Hata Lissu hapendi ziara za Marekani na nchi za Ulaya

Saturday February 9 2019

 

By Luqman Maloto

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anaendelea kuchanja mbuga Ulaya na Marekani. Anafanya mahojiano kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu hali ya kisiasa nchini.

Hatimaye, Lissu ambaye ni mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amegeuka maudhui ya ulimwengu kuhusu siasa za Afrika. Jinsi vyombo vya habari vya kimataifa vinavyomwalika na kumpokea, ni dhahiri wanamchukulia ni mfano wa siasa za Afrika.

Ziara za Lissu zinaionyesha Tanzania katika sura ambayo si nzuri katika demokrasia na utawala bora. Inakuwa mara ya pili nchi kuonekana hivyo kimataifa kama ilivyotokea Januari 26 na 27, 2001, watu kadhaa walipouawa Zanzibar na wengine kujeruhiwa katika maandamano ya CUF, huku makumi wakikimbia nchi kwenda kuwa wakimbizi Mombasa na Lamu, Kenya.

Miaka 18 baadaye, Tanzania inakuwa mfano mbaya wa kisiasa. Lissu anazunguka kuzungumza yenye kumuumiza kuhusu nchi yake. Si kwamba hajui kuwa nchi yake inachafuka. Bila shaka anajua na hapendi lakini labda ameona ndiyo njia sahihi kwa wakati uliopo.

Anachokifanya Lissu, tulizoea kukiona kikitekelezwa na wanaharakati wa mataifa mengine. Mfano wa hivi karibuni zaidi ni mbunge wa Kyadondo Mashariki mwa Uganda, Robert Kyagulanyi “Bobi Wine”, alikwenda Marekani kwa matibabu ambaye pia aliutumia muda huo kuzungumza na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu nchi yake.

Bobi Wine aliumizwa baada ya kupewa mateso alipowekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa. Baada ya kupata dhamana alikwenda Marekani kutibiwa. Akatumia nafasi hiyo kueleza namna polisi wanavyoua watu. Alisimulia mauaji ya kisiasa, uminywaji wa uhuru na demokrasia.

Lissu akiwa kwenye mahojiano naye anasimulia jinsi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai, vilevile Kiongozi wa Kambi ya Upinzani pamoja na mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko walivyonyimwa dhamana na kukaa mahabusu.

Uwepo wa Mbowe na Matiko mahabusu, Lissu anauelezea kuwa ni sababu za kisiasa. Wakati huohuo, muungano wa vyama 10 vya upinzani nchini, mwishoni mwa mwaka jana, vilitoa tamko kuwa Freeman Mbowe na Esther Matiko ni wafungwa wa kisiasa.

Lissu anazungumzia matukio ya Kibiti, kupotea kwa Ben Saanane (kada wa Chadema) na Azory Gwanda (mwandishi wa habari), vilevile kuuawa kwa risasi aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, kama sehemu ya madhila ya kisiasa.

Lissu alipofanya mahojiano BBC, kipindi cha HARDtalk, mtangazaji Stephen Sackur alimuuliza kwa nini amefika mbali kuiita Tanzania ni “skunk of the world” (kitu kinachonuka ulimwenguni).

Maneno skunk of the world, yalitumiwa na Rais wa kwanza mzalendo, Afrika Kusini, Nelson Mandela, alipokuwa akilitambulisha taifa lake, kipindi nchi hiyo ilipokuwa imekumbatia siasa za ubaguzi wa rangi.

Unadhani Mandela aliposema hivyo alikuwa haipendi nchi yake? Aliipenda Afrika Kusini, alikuwa tayari kuifia na alikaa jela miaka 27 kwa ajili ya kuipigania. Tatizo mfumo uliokuwepo ulimfanya atoe maneno hayo. Bila shaka Lissu naye anaipenda Tanzania, ila ndani yake anaona kuna maumivu makali.

Katika mahojiano yake, Lissu anazungumzia tukio la kupigwa risasi 16 zilizopenya mwilini kati ya 38 zilizolitoboa gari lake. Anaumia kuona baada ya tukio hilo, hajawahi kuona taarifa yoyote ya polisi kuhusu upelelezi wa jaribio la kumuua.

Suala jingine liko katika matibabu. Mbunge anastahili kutibiwa na Bunge, ndani ya nje ya nchi. Pia, lina makubaliano na Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF) kuhusu kuwatibu wabunge. Utaratibu wa bima ni kuwa mgonjwa hupewa rufaa ya kutibiwa nje na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mbowe aliwahi kutoa taarifa kwamba kulitokea ubishani kuhusu ama Lissu apelekwe Muhimbili au Nairobi. Familia ya Lissu na viongozi wa Chadema, waliona Muhimbili si salama kwake, kwa hiyo walitaka apelekwe Nairobi. Spika wa Bunge, Job Ndugai na Serikali walishauri aende Muhimbili kama yalivyo matakwa ya NHIF.

Mwisho, Lissu alipelekwa Nairobi. Na hakukuwa na kificho kuhusu wasiwasi wa maisha yake, kwani bila shaka wahusika walilenga kumuua. Baada ya hapo Bunge halijamhudumia matibabu.

Lissu anaamini kesi yake ilikuwa ya kipekee kutosha kuvunja utaratibu wa NHIF. Hivyo, isingefika mwaka mmoja na miezi mitano pasipo Bunge kuhusika vyovyote vile na matibabu yake, wakati alishambuliwa akiwa kazini. Lissu anasikitishwa kuhusu hili, na anapofanya mahojiano na vyombo vya kimataifa, analisema kwa hisia.

Upelelezi wa kesi yake ni tatizo. Analalamika kuwa kulikuwa na kamera za usalama (CCTV Camera) kwenye nyumba za Serikali ambazo anaishi akiwa Dodoma kikazi. Anadai ziling’olewa baada ya tukio. Ni dhahiri picha za CCTV zingesaidia kuwaona watu waliomshambulia.

Lissu anasema pia kuwa ulinzi kwenye nyumba hizo ni saa 24, lakini siku aliposhambuliwa hakukuwa na ulinzi kabisa. Alipohojiwa na Sauti ya America, kipindi cha Straight Talk Africa, Lissu alitoa tuhuma kwamba walinzi waliondolewa ili kurahisisha yeye kushambuliwa.

Polisi hawajawahi kujibu tuhuma za CCTV kung’olewa na ulinzi kuondolewa lakini Serikali imekuwa ikisisitiza arejee ndipo na dereva wake ili upelelezi ufanyike. Je, ndivyo taaluma inasema? Kama Lissu na dereva wake wangeuawa siku ya tukio, kusingekuwa na upelelezi kabisa?

Kimsingi nchi inachafuka sana. Leo ni Lissu, jana Seif Sharif Hamad, malalamiko ya hali ha kisiasa kwenye jumuiya za kimataifa. Na suluhu si kingine bali mazungumzo.

Nimeona Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ameitisha mazungumzo na viongozi wote wa kisiasa ili kujenga maridhiano ya kitaifa. Naamini hata Tanzania inawezekana, ni utayari tu.

Advertisement