Halimoja: Mwandishi mkongwe anayelia kudhulumiwa haki

Ana historia ya kipekee ikiwamo kuwa Mtanzania wa kwanza kwenda kusomea masuala ya uandishi na uchapishaji wa vitabu miaka ya 1960.

Aliporudi akaitendea haki elimu aliyoipata kwa kutunga vitabu zaidi ya 30 vikiwamo kadhaa vilivyowahi kutumika katika mitalaa shuleni.

Hata sasa kitabu chake kiitwacho: Historia Darasa la 7 kinaendelea kutumia katika shule za msingi.

Kama haitoshi, Yusuf Halimoja ambaye sasa ana miaka 84 anajivunia kuwa mmoja wa wajumbe wa bodi iliyopendekeza kuanzishwa kwa kijiji cha Makumbusho kilichopo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, pamoja na mchango wake, Mzee Halimoja ambaye sasa anaishi kwa kusitiriwa na wasamaria wema, anasema amekuwa akidhulumiwa haki za vitabu vyake.

Umuonapo akitembea au akiwa amekaa, lazima utabaini kuwa ni mtu aliyechoka. Kichwa kimejaa mengi akifikiri hali ya maisha ya sasa. Huyu sio Halimoja yule wa zamani ambaye historia yake inaonyesha kuwa aliwahi kushika fedha nyingi kiasi cha kuwa mfadhili wa makanisa.

“Nisingekuwa hapa nilipo, nimefika kwa sababu ya kudhulumiwa haki zangu, hiki kitabu cha darasa la saba cha Historia kinachotumika sasa sijawahi kulipwa hata senti moja, namuomba Rais John Magufuli anitazame mimi mzee,” anasema na kuongeza:

“Nimekuwa mwandishi mzuri na mwaminifu sana lakini matokeo yake hata kitabu changu nilichoandika mwenyewe natakiwa kununua wakati hata hiyo pesa ya kununulia sina. Kuna wanafunzi wengi sana wanaweza kujivunia vitabu vyangu lakini hawajui mimi mwenyewe, hali yangu kama ni duni,” anasema.

Anasema mwaka 2011 vitabu vyake vinne vilipitishwa na iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutumika shule za msingi.

Vitabu hivyo ni Historia darasa la saba- mwanafunzi, Historia darasa la saba- mwalimu, Uraia darasa la saba- mwanafunzi na Uraia darasa la saba-mwalimu.

‘Vitabu hivi nikilipwa haki yangu hakika sitakuwa nilivyo, miaka nane sasa nahangaika tu kufuatilia bila kuambulia chochote,” anasema.

Vitabu vingine ambavyo Mzee Halimoja aliwahi kuviandika ni Nchi Yetu Tanzania, Historia ya Utawala, Chama cha Mapinduzi, Miongozo ya CCM, Serikali Kuu, Serikali za Miji, Serikali za Vijiji, Mahakama, Tume ya Kudumu ya Uchaguzi, Uchumi wa Taifa na Huduma za Kijiji

Vingine ni Mipango ya Maendeleo, Mashirika ya Umma, Ulinzi na Usalama, Uhusiano wa nchi za Nje, Sifa za Mwalimu Bora,Tanzania Inavyotawaliwa na Utamaduni wa Taifa

Historia yake

Mzee Halimoja ndiye Mtanzania wa kwanza kupata mafunzo ya uandishi, uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya shule nchini Uingereza mwaka 1964 mpaka 1965.

“Huo ulikuwa mwanzo wangu wa kupenda kuandika na ninamshukuru Mungu nilifanya vizuri darasani,” anasema na kuongeza kuwa elimu hiyo ilimfanya ateuliwe kuwa ofisa wa vitabu wa kwanza mwenye asili ya Afrika.

Anasema wakati anateuliwa kwenda nchini Uingereza alikuwa mwalimu wa sekondari, hivyo, haikuwa vigumu kwake kuwa mwandishi mzuri wa vitabu.

Ajiunga na UMATI

‘Wakati nafanya kazi kama ofisa vitabu niliamua kujiunga na Chama cha Uzazi wa Mpango (UMATI) baada ya Wazungu kufungua tawi, ilibidi niache kazi na nijiunge na shirika hili,” anasema.

Anasema japo Umati ilipingwa vikali aliona faida za kuwepo kwa shirika hilo hasa katika suala la uzazi wa mpango.

“Siku zote niliamini mama akizaa kwa kupangilia uzazi kwa kupishanisha watoto angalau miaka miwili anaweza kuwa na afya bora. Lakini familia yake itaweza kuwahudumia watoto kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya msingi,” anasisitiza.

Arudi serikalini

Alipotoka Umati anasema alipata nafasi ya kuwa ofisa habari wa iliyokuwa Wizara ya Utamaduni, huku akiwa na jukumu la kutangaza vipindi vya historia na utamaduni.

Halimoja anasema aliwahi kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Makumbusho ya Taifa na kazi kitu pekee anachokumbuka ni kuwa mmoja wanabodi walioanzisha kijiji cha Makumbusho mwaka 1992.

Je, Taifa linatambua mchango wake?

Halimoja anasema hajui hata kama anakumbukwa licha ya jitihada zake za kuandika vitabu vilivyoweza kubadilisha maisha ya watu.

“Ni swali gumu sana umeniuliza labda lingeulizwa Taifa lenyewe linanitambua? Binafsi naweza jibu linanitambua ndio maana lilipitisha vitabu vyangu vitumike kufundishia na vinatumika bado japo mie mwenyewe naisha maisha magumu,” anasema.

Wasifu wa elimu yake

Anasema alimaliza elimu ya sekondari mwaka 1953 kabla ya kujiunga na chuo cha ualimu cha Minaki na kuanza kufundisha kati ya mwaka 1955 mpaka 1961.

Aliwahi kuwa mwalimu wa shule za sekondari za Mindu, Luatala na Migongo wilayani Tunduru kabla ya kwenda nchini Uingereza kusomea masuala ya vitabu.