Harufu mbaya ya kinywa inavyowatesa watu wengi

Friday August 10 2018

 

Sina uhakika sana kama unafuata utaratibu wa kusafisha meno na kinywa kwa kama inavyotakiwa. Wakati mwingine fizi zako zinaweza kuashiria kama kuna kitu hakipo sawa lakini unaweza usichukulie ni tatizo.

Hati-maye, unaanza kupata ile harufu mbaya na nzito kutoka mdomoni mwako. Lakini mbaya zaidi, ile harufu huambat-ana na matone ya damu kutoka kinywani mwako na hapo sasa unaanza kushtuka na kuhisi kuwa una tatizo mdomoni mwako.

Hiki ndicho kilichotokea kwa John (sio jina lake halisi) kijana mwenye umri wa miaka 30 ambaye amekuwa akisumbuliwa na tatizo la harufu mbaya ya kinywa kwa takribani miaka zaidi ya mitano. Lakini cha ajabu zaidi, kitendo cha yeye kutokwa na harufu mbaya ya kinywa kwa miaka yote hii, hakuchukulia kama ni tati-zo linalohitaji msaada wa kitabibu hadi lilipozidi na hatimae kuanza kutoa damu kwenye fizi zake na hapo ndipo aliposhtu-ka na kuwahi hospitali kwa ajili ya msaada wa kitabibu. Nilikutana na kijana huyu kwenye hospitali ninayofanyia kazi na baada ya kumpokea kwa ajili ya kuanza kumhu-dumia, nilishtushwa na ukweli kwamba john hajawahi kumuona daktari kwa aji-li ya huduma ya afya ya kinywa maisha yake hadi alipoanza kutokwa na damu kinywani. “kwa kweli daktari sikuwahi kufikiria kama harufu mbaya ya kinywa ni tatizo la kiafya ambalo lingehitaji msaada wa wa daktari, ila baada ya kuanza kuto-kwa damu nimeogopa sana na nikaona ni vyema niwahi hospitali ili nipate msaada. Nina hofu isije likawa tatizo kubwa,” john aliniambia.

Nikachukua kifaa kinachoitwa ‘pen torch” kwa ajili ya kumfanyia uchungu-zi kabla ya kumpeleka idara ya afya ya kinywa na meno kwa matibabu zaidi.Hata hivyo, utafiti mbalimbali unaonye-sha vijana wengi wanakosa uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya afya ya kinywa na hasa namna ya kukabiliana na tatizo la harufu mbaya ya kinywa. Utafiti uliofanyika hivi karibuni uli-opewa jina la ‘prevalence and correlates of perceived oral malodor’ katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam, ulilenga kufuatilia ukubwa wa matatizo ya afya ya kinywa.Ulikuja na majibu kuwa elimu zaidi inahitajika ili jamii ielewe kuwa mata-tizo yanayojitokeza kinywani, ni ya kiafya kama yalivyo mengine na yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito wake tofauti na watu wanavyofikiria.

Utafiti huo ulifanyika baada ya kubaini-ka kuwa watu wengi wanapata matatizo mbalimbali ya kiafya yanayoathiri afya ya kinywa bila wao kujua.

Harufu mbaya ya kinywa ni nini?

Hii ni hali inayotafsiri kinywa kutokwa na harufu nzito na mbaya. Ikumbukwe kuwa kinywa cha binadamu hakikuumbwa kutoa harufu, lakini kutokana na sababu na vihatarishi mbalimbali, tatizo hili hujitokeza.

Takwimu zinaonyesha takribani watu saba kati ya 10 wanaugua au wamewahi kuugua tatizo hilo.

Husababishwa na nini

Kinywa cha binadamu kimeundwa na mamia ya bakteria (oral micro flora) ambao ni rafiki kwa afya ya kinywa. Lakini kinachotokea, kila wakati unapokula kitu chochote kile, ujue unatentegeneza hatari ya kile ulichokitafuna au kunywa.

Mara nyingi hutengeneza utando juu ya meno kutokana na mabaki ya kile ulichokila.

Utando huu kwa kisayansi unaitwa ‘plaque’, huwa unazidi kujiimarisha kadiri mtu anavyokula na hasafishi kinywa kwa usahihi.

Wale bakteria ambao ni rafiki kwa afya ya kinywa, hupambana na utando huo na kusababisha kinywa kutoa harufu mbaya hasa pale bacteria hao wanapozidiwa nguvu na utandao huo uliotokana na mabaki ya vyakula kwa muda mrefu.

Hali hii mara nyingi husababishwa na kutosafisha kinywa mara kwa mara.

Sio tu kupiga mswaki, lakini ni muhimu pia kuzingatia ni mara ngapi unapiga mswaki kwa siku?

Hicho ndicho kitu muhimu cha kuzingatia. Watu wengi wanaamini kwamba, wanapaswa kusafisha vinywa vyao mara moja au mbili kwa siku.

Lakini utaratibu unaopaswa kuzingatiwa na unaoshauriwa na matabibu, mtu anapaswa kupiga mswaki kila mara.

Kwa mfano, mtu anakula chakula mchana, lakini anakuja kupiga mswaki usiku anapotaka kuingia kulala.

Hali hii si sahihi, kwasababu inatoa nafasi kwa vijidudu na mabaki ya chakula kujijenga kwenye fizi na ukipiga mswaki usiku hutaweza kuvitoa vyote kama inavyodhaniwa.

Hivyo, ni muhimu kuazingatia usafi wa kinywa wakati wote. Kama mtu utapata chakula cha mchana ukiwa nje ya nyumbani sehemu ambayo huwezi kupiga mswaki, ni vema ukasukutua mdomo kwa kutumia maji mengi.

Kuwa makini na unachokula

Sambamba na vihatarishi vinavyotokana na mfumo wa maisha vinavyochangia kwa kiwango kikubwa tatizo la harufu mbaya ya kinywa ni pamoja na kutozingatia usafi wa kinywa, uvutaji wa sigara na unywaji pombe.

Pia, ulaji wa baadhi ya vyakula huchangia kutokea kwa tatizo hilo na hasa kama vinaliwa mara kwa mara.

Mabaki ya vyakula vilivyomeng’enywa kwa meno vinaweza kubaki kwenye meno nakusababisha harufu mbaya ya kinywa.

Baadhi ya vyakula hivyo ni vitunguu maji, vitunguu saumu, vyakula vya wanga na vyenye kiwango kikubwa cha sukari hasa vilivyochakatwa na unywaji wa kahawa na vinywaji vingine vyenye ‘caffeine’ husababisha kwa kiasi kikubwa harufu mbaya ya kinywa.

Wataalamu wanasemaje kuhusu tatizo hili?

Shreyanshi Khanna, daktari bingwa wa kinywa na meno kutoka Hospitali ya TMJ Super specialized polyclinic, anasema tatizo la harufu mbaya ya kinywa huwapata watu wengi lakini hawatilii maanani.

Anasema asilimia kubwa ya watu hawana utamaduni wa kusafisha ulimi wakati wa kupiga mswaki.

“wa bahati mbaya, watu hawajui kama harufu mbaya ya kinywa kwa kiasi kikubwa inatokana na bakteria wanaotengeneza makazi yao sehemu ya nyuma ya ulimi.

Daktari huyo anasema ni vema kusafisha ulimi na ni rahisi. Anasema mtu anaweza kuusafisha kwa kutumia mswaki au kifaa maalumu kinachoweza kupatikana kwa wataalamu wa kinywa na meno.

Matatizo mengine ya kiafya yanayochangia harufu mbaya ya kinywa

Pamoja na sababu zote zilizoainishwa hapo juu, harufu mbaya ya kinywa inaweza kusababishwa na matatizo mengine ya kiafya, hivyo kuifanya harufu mbaya ya kinywa kuwa kama ni dalili ya matatizo hayo.

Matatizo haya ni pamoja na maradhi ya figo, kisukari au hata matatizo yanayoathiri mfumo wa chakula na hasa vidonda vya vya tumbo.

Uwapo wa matatizo haya unasababisha kwa kiasi kikubwa mdomo kuwa mkavu na kuufanya utoe harufu.

Hii ni kwasababu mdomo unakosa kiwango cha kutosha cha mate hivyo kuufanya utoe harufu.

Dk Shreyanshi anashauri kama mtu anatatizo la kutokwa na harufu mbaya mdomoni inayodumu kwa muda mrefu,

ni vema akawahi hospitali kuonana na daktari wa kinywa na meno kusudi kubaini sababu inayochochea hali hiyo kuwapo.

Kuwa mwema kwa fizi zako

Watu wengi wanatabia ya kutumia vijiti ‘toothpick’ kuondoa mabaki ya chakula kwenye fizi na meno.

Matumizi hayo si sahihi na ni hatari kwa kinywa chako.

Kama mtu atabaini kuwa anahitaji kutumia vijiti hivi, hii ni ishara kuwa meno yako yameshaanza kutengeneza nafasi kati ya jino moja na lingine na hapo ndipo unapohitaji kumuona daktari wa meno.

“Kinachotokea ni kwamba, unapotumia kijiti, unaanza kuzitoboa na kuzijeruhi fizi na zinaanza kutokwa na damu ndani kwa ndani hata kama hautogundua na lile eneo la fizi linapanuka, linazidi kutengeneza shimo la kuruhusu mabaki zaidi ya chakula na mazalia ya vijidudu kutokana na kutokwa na damu. Hapo ndipo tatizo la harufu mbaya ya kinywa linapozidi,” anasema Dk Shreyanshi.

Hivyo ni vema kuepuka kutumia vijiti ili kujilinda na tatizo la harufu mbaya ya kinywa.

Advertisement