HEKAYA ZA MLEVI: Siafu mwenye domo kubwa ndiye askari

Mambo mengine tumwachie Mungu. Ukianza leo kujiuliza hivi inakuwaje wanyama walioumbwa na matanki ya kuhifadhi maji wakaishi jangwani, wenye meno makali na kucha kama visu wakawa wawindaji, au siafu wenye meno makali wakawa walinzi wa wenzao utaingia kwenye utafiti mkubwa bila kupata majibu. Afadhali tatizo lingeishia hapo, lakini baya zaidi utakuwa umeshakula pesa zetu chungu nzima za kodi.

Ukimpeleka mbuzi kuishi jangwani atashindwa kutembea juu ya mchanga laini miksa vumbi. Pia atashindwa kuvumilia wiki nzima bila kunywa japo maji kidogo. Lakini ngamia mwenye miguu kama viatu vya talawanda na nundu inayohifadhi pipa mbili za maji anadunda tu huko.

Siyo jambo rahisi kuwa ngamia aliamua kwenda kuishi huko ati kwa sababu alijiona akiwa na vigezo hivyo. Wala hauwezekani kwa wanyama kama simba na chui kujifunza kula wenzao ati kwa kuwa wamegundua zana zao. Ndiyo maana nasema hayo tumwachie Muumba.

Lakini utashuhudia kwenye zizi lenye ng’ombe mia, watatu ni vichaa. Utashangaa kuona vichaa hao wanafanana kwa kuwa na pembe ndefu kuliko wenzao. Utajiuliza kichaa chao ndicho kilichoongeza ukubwa wa pembe? La hasha. Kama ni hivyo kichaa wa Bongo angeumbwa kwa chuma.

Ukichungulia zizini utagundua kuwa ng’ombe huwaogopa wenzao wenye mapembe makubwa. Kila wanapowaona wakielekea pande zao huwakimbia kwa kudhani kuwa watawadhuru. Sasa hawa wenye mijipembe kwa kuwa hawajioni, wanabaki kushangaa na kujiuliza maswali ya tashwishi: “Hivi ni kweli mnanikimbia?”

Kama nilivyosema, wenyewe hawajioni kwa sababu hawana utamaduni wa kujipodoa mbele ya kioo. Hawajui tofauti yao na wenzao. Ili kujua ndiyo wanapowarukia wenzao ili kuona tofauti. Sasa ishu inakuja pale wanaporukiana wenyewe; badala ya kukimbiana linapigwa palingi mpaka mmoja afe! Utafiti unaonesha kila mtu ni kichaa. Utaachia mdomo wazi na kupiga “astakafiru” lakini ndiyo ukweli wenyewe. Maandiko yamesema kila kitu kinachozidi ndio huwa sumu, kero, kifu na hatari. Wale tunaowaona kuwa “saa mbovu” au “dishi limeyumba” ndio ambao kichaa kimekuwa “fulu geji”.

Kwa mfano nikisema kila aliye hai ana shinikizo la damu nipo sahihi kabisa. Wengine watashtuka maana neno “shinikizo” limekaa kufosifosi, halina ushirikiano. Lakini shinikizo (au msukumo) kwa Kiingereza ni pressure, sisi tunalitohoa kama “presha”. Hivyo kila aliye hai hakosi presha, ila inapozidi huwa ugonjwa.

Sir Isaack Newton aligundua kuwa kila maada hubaki katika hali yake ya utulivu pale ilipo mpaka itokee nguvu ya nje kuisukuma ndipo maada itasogea. Damu nayo hubaki katika utulivu mpaka moyo unapodunda ndipo huitembeza na kwenda kugawa virutubisho katika mwili. Nilishaonya kuwa mambo mengine tumwachie Mungu. Maswali ya “moyo unasukumwa na nini” kwa sasa siyo nafasi yake. Tuendelee na lililotuleta hapa.

Tuliishia wapi vile… Sawa, nilisema kila mtu ana kichaa. Lakini uzuri ni kwamba kila mtu ana kichaa chake. Hatusigani; kama zilivyo ncha za sumaku, zilizofanana husigana na zilizotofautiana huvutana. Tofauti na mnyama yeyote unayemjua (hata gendaheka) binadamu ana vichaa vingi usipime!

Kichaa cha binadamu hukizidi cha ng’ombe. Usemi wa “Mafahali wawili hawakai zizi moja” unatanabaisha kuwa hata wezi wawili wanapokutana saiti bila kutegemea patachimbika. Ndiyo maana nikasema uzuri wa uchaa wa watu ni sawa na ncha za sumaku.

Binadamu ni kama ng’ombe anayejitengenezea pembe. Yeye anataka zilizo kubwa kuliko za wote ili wenzie wamwogope jumla hata kama hana nguvu. Wapo vichaa wa mavazi, wa wanawake, wa magari, wa starehe... Unakuta mtu anaacha watoto wafukuzwe shule kwa ukosefu wa ada wakati yeye ananunua Ferrari modeli mpya.

Mtaani yupo Mkongo mmoja ana kichaa cha starehe. Siku moja nilimkuta anafanya uchakavu kwenye klabu ya usiku kule Upanga, mpaka leo nashindwa kuelewa kwa nini anasaidiwa chakula na malazi na swahiba. Alinipigia pamba ambazo hata Fally Ipupa hawezi kutinga.

Zamani zile vijana wetu walipandwa na kichaa cha uzungu. Kinadada walijikoboa ngozi na kuunguza nywele kwa kupaka, kuoga na kunywa makemikali. Midume nayo ilitengeneza shepu za “kipapaa” kwa kufosi bia kwa nyama choma asubuhi (nasikia inaleta kiriba tumbo). Wengi walishtuka baadaye kuwa kumbe ule sio ufahari, ila ni maradhi ya kujitakia. Sasa unategemea nini bibie aliyejikoboa anapodeti na mshefa halafu anapokutana naye laivu anaona kwashakoo? Kila mmoja atamkandia mwenzie na wajanja watafumbua siri. Wakaachana na ishu hizo.

Sasa siku hizi sijui kichaa ndo kimekuwa fulu geji? Manake habari ya mjini ni kinadada kuvimbisha makalio. Mimi huwa napata wasiwasi kuwa hivi sasa shetani mkuu kahamia jamvini petu. Haiwezekani kila siku tukajitengenezea sumu kali kuliko ya jana. Kwani tunajikomoa au tunakomoana?

Hakuna asiyejua ubaya wa magonjwa ya kitabia. Tofauti na magonjwa ya asili ambayo tiba zake zipo tangu enzi na enzi, magonjwa ya kutengenezwa hayajatengenezewa dawa. Ni nani aliyewahi kujikoboa ngozi halafu akaweza kuiotesha?

Mnaujua mwisho wake? Shauri yenu. Ni bora ufuge manywele kumzidi Jini Bahari kwa sababu yakikukera unanyoa dongo.