HEKAYA ZA MLEVI: Mchape adui ucheke na wanawe

Saturday December 8 2018GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Tumesoma kuwa siku ya kwanza dunia ilipoumbwa ilifunikwa na maji. Kwa kuwa Muumba alikuwa na mpango wake, akayatenga maji na nchi, zikatokea bahari, mito, maziwa, anga, visiwa, ghuba, rasi, milima, tambarare, mabonde na kila unachokiona juu ya uso wa dunia.

Akaweka idadi isiyo na idadi ya viumbe vilivyoihuisha dunia. Pia aliweka mifumo ya kutegemeana kati yao. Bila maji hakuna uhai. Maji hupatikana ardhini baada ya mvua kutoka angani, lakini ni baada ya jua kufyonza umande duniani na kutengeneza mawingu katika mfumo wa barafu, jua hilohilo linayeyusha barafu kuwa mvua.

Binadamu akapewa akili ya kuitunza dunia. Wengine wanadhani akili hupatikana darasani tu, lakini hata mtoto aliyezaliwa leo hujua ziwa la mamaye. Kabla ya darasa watu walichonga mawe na kuyageuza kuwa majembe, wakalima. Walijua mvua ya pandizi na ya palizi.

Hii kitu inaitwa elimu asilia au “Oral Tradition”. Tupo pamoja?

Kutokana na pilika za kuboresha maisha yake binadamu alilazimika kukata miti ili kujenga makazi na madaraja. Kukokea moto kwa mapishi na kujikinga na baridi kali na kadhalika, hakukuwa na athari yoyote kwa sababu idadi ya watu bado ilikuwa chini na pilika zake hazikuwa ndefu kiviiiile.

Hivi leo kuna idadi kubwa sana ya watu. Katika nchi zetu za kitropiki tumeshuhudia ukaukaji wa visima vya asili, kupotea kwa aina za ndege (kama shorwe bwenzi), wadudu (kama vunja jungu) na wanyama kama nyani na digidigi tuliowakuta na kuwazoea. Sasa hivi tuna kunguru “full suti” tu maana hata wale “bon tai” washatoweka.

Kwa kiasi kikubwa, hii inatokana na uharibifu wa mazingira. Binadamu sasa anahitaji miti kwa kujengea, kupikia, kutengeneza joto, samani za ndani na ofisini, nguo, nyenzo za usafiri na usafirishaji, bidhaa mbalimbali za karatasi pamoja na vifungashio. Wanaouana wanatengeneza mikuki, vitako vya bunduki na ngao wakati wanaookoana wanatengeneza dawa kutokana na magome, majani na mizizi ya miti hiyohiyo.

Dunia imeanza kuota “kipara”. Kila siku zaidi ya eka laki mbili za misitu inadondoshwa. Hiyo ni sawa na eka 139 kila dakika! Hebu ingiza hiyo akilini mwako.

Lakini kwa kuwa binadamu anajua kuwa hapaswi kuharibu mazingira yake, akaanza kampeni ya “kata mti panda mti”. Nakumbuka kwetu ikawa “kata mmoja panda mitatu” ili kuihami nchi yetu dhidi ya ukame. Bila miti hakuna maji, na bila maji hakuna uhai. Watu walishindwa kutengeneza makazi kwenye sayari ya Mars kwa kuwa hakuna maji.

Mtu huongezewa Elimu kulingana na majukumu anayokwenda kukabiliana nayo. Kwa mfano vijana wanaojiandaa kuwa matabibu wanasoma sayansi ya viumbe kwanza kinadharia, halafu kwa vitendo. Hapa ndipo hufundishwa upasuaji kwa kuanzia na wanyama wadogo kama chura. Yule atakayempasua chura na kushindwa kumwamsha hai hafai kujaribu tiba ya upasuaji kwa binadamu mwenzie.

Wale wanaojiandaa kuwa Wanajeshi wana mafunzo yao. Bila shaka ulishawahi kuona maonesho ya Kijeshi mnamo siku ya Mashujaa. ulipata picha jinsi mafunzo kwa vitendo (practical) Jeshini yanavyokuwa. Yanahusisha ukakamavu na nidhamu ya hali ya juu sana hata kama wanamkabili adui.

Namkumbuka Zahir Ali Zorro alipoimba na JKT Kimulimuli mara tu baada ya vita dhidi ya majeshi ya uvamizi kutoka Uganda, alibainisha jinsi wazazi walivyowaagiza watoto wao (akina Zahir, Mti Mkavu, Mamba n.k.) kumfukuza Amin aliyeitawala kimabavu nchi ya Uganda kisha kumpa adhabu kidogo tu ndani ya mipaka yake.

Baada ya kumuadhibu adui, watoto wakaanza safari ya kurudi. Wakawaaga jamaa huko Kampala, Masaka, Mbarara na walipoingia Kagera ndipo walipokutana na shangwe na nderemo za wazazi wao. Sasa fikiria; unamaliza kumtwanga adui halafu unaagana na wajomba zake hukohuko nyumbani kwake. Ni nidhamu iliyopitiliza.

Hakuacha kutoa siri ya ushindi: “Umoja wenye nguvu, mshikamano wa dhati na nidhamu ya hali ya juu”. Ikumbukwe kuwa walishashika nguvu pale Uganda kiasi kwamba wangeweza kuwafanyia lolote kama mauaji, uporaji, ubakaji na ovu lolote bila kushitakiwa.

Wakarudi na ushindi, tukasahau vita na kuendeleza ujenzi wa Taifa pamoja na kupanda miti.

Nilitegemea vijana wa sasa wataendeleza nidhamu hiyo ili kulitukuza jeshi letu. Lakini kinyume chake wanatumia nguvu ya ziada kabla hata ya kuelewa wanachokitaka. Kwa mfano walitakiwa kujua tofauti ya mboji na uchafu.

Sasa watu wanakamatwa na kupigwa vibao kwa kuwa majani yamepukutishwa kutoka mitini mchana. Wangefanyaje kuyazuia? Wapande miti ili kuiokoa dunia au waikate kwa kuyaogopa majani?

Ushauri wangu kwa mamlaka za juu ni huu: Wapewe mafunzo ya usimamizi wa mazingira. Ardhi yote ikisakafiwa kwa marumaru inapendeza, lakini ndio utakuwa mwisho wa dunia!

Hawa walifundishwa kijeshi lakini wanafanya kazi na raia. Wajue kuwa kufanya kazi na Wananchi ni tofauti na kumsaka adui.

Wananchi nao wapewe tena Elimu ya haki zao. Kuchoma na kufukia taka ni kosa. Kuziweka uwanjani kusubiri gari la taka ni kosa. Kukarabati ukuta wako usijewaangukia majirani ni kosa!

Mtupe Elimu japo kwa vipeperushi maana tumechoka kupigwa viboko mbele za wenetu.

Advertisement