Hata uwe hodari vipi lazima yupo aliyekuzidi

Muktasari:

  • Chuki, wivu na roho za kwa nini huanzia hapa. Kwanini kanizidi hiki, mbona anafanikiwa wakati mimi mzuri zaidi yake? Na maswali mengine yanayofanana na hayo.

Wanasema maisha ni vita, kupambana na kuishinda jana. Lakini kiuhalisia maisha ni unayopigana mwenyewe.

Hata uwe hodari vipi, kumbuka kuna mahali duniani yupo hodari zaidi yako. Hata uwe mrembo au mtanashati kwa namna gani, kumbuka yupo wa zaidi yako.

Ni kawaida yetu kujilinganisha au kujishindanisha na watu. Mara zote tunaangalia nje, pembeni kuona washindani wetu wanafanya nini. Hii inatufanya tuanze kuona mapungufu.

Chuki, wivu na roho za kwa nini huanzia hapa. Kwanini kanizidi hiki, mbona anafanikiwa wakati mimi mzuri zaidi yake? Na maswali mengine yanayofanana na hayo.

Muhimu ni kutambua kuwa kila mmoja ana karama yake. Kwamba lazima mahali fulani kuna mtu anakuzidi na iwapo hutalitambua mapema hutapata amani katika uyafanyayo.

Kuna Steve Jobs, Mo Dewji, Dangote, Diamond Platnumz, Alikiba au Khadija Kopa. Kila mmoja ana umahiri wake. Kila mmoja ana ubobezi wa jambo fulani na hakuna anayeweza kumshinda.

Kuendelea kutaka kujishindanisha na watu fulani ni kujinyima haki ya kufurahia maisha. Huwezi kuwashinda. Furahia ubora wako. Sherekea ushindi wako na shukuru kwa baraka ulizojaliwa.

Muhimu ni kushindana na uliyekuwa jana. Kwa maana kila hatua lazima ikufanye bora kuliko ulivyokuwa siku moja kabla. Mafanikio ni wewe kupiga hatua kila siku na leo yako iwe bora kuliko jana.

Katika ushindani wa kazi au biashara, hakuna kitakachobadilika kama wewe hutataka kuwa bora. Kujibidiisha kwa kufanya kazi kwa kiwango cha juu zaidi kuliko ulivyofanya siku za nyuma.

Je, mbinu zako ni zilezile, elimu je? Unakwenda na wakati au umebaki kuishi mwaka 2008. Kama una mgahawa na umeendelea kuuza sahani 20 kwa miaka mitatu hilo ni tatizo lako.