Gozbert: Hata Yesu alihubiri kwa watoza ushuru

Saturday October 12 2019

 

Wiki chache baada ya kuibua gumzo kutokana na kuonekana katika tamasha la Tigo Fiesta, Goodluck Gozbert amesema hajali maneno ya watu kwani anajua anachokifanya na kwamba hata Yesu alihubiri kwa watoza ushuru.

Katika tamasha hilo lililofanyika jijini Mwanza, Gozbert aliweka historia kwa kuwa msanii wa kwanza wa nyimbo za injili kupanda katika jukwaa hilo na kuibua maswali ya kulikoni mwanamuziki wa injili anayeimba nyimbo za kumtukuza Mungu, kupanda jukwaa la muziki wa dunia. Lakini Gozbert, ambaye sasa anatamba na kibao cha ‘Nibadilishe’, alisema mpaka anapanda jukwaani alikuwa anajua nini anafanya, na kama ni kusemwa alishazoea kwani tangu alipoachia wimbo wa “Acha Waambiane” na “Ipo Siku” kulikuwa na maneno na wengi walimuona hafai kuwa mwimbaji nyimbo za injili.

“Shida ni kwamba Wakristo tumegawana dhambi. Kuna maeneo pombe dhambi mengine si dhambi, mengine suruali dhambi mengine si dhambi,” alisema.

“Mengine kukatika dhambi, mengine we mchezee Mungu wako. Sasa ukiwa mtu maarufu kama mimi hujui kundi lipi linakushambulia kati ya hayo. Kinachotakiwa ni kuwasikiliza na kuwasoma, kisha kufuta soksi na kuendeleza mwendo.”

Hata hivyo aliwashukuru waliompigia kura na kumuona kuwa anafaa kutumbuiza kwenye tamasha hilo, akisema hiyo inaonyesha namna gani watu wanapenda huduma yake.

“Nitapanda kutumbuiza kwenye tamasha la Fiesta hapa Sumbawanga, Narudia ninajua ninachokifanya,” alisema.

Advertisement

“Kama ambavyo huwa napata maono ya mashairi ya nyimbo zangu, hata huku pia nina maono nako na naamini nawafikishia ujumbe watu wengi zaidi,” alisema.

Gozbert alisema hata Yesu alikwenda kuhubiri kwa wanaohitaji huduma ya kiroho kama watoza ushuru.

Advertisement