UCHAMBUZI: Hasara zimekuwa nyingi Bunge kutokuwa ‘live’

Wananchi kwa sasa hawashuhudii kwa uwazi namna wawakilishi wao wanavyowajibika bungeni. Hii ni kwa sababu matangazo ya moja kwa moja ya Bunge yalisitishwa tangu Januari 2016.

Wapigakura hawaoni namna wabunge waliowatuma kuisimamia Serikali, wanavyotenda kazi hiyo au wanakuwa timu moja na Serikali? Hii ni hasara ya Bunge kutorushwa moja kwa moja.

Maisha ya watu yanajadiliwa lakini wahusika hawaoni. Wanaona vipande mitandaoni kwa wale wenye fursa. Hawajui wabunge wao wamechangia nini.

Miswada ya mabadiliko ya sheria na uanzishwaji wa sheria mpya inapelekwa bungeni, inajadiliwa, wabunge wanalumbana kisha inapitishwa, lakini mwananchi anakuwa hajui chochote.

Laiti Bunge lingekuwa live, mwananchi angeweza kuelimika kuhusu uzuri au ubaya wa sheria kupitia michango ya wabunge. Na pengine angekuwa anafahamu kwa ukaribu kama mbunge wake ametoa mchango mzuri au mbaya.

Mwananchi angeelewa sheria iliyopitishwa ni nzuri au mbaya na faida au hasara zake.

Badala ya sasa hivi anasikia tu imepitishwa Sheria ya vyama vya siasa, halafu yanaibuka malumbano ya pande mbili. Tena malumbano siyo ya kitaalamu, bali vijembe na kukomoana. Kuzomeana na kuoneshana umwamba.

Bunge lingekuwa ‘laivu’ mwananchi angeona wabunge wanavyolumbana kwa hoja na kuelewa je, sheria iliyopitishwa ni kwa maslahi yake na Taifa zima, au imewekwa kwa makusudi maalumu ya kisiasa? Hii ni hasara iliyo wazi.

Vipi sheria ya huduma ya vyombo vya habari, takwimu na nyinginezo zilizopitishwa? Michango ya wabunge ingemwezesha mtazamaji kutambua mambo mawili. Mosi, mantiki ya sheria zenyewe katika uwanda mpana. Pili, namna mbunge wake anavyoitumikia tiketi aliyompa kupitia sanduku la kura.

Hivi karibuni Bunge lilijadili ripoti ya Hesabu za Serikali na ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha Sh1.5 trilioni ambazo hazikuonekana matumizi yake katika bajeti ya mwaka 2016-2017. Wananchi wangejionea mengi kama Bunge lingekuwa ‘laivu’.

Mwananchi angepigwa na butwaa kuhusu hitimisho la Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) kuwa utata wa fedha Sh1.5 trilioni uliondoka baada ya Serikali kuweka sawa hesabu zake. Wakati huohuo kuna wabunge kupitia ripoti ya CAG, wakaibua hoja nyingine za utata wa mabilioni ya fedha. Yupo aliyeibua Sh2.4 trilioni.

Bunge lingekuwa ‘live’, mwananchi angejionea ni nani mkweli. Je, PAC au wabunge waliosema kuna ubadhirifu serikalini? Angetambua kama kweli CAG alisema utata wa Sh1.5 trilioni umeondoka au alisingiziwa.

Lipo ombi kuwa ripoti ya CAG ipelekwe bungeni ili wabunge waijadili moja kwa moja badala ya kutegemea uchambuzi wa PAC. Ombi hilo lilikataliwa. Kama Bunge lingekuwa live mwananchi angetambua mbivu na mbichi kuhusu zuio hilo.

Hasara ni nyingi. Bajeti hupitishwa, mwananchi angeona kwa uwazi. Kuna wabunge hutumia muda wa thamani ndani chombo hicho kufanya siasa badala ya kuwatetea wananchi. Angemuona kwa urahisi mbunge wake ambaye hufanya ambacho hakumtuma.

Faida chache

Hivi karibuni wakati wa mjadala wa mapambano dhidi ya Ukimwi, iliibuka hoja kuwa mashine zifungwe bungeni ili kutambua wabunge wanaume ambao hawajatahiriwa. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Ngonyani aliianzisha na kupewa taarifa na mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kwa kutolea mfano wa Kenya.

Bunge likaingia kwenye hoja ya wabunge kukaguliwa kama wametahiriwa. Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku ‘Msukuma’ naye akachangia kwamba wabunge wanawake nao wawekewe mashine ili wajulikane ambao wamekeketwa.

Hoja hiyo ni moja ya zile ambazo huleta maana ya Bunge kutorushwa moja kwa moja. Fikiria wananchi wanakaa kwenye runinga na watoto wao wanatazama Bunge ambalo wabunge wake wanalumbana eti kujua wabunge ambao hawajatahiriwa na waliokeketwa.

Mwananchi anajua kuwa Septemba 7, 2017, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alipigwa risasi nyingi na aliumizwa vibaya. Ni mwaka na zaidi ya miezi mitano sasa tangu shambulio hilo lilipotokea, na halijapatiwa ufumbuzi.

Mwananchi anafahamu kuwa suala la Lissu siyo la kisiasa bali linahusu utu na haki za binadamu. Anaona kuwa anahitaji kuhurumiwa na kupewa faraja badala ya kusimangwa na kukejeliwa.

Mshangao wa mwananchi ni kuwa Bunge halitoi fedha za matibabu licha kuumia mazingira ya Bunge na sheria inataka Bunge limtibu.

Hata hivyo, Bunge husema familia yake na chama chake, walikiuka utaratibu wa kumpeleka Nairobi badala ya Muhimbili, kwa hiyo inabidi ajitibu mwenyewe.

Wakati hali ikiwa hivyo, mbunge anasimama kuomba Lissu asimamishiwe mshahara kwa sababu haonekani bungeni.

Lissu kwa sasa anatembea kwa magongo na anaeleza operesheni ya 23 inamsubiri.

Mwananchi anapomuona mbunge mwenye kuomba Lissu asitishiwe mshahara bila shaka angeona namna utu unavyotoweka kwa Watanzania na kuwa siasa zina nguvu kuliko utu. Angalau hili hakuliona, maana Bunge halipo live.