Hatua 10 za kukuwezesha kupandishwa cheo

Sunday April 14 2019

 

By Dk Chris Mauki

Watu wengi hutamani sana kupandishwa vyeo baada ya kuchoka sana na nafasi walizokuwa nazo kwa muda mrefu, au pia wengine wanatamani sana kupandishwa vyeo kwa sababu ya kuongeza kipato ili kufikia malengo fulani maishani, kilammoja ana sababu binafsi ya kuhitaji kupandishwa cheo. Taarifa za kupandishwa cheo ni za kufurahisha kwa kila mmoja wetu, wako ambao huilazimisha fursa hii hata kwa kwenda kwa waganga, kuhonga, kujipendekeza, kujitoa miili yao na njia nyingine nyingi ili tu kupata cheo. Mara nyingi tumejiuliza kwanini sipandi cheo, wengine wapya wanakuja hapa wanafanya kazi kidogo mara wanapandishwa cheo, wanabadilishiwa ofisi, wanapata gari la ofisi, nyumba, na marupurupu mengine lakini si mimi, ukweli ni kwamba sababu kubwa ni sisi wenyewe, vitu vinavyotuangusha na kutufelisha si vile vilivyo nje yetu bali vile vilivyo ndani yetu, vilivyo ndani ya uwezo wetu. Leo unaweza kuamua kufanya jitihada binafsi za kujua namna ya kuweza kupandishwa cheo. Pengine wewe ni mmoja wa hawa ninaowazungumzia hapa ili uweze kujikwamua.

Jaribu kufuata kanuni hizi rahisi:

Jitahidi kujuana na watu

Unaweza kufikiri kuwa njia pekee ya kubadilisha mazingira uliyonayo ni kukaa na kuwaza sana, hapana, hii si kweli, jaribu kujipenyeza kufahamiana na wengine, usijitenge sana, shiriki maisha yako na wale walioko karibu nawe.

Usifikiri kuwa hustahili kujichanganya katika mazungumzo ya kawaida na watu wa ofisini kwako, usifikiri kuongea na bosi wako masuala ya kawaida ni kujipendekeza, kumbuka kwa kuwajua na kujichanganya na wafanyakazi wenzako tunajenga nguvu ya umoja wa kazi, taratibu wote tunakuwa ni timu moja katika utendaji.

Pia usibaki umefungiwa katika kiti chako au meza yako ya kazi hata zile nyakati ambazo wengine wanapumzika au kujiburudisha, kama kuna hafla ya ofisi na wenzako wanaenda basi shiriki nao, usifikiri wanapoteza muda, kama mwenzako ana tukio fulani la furaha nyumbani basi usiache kushiriki, na kama wewe una tukio kama hilo kwako basi wakaribishe wenzako na usisahau kumualika hata na bosi wako pia. Taratibu unapoanza kumfahamu zaidi bosi wako ni mwelekeo mzuri kuelekea mafanikio yako.

Usijifanye mkamilifu katika kilakitu.

Usije ukafikiri kuwa haukuumbiwa kufanya makosa, kufanya kosa kupo katika maisha ya mwanadamu. Kama wewe ni mtu unayefanya kazi sana si kitu cha kushangaza sana ukikosea. Ikiwa unatokea kufanya kosa, usikae ukijilaumu na kujiuliza kwa nini umefanya kosa bali jifunze, pata somo katika kukosea na uendelee mbele. Kama utaweka akili yako yote katika kujichunguza kila unachokifanya ili usikosee basi hata bosi wako anaweza kufikiri kuwa wewe ni kati ya wanaojifanya wakamilifu kwa kila wafanyalo na kinyume chake cheo kikaenda kwa wenzako. Usisahau kuwa waweza kujikuta unafanya vimakosa vingi zaidi wakati unajitahidi kujiweka mkamilifu katika jambo.

Kuwa mwaminifu

Uaminifu ni kitu kizuri na cha maana na kinachowashinda wengi wetu. Wakati wowote unapopata nafasi ya kuongea na bosi wako, kuwa mkweli kwa kila neno litokalo kinywani mwako, liwe dogo au kubwa, liwe kuhusu wewe mwenyewe au kuhusu mtu mwingine.

Advertisement