HOJA ZA MALOTO: Ya Omar al Bashir na unabii wa Barack Obama

Muktasari:

  • Obama alisema pale kiongozi anapoamua kubadili ili aendelee kubaki madarakani, huhatarisha mshikamano na kuibua migogoro kama ilivyo Burundi. Hivyo akatoa rai kwa viongozi kuachia madaraka wenyewe ili kujiweka mbali na hatari.

Julai 28, 2015 Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, kipindi hicho akiwa bado madarakani, aliwahutubia viongozi nchi za Afrika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Pia walikuwapo wakuu wa taasisi za kiraia, kidini na wageni wengine waliohudhuria mkutano huo.

Pamoja na kuisifu Afrika akisema na yeye ni mtoto wa Mwafrika, alipongeza hatua za maendeleo ambazo Waafrika wanapiga kutoka kuporwa mali zao na wakoloni na biashara ya utumwa, akitolea mfano makumbusho ya Jumba la Watumwa, Afrika Magharibi.

Obama alisema “Leo, demokrasia ya Afrika ipo kwenye hatari kwa sababu ya viongozi ambao wanakataa kutoka madarakani baada ya muda wao kwisha. Nataka niwe mkweli kwenu. Hili silielewi kabisa. Mimi nipo muhula wa pili, chini ya Katiba yetu, siwezi kugombea tena. Ila kwa katiba zenu ningeweza kugombea. Na najiamini ni Rais mzuri, hivyo ningeshinda.”

Aliendelea kusema kuwa alikuwa bado ana mambo mengi ya kufanya ili kuipeleka Marekani mbele. Hata hivyo alibainisha kwamba sheria ni sheria na hakuna aliye juu ya sheria, hata Rais. Akasema angeondoka madarakani, kwa hiyo angepata muda mrefu zaidi na familia yake. Angeihudumia nchi kwa namna mpya na kuitembelea Afrika mara nyingi.

Obama alisema pale kiongozi anapoamua kubadili ili aendelee kubaki madarakani, huhatarisha mshikamano na kuibua migogoro kama ilivyo Burundi. Hivyo akatoa rai kwa viongozi kuachia madaraka wenyewe ili kujiweka mbali na hatari.

Alisema kuna viongozi husema kuwa kubaki kwao madarakani ni kwa ajili ya kuendelea kuifanya nchi iwe moja. Akaonya kwamba kama kiongozi anakuwa anafikiri yeye peke yake ndiye anaweza kuifanya nchi kuwa na mshikamano, kiongozi huyo anakuwa amefeli kuijenga nchi yake.

Unabii wa Obama

Obama alisema kuwa viongozi wengi wanaong’ang’ania madaraka muda mrefu hufanya hivyo hasa wanapokuwa wameshatajirika. Hakwenda ndani sana kuchambua kauli yake, lakini bila shaka alifikisha ujumbe kwamba viongozi wakishachuma mali nyingi, huhofia wakitoka madarakani, ama watafilisiwa au watahojiwa walivyozipata.

Na hapa ndipo kwenye mantiki ya viongozi kung’ang’ania madaraka Afrika. Wengi wao wakishakosa namna, ama kwa Katiba kuwabana au uzee, huhakikisha wanaandaa warithi wao ambao watawahakikishia usalama baada ya kuachia ngazi. Mifano ipo mingi. Wengine huwaachia watoto wao uongozi.

Aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar al Bashir hivi karibuni aliondolewa marakani. Bashir alidumu madarakani kwa miongo mitatu. Aliingia kwenye mamlaka kijeshi kisha akawa kiongozi wa kikatiba. Baadaye akanogewa na kuamua kusalia madarakani kwa miaka 30 na hakuwa na dalili za kung’oka.

Habari ya kushtua ni kuhusu ndani ya nyumba ya Bashir kukutwa kiasi kikubwa cha fedha, dola 130 milioni (Sh312 bilioni). Ikiwa ni muunganiko wa noti za dola, Euro na pauni za Sudan.

Hizo ni pesa tu alizokuwa ameweka ndani, vipi alizohifadhi maeneo mengine. Inafahamika viongozi wengi Afrika huhifadhi fedha Ulaya hasa kwenye nchi zenye unafuu wa kodi na zisizo na sheria ngumu za usimamizi fedha, yaani offshore countries.

Hapo havijaguswa vitega uchumi vyake kabisa. Na inajulikana viongozi wengi Afrika ni wajanja wa huwekeza mali zao kwa kutumia majina ya ndugu zao. Kwa namna yoyote ile, mtu ambaye anaweza kuweka Sh300 bilioni nyumbani kwake, huyo bila shaka ana mali za matrilioni. Na hakuna namna ya kujitetea kwamba hizo siyo fedha za umma.

Alichokizungumza Obama ni tafsida tu, kwamba wakishatajirika hung’ang’ania madaraka. Lugha nzuri yenye kunyooka ni kwamba viongozi wengi Afrika ni wezi. Huwaibia wananchi chini ya mwavuli wa kuwahudumia. Inafikia hatua kiongozi anakuwa anadhani yeye ni mja aliyeshushwa na Mungu kuwasaidia wananchi anaowaongoza. Anasahau kuwa ameomba kuwatumikia.

Baada ya Bashir kuondoka kwa aibu madarakani na kukutwa na mabilioni ya fedha nyumbani kwake, nani anaweza kupinga kauli ya Obama? Hata Bashir alikuwa akiamini bila yeye Sudan haiwezi kuwa bora. Ndiyo maana hata baada ya kudumu kwenye mamlaka miaka 30 bado hakutosheka.

Viongozi wa Afrika wanahitaji msasa. Watambue kuwa nchi ni wananchi. Ni makosa makubwa kudhani bila wao nchi zao haziwezi kupiga hatua. Zaidi wafahamu ya kwamba shilingi 100 ya halali ni tamu kuliko dola 100 ya wizi. Sudan kulikuwa na watu ambao walikuwa bado na imani na Bashir.

Baada ya taarifa ya kukutwa na Sh300 bilioni, imani hiyo wanaweza vipi kubaki nayo?

Kiuchumi, alichokifanya Bashir ni kitu kibaya. Kwanza, amewaibia wananchi, pili, mabilioni hayo ya fedha kuyaweka nyumbani kwake yanazuia mzunguko wa kifedha kama yangewekwa benki au yangewekezwa katika uzalishaji. Kwa maana hiyo amefanya uhujumu mkubwa wa uchumi kwa Sudan.

Sh312 bilioni, kama Bashir angekuwa na matumizi ya fujo na kutumia Sh5 milioni kwa siku, angetumia kwa miaka 200. Umri huo anao? Atasema aliwaandalia watoto wake. Miaka 200 ijayo, hakuna mtoto wa mjukuu wa Bashir atakuwa hai. Vema kuwarithisha watoto maisha salama na yenye amani kuliko fedha za damu.