HEKAYA ZA MLEVI: Kauziwa feki naye kalipa feki…

Aliondokea mzee mmoja aliyesemekana kuwa mwenye busara zaidi ya watu wote kijijini kwake. Sifa zake zilisambaa hadi kwenye vijiji vya jirani kwa sababu wenyeji walikiri kuwa lolote atakaloliamua yeye ni sahihi.

Akaanza kupata wageni waliokuwa na mashauri yao kutoka kila upande.

Siku moja alifuatwa na mama wa watoto mapacha. “Shehe aliwapa wanangu baraka kulingana na majina yao. Akamfunga Hassan kitambaa chekundu na Hussein cha buluu mkononi. Kwa bahati mbaya nimevipoteza vitambaa vile na kwa jinsi walivyofanana nashindwa kuwatofautisha. Naogopa kuwachanganya majina kwa sababu nitawapotezea baraka zao”. Mzee alimwambia mama amletee hao watoto. Akawauliza watu: “Hakuna hata mmoja anayefahamu nani ni nani?” Wakajibu hakuna. Akasema “Huyu ndiye Hassan na huyo Hussein”. Watu wote walishangazwa na uwezo wake mkubwa.

Siku ingine alifuatwa na mtu aliyedai kutoroshewa mwanaye wa pekee. Mtoto alikuwa mdogo kiasi kwamba haikuwa rahisi kwake kugundua kuwa alikuwa anaibwa. Kwa bahati nzuri basi la kitongoji chao hufanya safari tatu tu kwa siku; asubuhi, mchana na jioni.

Mzee aliona pipi ya kijiti iliyoonesha kuangushwa muda huohuo kando ya njia. Akamwambia, “ifuate njia hii hadi kituo cha basi utawakuta”. Yule bwana akatoka mbio kuelekea huko na punde akarudi kwa furaha akiwa na mwanaye.

Ukweli huyu mzee hakuwa na akili za ziada. Swali la mapacha lingejibiwa vyovyote kwa sababu halikuwa na jibu. Hata lile la kuibwa mtoto linaeleweka. Watoto hunaswa kwa lambalamba. Na kwa kuwa kilichoibwa haifichwi palipoibiwa, kuonekana kwa pipi mpya mchangani kulithibitisha kuwa kuna mtoto alipelekwa mbio kuwahi basi ili atoroshwe.

Katika miaka hii watu hawafikirii sana. Itafikia hatua watu watasahau kuwa dalili ya mvua ni mawingu, na mkulima atagugo ili kujua mvua itashuka muda gani. Unamkumbuka yule mkata mti wa Abunuwasi? Alikalia tawi wakati anakata shina. Akaambiwa kuwa ataanguka na tawi. Alipoanguka akamwita Abunuwasi “Nabii”.

Wapo watu wanatumia fursa za namna hii. Ulimwengu wetu umetawaliwa na teknolojia, hasa kompyuta. Mtu akitaka kujua Ufaransa ilichukua kombe la dunia mbele ya Brazil mwaka gani anawasha data na kugugo. Akitaka kujua dola ya Marekani ni sawa na randi ngapi za Afrika ya Kusini atafanya vivyo hivyo.

Kutokana na teknolojia iliyotutawala, maisha yetu yanakwenda mbio za ajabu. Leo mtu anayetaka kununua gari la mtumba anagugo “used cars” na sekunde hiyohiyo analetewa bei za magari hayo kutoka Japan, Malyasia na kwingineko. Mchakato unaanzia muda huo huo.

Lakini katika karne nyingi zilizopita mfanyabiashara alitumia mwaka mzima kwa msafara wa ngamia kutoka kwenye pembe ya Afrika (Ethiopia) hadi kufika Mashariki ya Kati. Alitumia tena mwaka kurudi nyumbani. Haikuwa hatari kwani hali haikuwalazimisha kwenda mbio kama hivi leo.

Kwa kawaida maisha kwenda kasi maana yake moyo utaenda kasi kusafisha damu, damu itakimbia maradufu kukidhi mahitaji ya mwili, maini, figo, nyongo na bandama vitakuwa bize ajabu na ubongo utafanya kazi ya ziada kugawa majukumu ya mwili. Wakati huohuo mwili wenyewe utakosa mapumziko.

Kwa maana hii ni lazima mtu atachoka mapema. Sio kitu cha ajabu kwa watu wa kale kuishi miaka zaidi ya mia tisa wakiwa kwenye ubora wao wakati sisi mtu anaanza uzee akiwa na miaka arobaini!

Jambo la kushangaza kuliko yote ni jitihada za mtu huyu wa leo kufupisha zaidi umri wake. Nilitegemea kutokana na hali aliyonayo sasa angerekebisha mwenendo na kutibu vidonda anavyovianzisha. Nina maana kuwa chimbua ardhi ili upate udongo wa kujengea nyumba, lakini fukia mashimo hayo baada ya ujenzi ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi.

Maisha yako hivyo. Unafanya kazi bila kupumzika lakini basi upumzike baada ya kazi. Unapofanya kazi zinazohusisha sumu (toxic au radiation) kumbuka kunywa maziwa baada ya kazi. Hii siyo tiba kwa asilimia zote, lakini inafanana na kufukia mashimo uliyokwisha kuyatumia.

Sasa jitihada za leo ndio hizi: Badala ya kurutubisha shamba ili apate mazao kwa wingi, anatia sumu (dawa) ili kuyavimbisha. Chungwa linapata ukubwa wa dalanzi na embe kama dafu.

Badala ya kuwapa lishe bora mifugo, watu wanaongeza dozi ya sindano ili mifugo hiyo ikomae kabla ya wakati wake. Hivi sasa kuku analiwa siku chache tu baada ya kutengenezwa (sio kutotolewa). Janga hili pia limewasibu ng’ombe na hata samaki kwani nasikia kuna samaki wa Mchina wasio na baba wala mama.

Badala ya kujitibu sasa wanajiua. Mtu anajua kuwa kasi anayokwenda anauumiza mwili wake. Badala ya kuutibu anakunywa vidonge vya kufunga mishipa ya fahamu ili maumivu yasisikike. Kazi ya dawa ni kuufanya mwili uondoe mapungufu ya mwili, na si kuuziba mwili usione mapungufu.

Hatuwezi kuikwepa kasi kwa kuwa hatuna budi kwenda nayo lakini kama nilivyosema uking’oa basi uzibe pengo. Inapotokea huyu kamwaga ugali nawe ukaona ndio sababu ya kumwaga mboga kuna hatari ya kuteketea wote. Mkulima anapomlisha daktari sumu na daktari akamdunga mkulima sumu ya kutuliza maumivu kuna nini tena?