Hivi ndivyo Kondomu inavyopaswa kutumika kwa usahihi

Matumizi ya mpira wa kiume ni miongoni mwa njia za kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi, kaswende, kisonono, virusi vya homa ya ini na papiloma.

Vilevile hutumiwa kama njia ya uzazi wa mpango na tiba ya kuwahi kufika mshindo yaani premature ejaculation kwa wanaume.

Mpira wa kiume hutumiwa zaidi kuliko ya kike huku kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya Ukimwi. Mipira hii inayojulikana zaidi kwa jina la kondom, hutumiwa na walioshindwa kujizuia kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu.

Pamoja na msisitizo wa baadhi ya watu kutumia mipira hii kila wanapokutana na wenza wasiowaamini, tatizo kuitumia kama inavyopendekezwa na wataalamu wa afya.

Tahadhali za kondomu

Ikitumika vizuri, kondomu ina uwezo wa kuzuia maambukizi kwa kati ya asilimia 90 hadi 95. Kati ya vitu muhimu ambavyo kilamtumiaji anapaswa kufahami ni mahali inaponunuliwa au kupatikana kwa ubora na ufanisi unaohitajika wakati wote.

Mipira hii inapatikana katika maduka ya dawa hata ya kawaida, vituo vya afya au maeneo ya umma kama vile ofisini. Unapolinda afya yako, huna haja ya kuona aibu. Nenda kanunue au kuichukua bure mahali lilipo boksi lake.

Unapoipata kondomu unayotarajia kuitumia, angalia tarehe ya mwisho wa matumizi na ukague kama ipo salama. Tazama kama haina mipasuko na kasha lake limefungwa vizuri.

Kumbuka mipira iliyopita muda wake huchanika kirahisi hivyo kukuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi au kumpa mwanamke mimba.

Suala la tatu unalotakiwa kulizingatia ni kuihifadhi mahala pasipo na joto kali. Wapo baadhi ya watu hununua mipira hii na kuiweka kwenye vyombo vyao vya usafari sehemu ambako kuna joto kali. Ni suala lisilopendekezwa.

Wapo wanaohatarisha ubora wake kwa kuiweka katika pochi na kuikalia kwa muda mrefu pasipo kuitumia hivyo kugandamizwa na kupata joto kali.

Kutumia kondomu

Kuna watu hupoteza umakini wa kutumia kondomu unapofika wakati wa kujaaminiana. Licha ya kuwa na maandalizi mazuri kabla ya kukutana na mwenza au kuingia katika uwanja wa fundi seremala.

Wakati wote unapaswa kuwa makini hasa unapofika hatua ya kuitumia. Hakikisha kiu ya kujamiana haifubazi malengo ya kuitumia kwa usahihi.

Ongea na mweza wako kuwa mnaitumia kulinda afya zenu, hivyo ni vyema kushirikiana kuitumia kwa usahihi.

Unapoitoa kwenye boksi lake na kusoma maelekezo yaliyoandikwa, unatakiwa kuifungua kwa ncha za vidole vyako na usithubutu kutumia meno kwa kuwa unaweza kuipasua hivyo kutofaa kwa malengo yaliyokusudiwa.

Ivishe uumeni ukiwa umesimama. Kwanza finya chuchu ya mpira kwa ubapa wa dole gumba na kidole cha shahada ili kuacha nafasi ya hewa na kuzuia isipasuke wakati tendo likiendelea.

Katika hatua hii mwenza anaweza kukusaidia kufinya chuchu ya mpira ila mhakikishe kucha zenu hazina ncha.

Hakikisha mviringo wa mpira unatazama nje kisha viringisha kuelekea shina la uume, ukikosea ukaweka nje ndani tupa na tumia nyingine mpya.

Kila kondomu inatakiwa kutumika kwa tendo moja, usizidishe. Usipoibadili na ukaunganisha mshindo wa pili huweza kuvuka na kupotelea ukeni hivyo kuhitaji kutolewa kitabibu.

Haushauriwi kuvaa kondomu mbili kwa wakati mmoja wala kuongeza kilainishia cha ziada mfano mafuta. Itumie kwa njia iliyokusudiwa.

Kumbuka, kondomu zina kiwango cha kushindwa kufanikisha lengo kwa kati ya asilimia 10 hadi 15 hivyo unahitaji utulivu unapoitumia, wewe na mwenza wako.

Jitafutia elimu ya afya kila mara kupata taarifa mpya za mipira hii na elimu ya afya kwani muda, vitu na watu vinabadilika.

Ukimaliza kuitumia, jitahidi uwe rafiki wa mazingira kwa kuitupa mahala salama kwa kuifunga fundo moja na kuiweka ndani ya tishu, karatasi au kipande cha gazeti kisha uitupe katika pipa la taka.

Historia ya kondomu

Historia ya mipira hii ilianzia miaka mingi kabla ya Kristo zikiwa zimetengenezwa kwa malighafi za mimea, utumbo wa wanyama na ngozi lakini baadaye, kati ya karne ya 19 na 21 zikaanza kutengenezawa kwa mpira.

Dk Condom ndiye anayefahamika zaidi kiasi cha jina hili kubaki kama msamiati, alikuwa daktari wa Mfalme Charles ll wa Uingereza.

Dk Condom aliwahi kumshauri mfalme huyo kutumia utumbo wa kondoo kujikinga na magonjwa ya zinaa, hii ilitokana na tabia ya mfalme huyo kuwa na uhusiano na wanawake tofauti.

Mwaka 1839 mwanasayansi aliyejulikana kwa jina la Charles Goodyear ndiye mbunifu wa kwanza wa kondom iliyotengenezwa kwa malighafi ya mpira na mwaka 1855 kondomu ya kwanza ya kisasa ilitengenezwa kisha kampuni mbalimbali zikaingia kwenye biashara hiyo.

Yapo mapango ya kale nchini Ufaransa yanayoonyesha kuwapo kwa matumizi ya mipira hii kabla ya Kristo. Matumizi yake yalichangiwa na kulipuka kwa ugonjwa wa kaswende kwa askari wa Ufaransa.

Kabla ya Kristo, Wamisri, Wagiriki na Waroma walizitumia kuvisha katika kichwa cha uume kwa ajili ya kupanga uzazi kwa kuwa walipenda kuwa na watoto wachache.

Watu hawa walitumia kondomu zilizotengenezwa na utumbo wa wanyama au samaki, ngozi na mimea.

Ilipofika mwaka 1929 ndipo kampuni ya Young Rubber ilikuwa ya kwanza kutengeneza kondomu ya kisasa zaidi yenye mpira laini wenye kiwango madhubuti kinachovutika. Aina ya kondom hiyo zilijulikana kama Latex.

Baadaye kampuni nyingine ya London, iliingia katika utengenezaji wa bidhaa hiyo mwaka 1932 ikiunda kondom ya kwanza yenye ubora zaidi ijulikanayo kama latex, durex.

Mipira hii ilisambazwa na kutumika barani Ulaya katika vita vikuu vya kwanza vya dunia baada ya wanajeshi 400,000 wa Marekani kugundulika kuugua kaswende na kisonono.

Kugundulika kwa ugonjwa wa Ukimwi mwanzoni mwa miaka ya 1980 na kuhusishwa kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi kwa njia ya kujamiana ndipo kampeni za matumizi yake zilipohamasishwa duaniani kote.