Hamad: Mapema kuulaumu utawala wa Rais Magufuli

Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed ametathmini miaka mitatu ya utawala wa Rais John Magufuli na kusema kwa kipindi kifupi haupaswi kulaumiwa kwa lolote kwa kuwa kila zama na kitabu chake.

Hamad ambaye pia ni Waziri wa Afya wa SMZ, amesema hayo alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusiana na mtazamo wake juu ya miaka mitatu ya Rais Magufuli madarakani.

Anasema tangu utawala wa awamu ya kwanza, watu ni walewale, katiba ileile na taratibu ni zilezile, lakini viongozi wamekuwa wakibadilika kulingana na mahitaji au mazingira ya wakati husika, hivyo baadhi ya mambo yanayopewa kipaumbele yanaweza kuwa tofauti.

Mwanasiasa huyo alijenga hoja yake kwa kufanananisha na mambo aliyoyafanya Mwalimu Julius Nyerere katika awamu ya kwanza na yale yanayofanyika sasa.

“Wapo walioona siasa ya ujamaa imepwaya na kutaka ibadilishwe, kila mmoja alitumia njia zake katika kuongoza,” anasema.

Katika kulinganisha, Hamad anajiuliza swali na kutoa majibu yake, “Je, Rais Magufuli ndani ya miaka mitatu amepambana na rushwa? Ukimtazama jawabu ni kweli anapambana na rushwa na ufisadi ingawa aina ya mapambano yanatofautiana kati ya awamu ya kwanza, ya pili, tatu na nne,” alisema.

Anasema Dk Magufuli amejitokeza waziwazi kupambana na rushwa, akilinda rasilimali za nchi na kuwazindua wananchi kama alivyofanya Mwalimu Nyerere wakati wake, ingawa wapo waliomuona hataki kutumia rasilimali za nchi huku yeye akihitaji kwanza upatikane ufahamu na taaluma kwa Watanzania.

“Utawala wa Rais Magufuli umejitahidi kuwaelimisha wananchi kuhusu mantiki ya haki na usawa, kupambana dhidi ya uonevu, manyanyaso na dhuluma chini ya misingi iliyowekwa.

“Nataka nitoe mfano mmoja. Mwaka 1983 ujambazi ulikuwa juu. Nikiwa naibu waziri wa Mambo ya Ndani, mama mmoja alipigwa risasi mchana hadharani pale Kisutu. Mwalimu akaniita Msasani. Akaniuliza, ‘Hamad kwa nini watu wanakufa hovyo’. Nikamjibu watazidi kufa. Akasema kwanini unanijibu hivyo. Nikamwambia nina gari moja la polisi nashindwa kuimarisha ulinzi. Akaiambia nenda,” alisema Hamad.

Anasema ilipofoka saa 9 alasiri aliitwa tena na Rais alipofika akamkuta Waziri Mkuu Cleopa Msuya na katibu wa kamati ya ulinzi na usalama, Edward Sokoine (marehemu). Ikaamriwa mashirika yote ya umma yatoe magari kwa polisi ili yafanye kazi ya kuimarisha ulinzi.

Akitoa mfano mwingine, Hamad anasema, “Wakati fulani nilimshauri Mwalimu Nyerere aruhusu polisi watembee na silaha mitaani. Akaniambia hapana. Akanieleza ‘You need to create a violent society’ (unataka kutengeneza jamii ya vurugu).

Akasema wakoloni waliwavisha polisi tarabushi nyekundu wakaogopwa. Wakapewa magongo wakachukiza. Sasa mkitaka kuwapa silaha polisi itafika mahali wananchi hawataogopa silala na hiyo itakuwa hatari.

“Leo baadaa ya miaka mingi kupita nayashuhudia maneno yale ya Mwalimu Nyerere. Watu sasa hawaogopi jela, polisi wala bunduki. Hawaogopi kutekwa wala kukamatwa au kuwekwa ndani. Hakuna haja ya kutumia nguvu nyingi bali tutoe elimu ili watu watii sheria bila kuvunja misingi iliyowekwa,” aliongeza Hamad.

Anasema Watanzania ni wasikivu na watulivu hivyo hakuna haja ya kuwabadili kifikra na kiakili ili kuwafanya wawe manunda, kuwapa usugu na hatimaye kuwa watu wasiosikia maneno bali watii jambo lolote kwa mazingira ya ridhaa na utashi bila kutumia nguvu nyingi.

Demokrasia finyu

Kuhusu demokrasia, Hamad anasema ni vyema kwanza kuutazama utawala wa Nyerere na uongozi wake na kwa maoni yake haiba ya demokrasia na siasa huenda wakati wa mfumo wa chama kimoja ilikuwa pana na imara zaidi kutokana na utashi wa Serikali kuheshimu mihimili mingine kama Bunge na vyombo vya dola.

“Mwaka 1983 nilipeleka bungeni sheria ya Nguvu Kazi ambayo ilipita kwa kura moja. Nakumbuka kabla ya kura kupigwa nilimhimiza na kumtaka Sukwa Said Sukwa awahi kupiga kura. Sokoine akaniuliza kama sheria hiyo kwa mtazamo wangu ingepita. Nikamwambia itapita.

“Tazama hata wakati wa mfumo wa chama kimoja bado utawala wa Mwalimu Nyerere uliheshimu Bunge. Kuheshimu vyombo vya kitaasisi ni jambo la msingi lisilohitaji kuchengwa na yeyote kwani ndiyo sauti zinazowawakilisha wananchi,” alisisitiza Hamad ambaye aliwahi kuwa mbunge na waziri kwa vipindi kadhaa.

Mwasiasa huyo ambaye kabla ya kuwa Waziri wa afya alikuwa waziri wa kilimo, maliasili, mifugo na wvuvi Zanzibar, alisema kwa mtazamo wake wakati wa mfumo wa chama kimoja mazingira yaliendelea kuheshimu sheria na kwamba wakati mwingine unatamani mfumo wa demokrasia uliokuwapo ungebaki kwani ulisaidia kujenga uwazi na uwajibikaji.

Anasema Nyerere katika wakati wake aliheshimu matakwa ya sheria na katiba ya nchi. Alijilinda kuingilia vyombo vya sheria, mahakama na bunge kwa lengo la kuonyesha uwazi na uhuru zaidi.

“Magufuli anavipatia fedha vyombo vya sheria na kuvitaka vitende haki lakini bado hakujaonekana nuru ya uwazi wake au uwajibikaji unaofaa, utendaji na usimamizi unaojenga imani kwa watu wengi,” alisema.

Hamad anasema Rais Magufuli ana wajibu wa kuheshimu sheria za nchi zilizopitishwa na Bunge. “Tuna sheria iliyoruhusu vyama vingi. Haiwezekani katikati ya sheria baada ya kupitishwa isitumike ipasavyo. Kama kuna kasoro zinazohitaji kurekebishwa, zirekebishwe ili yanayofanyika yafanyike kwa mujibu wa sheria.”