HEKAYA ZA MLEVI: Je soda ikikutwa kwa mlevi ni uchafu?

Sitakuja kuisahau safari yangu ya kwanza nje ya jiji nililozaliwa, jiji lililonikuza, ninaloishi hadi leo. Ni dunia yangu iliyonifunza kuishi na kila kiumbe. Hata leo nikitupwa sayari nyingine nitaelewana na wenyeji wa huko kwa kuwa nilijifunza hapa.

Kabla ya safari hiyo sikuwahi kutoka nje ya jiji, hata Chalinze na Pugu. Japo ni miaka mingi imepita lakini nakumbuka safari ya Mbagala ilivyonitoa ‘ujiji’ badala ya ushamba. Wakati huo Mbagala ilikuwa chaka la kufa mtu. Mwisho wa usafiri wa mabasi ya umma ya wakati huo maarufu UDA ilikuwa Kurasini!

Siku iliwadia, nilitakiwa kwenda Lutengano, Tukuyu, Mbeya masomoni. Sikupata picha ya mahala hapo lakini nilikuwa na bashasha kutaka kujionea. Kwangu siku zilisimama na niliona kama siku ya safari imesahaulika kwenye kalenda ya mwaka.

Bahati nilipata lifti ya mabosi wa Wizara ya Nishati na Madini walioelekea kwenye machimbo ya makaa ya mawe, Kiwira. Nami kwa kuwa nilikuwa mtoto wa bosi, wakaelekezwa kunifikisha shule kabla ya kuendelea na yao.

Safari ilikuwa tamu ukizingatia tuliteleza na Land Rover 110 ambazo ndio kwanza zilikuwa zinaingia mjini. Muda wote sikutaka hata kupepesa kwa hofu ya kukosa visivyopaswa kukoswa. Niliona kila kitu kikiwa tofauti na mazoea; watu, wanyama, miji, misitu, hata kuku wao walikuwa wa staili ya Goliati.

Tulipovuka Mikumi tulipaki. Wote walicheka nilipouliza “Ndio tumefika?”Nikaambiwa hata nusu bado. Tunasafiri karibu kilomita 900 na ndio kwanza tupo theluthi ya kwanza! Nikadokezwa nitegemee maradufu ya kila nilichokiona.

Sikatai wakati tunaupanda Mlima Kitonga niliushika moyo usiniponyoke, lakini tukapiga mwendo hadi Makambako. Nilikwambia sitaisahau asilani siku hii, maana nilimshuhudia mbwa na jeuri yake ya kutembea utupu, alijikunyata kwenye jiko la mchoma mahindi akiota moto!

Kwa upeo wangu paliongoza kwa baridi duniani, sawa na jokofu. Dereva aliwasha mashine za kuongeza joto, bado vitambi vya mabosi vilirukaruka. Mmoja alituongoza kwa kijana mchoma mahindi jirani na stendi.

Kijana alinipukuchulia mahindi baada ya meno yangu kukosa ushirikiano kutokana na baridi ile. Akaniuliza tunapoelekea, nikamjibu Tukuyu. Kijana alipiga yowe na kulalamika “Wanaenda kumuua mtoto wa watu”!

Mwenzie aliyekuwa akimenya mahindi akasema, “Kule ukifungulia maji linaanza kutoka donge la barafu”. Mwingine sijui aliibukia wapi akadakia na neno baya zaidi: “Hata akijisaidia haja ndogo…!!!”

Kwa maneno yale safari ilinitumbukia nyongo. Nikawaza mabaya likiwemo la ‘kutupwa’. Nilijiona nisiye na bahati kupelekwa mahala ambako huwezi kujisaidia iwapo donge la barafu litashindwa kuanza kutoka.

Kumbe nilikuwa mpumbavu, bado. Sikuelewa sababu za wazazi kupeleka watoto shule za bweni. Sikuelewa kwa nini shule hizo zinapata matokeo chanya maradufu ukilinganisha na za kutwa. Sikujua ni kwa nini wakitoka kule wanakuwa wabunifu kuliko wenzao wa huku.

Ukweli ni kwamba binadamu mbunifu anataka utulivu. Daima unapotaka kupokea ama kufanya jambo tofauti na lenye mashiko katika jamii, utafakari kwanza. Na tafakari haiwezi kukubali mahala penye bla blaa. Mtoto gani atajisomea, akaelewa katikati ya kigoma cha harusi?

Ndio maana shule zilijengwa mbali na pilika za wakazi. Hilo lilifanyika zama zile ingawa sasa ni kitendawili. Ongezeko la watu limewafanya raia waunge nyumba zao na ukuta wa shule. Sitaki kufukua makaburi ya wajanja waliouziana hadi barabara za mitaa, ila ukweli ndio huo.

Kwa kuwa shule zilivamiwa na kushindwa kujitetea, haimaanishi mipango ya watoto wetu iishie hapo. Ndio maana tunawapeleka bweni. Na si kwamba kwingine hakuna walimu, bali tunawatafutia utulivu wa kutafakari watoke na ubunifu mpya.

Kwa ridhaa yenu, figisu zote zinazowafanya wanafunzi kukosa utulivu wa kutafakari naziita uchafu. Kwa mujibu wa kamusi yangu, uchafu ni chochote kisicho mahala pake. Chakula kikikutwa chooni ni uchafu. Ufagio ulio mezani, hata bia ikikutwa darasani ni uchafu. Sijui soda ikikutwa kwa mlevi?

Kwenye soko la mitumba kuna wapiga debe wanaonadi balo jipya likifunguliwa. Wana kelele sana, lakini kelele zao si uchafu kwani pale ni sokoni. Kidonda ni halali ya nzi. Lakini wapo madalali wanaochukua kazi ya kunadi bidhaa zinazoondolewa kwenye mzunguko wa mauzo. Weeee!

Kumbe hata magari ya matangazo yanayopiga kelele mtaani wakati watu wanafanya shughuli zao ni uchafu. Baa zinazokoleza muziki kwenye makazi ya watu wenyewe wakiwa wamelala ni uchafu. Yaani doa moja jeupe kwenye nguo nyeusi ni uchafu.

Tunaweza kuwasaidia watoto kuondokana na uchafu huu. Tuwapunguzie kelele za madalali wa sabuni na laini za simu kwenye spika za magari ya matangazo. Wasome na kutafakari, watatuopoa kwenye vibarua vya u-MC wa kunadi bidhaa zinazokwenda kueksipaya!