri mkubwa.

Pamoja na filamu kuwa chanzo kikubwa cha mapato yake, nyota huyu amekuwa akijihusisha na biashara mbalimbali ikiwamo lebo ya mavazi na nywele zilizochangia utajiri wake kuwa zaidi ya naira 100 milioni.

Ukitembelea maduka mbalimbali ya nguo nchini Nigeria na kukutana na nguo zenye nembo ya St. Genevieve jua ni za mwigizaji huyu.

Ukiachilia mbali uigizaji, Genevieve ameanza kutayarisha filamu zake mwenyewe zinazotajwa kufanya vizuri sokoni.

Kana kwamba hiyo haitoshi, hivi karibuni Genevieve aliwekeza fedha nyingi kwenye ununuzi wa viwanja na mashamba.

Katika kuonyesha kuwa hakamatiki, tayari ameshaanza kuvifanyia kazi viwanja hivyo kwa kujenga nyumba ambazo atazipangisha baada ya kukamilika kwake.

Unapotaja orodha ya waigizaji wanawake matajiri, jina la Genevieve Nnaji haliwezi kukosekana kutokana na uwepo wake katika tasnia hiyo kwa muda mrefu.

Uwepo wake muda mrefu kwenye tasnia ya filamu Nollywood siyo kigezo pekee kinachomwingiza katika orodha hiyo, kwa kuwa wapo wakongwe wengi na hawamo hata katika orodha ya 30 bora.

Kujituma katika uchezaji filamu kumemfanya awe mwigizaji ghali Afrika ambaye kumchezesha katika filamu moja inabidi mtayarishaji atoboe mifuko yake.

Genevieve pia ni balozi wa bidhaa mbalimbali ambazo zinamwingizia mamilioni ya fedha kila mwaka.

Advertisement