Hata nawe unaweza kufuga konokono

Ni dhahiri msomaji utapatwa na mshangao usomapo kichwa cha habari cha makala haya.

Hata hivyo, huo ndio ukweli. Konokono wanafugwa na pengine usichokijua ni kuwa ufugaji wake unaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato.

Kwa Tanzania ufugaji huu unaweza kuonekana mgeni licha ya baadhi ya watu kujaribu lakini wakaishia njiani. Lakini kwa Rosemary Odinga anayeishi nchini Kenya habari ni tofauti. Kwake konokono ni fedha na wanampa fedha sio mchezo.

Rosemary ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alianza kufanya biashara hiyo mwaka 2007 aliporudi nchini Kenya akitokea Nigeria.

Anasema alikwenda kumtembelea Rais mstaafu wa nchi hiyo, Olesegun Obasanjo ambaye ni mmoja wa wafugaji wakubwa wa kilimo cha konokono nchini humo.

Anasema aliporudi Kenya alianza kufanya udadisi kuhusu konokono ikiwamo kutembelea Chuo Kikuu cha Nairobi na kukutana na mtaalamu mmoja wa wadudu hao aliyemsaidia kuwafahamu na pia alimpa konokono 12 kama mtaji katika biashara yake.

Rosemary anasimulia kwamba konokono 10 kati ya hao walikufa kutokana na joto, lakini alipogundua hilo aliwatengenezea sehemu nzuri ambapo miezi kadhaa baadaye, konokono wawili waliosalia walizaliana na sasa ana miliki konokono wengi.

Anasema soko la konokono ni lipo katika hoteli na migahawa mikubwa ambayo huwatumia kama kitoweo.

Kutokana na ufugaji huo, anawashauri wanawake kujikita katika biashara hiyo ambayo bado haijapata ushindani mkubwa huku soko lake likiwa la kutosha.

Anavyowafuga

Konokono wake huwafuga katika shamba na hula majani ya spinachi, sukuma wiki na chainizi.

Anasema kilimo hicho hakihitaji fedha nyingi na muda mwingi, kwani kwa mwaka hupata konokono zaidi ya 12,000.

Wataalamu wa lishe wanasemaje?

Mtaalamu wa lishe Dk Elizabeth Kuria anasema konokono ana virutubisho vingi kama madini ya chuma na protini.

Dk Kuria anayeishi nchini Kenya anasema endapo utafiti utafanywa na kuonyesha kuwa konokono hao wana faida nyingi kwa afya ya bindamu, huenda idadi ya walaji wa kitoweo hicho ikaongozeka.

Ni konokono hatari

Ni kweli unaweza kufuga konokona hawa na ukajipatia kipato kizuri kama ilivyo kwa mtoto wa Odinga, lakini wataalamu wa sayansi wanasema aina hii ya konokono sio rafiki kwa mazingira.

Wanatajwa kuwa ni konokono waharibifu zaidi duniani, kwani wanakula zaidi ya aina 500 ya mimea na wanaweza kusababisha madhara makubwa katika majengo.

Ufugaji wa konokono Tanzania

Wakati mahitaji ya konokono yakiwa makubwa kwa nchi zilizoendelea, hapa nchini ufugaji wake ni mdogo. Pengine ni kutokana na biashara hiyo kuwa mpya kwa wengi.

Hata hivyo, kama watu watachangamkia fursa hii, huenda ikawa ni biashara inayolipa na kuwaingizia watu kipato kizuri.

William Urio aliwahi kufuga konokono lakini alishindwa kuendelea na kilimo cha hicho kutokana na changamoto kadhaa.

“ Mimi nilijifunza kilimo cha konokono kwa watu wa Nigeria, lakini nilipata changamoto katika ufugaji kwani wanunuzi walikuwa wanataka kononoko wenye rangi, tofauti na wale wa kawaida” anasema.

Anasema kuna konokono maalum wenye mistari minne mgongoni na rangi ya kahawia ambao ndio waliokuwa wakitakiwa.

“ Changamoto nyingine ni namna ya kuwafuga, wanatakiwa uwaandalie majani ya kutosha tofauti na konokono wengine ambao hawawekwi katika boksi zaidi ya kuwaweka katika shamba tu” anasema Urio.

Wakati Urio akifafanua hivyo, mfugaji mwingine kutoka Zanzibar, Abdallah Said yeye anasema mwaka 2017 alianza kufuga konokono lakini alishindwa kuendelea na kilimo hicho kutokana na kusafiri mara kwa mara, nje ya Zanzibar.

Anasema lengo la kuzalisha konokono hao ni kwa ajili ya kulisha funza na samaki ambao pia alikuwa anafuga.

“ Ili uwe na funza mwenye afya nzuri na samaki wenye afya nzuri, unatakiwa uwape protini ya kutosha, hivyo konokono wana protini nzuri kwa ajili ya samaki na funza” anafafanu.

Kwa upande wake, anasema hakuendelea na ufugaji huo kwa sababu hakuwa na uangalizi wa kutosha.