Hivi ndivyo diamond alivyofungua na kuufunga mwaka 2018

Saturday December 29 2018

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Diamond ni kati ya wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa ndani na nje ya nchi.

Tangu alipoachia kibao chake cha ‘Nenda Kamwambie’ mwaka 2013 na baadaye ‘Mbagala’ aliachia vibao vingine mfululizo na kuwa kipenzi cha mashabiki wengi.

Mbali ya kuwa na nyimbo nyingi na zinazopendwa pia ndio msanii anayemiliki wasanii wanaofanya poa kwenye muziki wa Bongo fleva, akiwemo Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Queen Darleen na Lavalava.

Hata hivyo yapo matukio mbalimbali aliyoyafanya katika mwaka huu, ambayo mengi yamemfanya awe midomoni mwa watu kila uchwao.

Pia huenda ndio akawa msanii aliyekuwa na matukio mengi yaliyokuwa gumzo kuliko mwingine huku kubwa likiwa kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kujihusisha na muziki kwa muda usiojulikana.

Aachana na Zari

Mwanzo wa mwaka 2018 haukuwa mzuri kwa Diamond, ikiwa ni miezi miwili tangu uanze alikutana na misukosuko ya kimapenzi baada ya kutemwa na mzazi mwenzake Zari au Mama Tiffah.

Tukio hilo lilitokea Februari 14, ambayo wengi huazimisha siku ya wapendanao kwake ilikuwa tofauti .

Zari aliyezaa na Diamond watoto wawili, Nillan na Tiffah, alitangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Instgram, maneno yaliyosindikizwa na picha ya ua ridi jeusi na kueleza sababu kuwa imetokana na Diamond kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine. Pamoja na uamuzi huo, Zari ambaye ni mama watoto watano alisema anaachana na msanii huyo kama wapenzi lakini wataendelea kuwa wazazi wenza.

Songombingo na Hamisa

Oktoba mwaka 2017, Hamisa Mobeto alifungua kesi katika mahakama ya watoto ya kudai matunzo ya mtoto.

Hata hivyo ilipofika Februari mwaka huu mahakama hiyo iliifuta kesi hiyo baada ya wawili hao kupatana nje ya mahakama.

Timbwili na Waziri Shonza

Wakati mambo ya kumaliza kesi ya matunzo ya mtoto yakiwa hayajapoa vizuri, Machi 20 Diamond tena alijikuta akiwa ameingia katika misukosuko na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Juliana Shonza.

Hii ilitokea baada ya nyimbo zake tatu kuwa mojawapo ya nyimbo 15 zilizofungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kutokana na kwenda kinyume na maadili na kanuni za Huduma za Utangazaji(Maudhui)2005.

Akiwa anahojiwa katika kituo cha redio Times kuhusu maamuzi hayo ya TCRA, Diamond alionekana kumshambulia zaidi Shonza huku akieleza kuwa anakurupuka katika maamuzi yake.

“Hivi leo unanifungia nyimbo yangu niliyoitengeneza kwa mamilioni ya pesa unadhani nitazirudishaje, au unadhani watoto wangu Nillan, Dyllan na Tiffah watanunuliwa na nini ‘pampas’? Ifike mahali viongozi wetu wavae viatu vyetu na si kuona raha tu kutufungia wakati tumetaabika katika kuyajenga majina yetu hadi sasa tunajulikana duniani,” alisikika akisema Diamond.

Hata hivyo Shonza alikataa kujibu tuhuma za msanii huyo dhidi yake kwa madai kuwa hakufuata taratibu za kudai haki. Malumbano hayo yalimalizwa na Waziri Dk Harrison Mwakyembe baada ya kuingilia kati na kumaliza tofauti zao.

Akutana uso kwa uso na Ali Kiba

Aprili 22, Diamond aliandika historia baada ya kukutana uso kwa uso na hasimu wake mkubwa katika kazi ya muziki, Ali Kiba.

Wawili hawa walikutana katika viwanja vya Leaders wakati wa shughuli ya kuuga mwili wa marehemu Agnes Masogange, aliyekuwa video queen maarufu nchini.

Tukio hilo, liliwafanya watu waliokuwepo katika shughuli hiyo kubadilika kutoka katika nyuso za huzuni na kuwa za shangwe na kushindwa kujizuia kushangilia hasa pale waliposhikana mikono kama ishara ya kusalimiana.

Amwaga misaada Tandale

Katika kujiweka karibu na jamii, Oktoba 6, aliwakonga nyoyo mamia ya wakazi wa Tandale eneo alilozaliwa kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo kuwakatia bima za afya na mikopo kwa kina mama.

Shughuli hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Magunia, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza. Mbali na kuwakatia bima watu zaidi ya 200, pia aligawa bodaboda 20 kwa vijana, ambazo lengo ilikuwa zizalishe nyingine zitakazoongeza ajira kwa vijana hususani wa eneo hilo.

Aja na Tamasha la Wasafi

Kwa mara ya kwanza msanii huyo ambaye ndiye mmiliki wa lebo ya Wasafi alitambulisha tamasha jipya alilolipa jina la ‘Wasafi Festival’.

Kabla ya Basata kutangaza kulifungia Desemba 18, lilikuwa tayari limeshazunguka Mtwara, Iringa, Morogoro, Sumbawanga, Zanzibar na Mwanza na kote lilikopita liliacha historia ikiwemo kusimamisha shughuli kwa wakazi wa eneo husika na kumiminika kuwalaki wanapopita mitaani na kwenye viwanja walivyofanyia shoo.

Katika tamasha hilo mbali na kutoa misaada mbalimbali kwa wakazi wa mikoa waliopita, pia alijitolea Sh68 milioni kujenga shule mjini Sumbawanga iliyopewa jina lake ‘Diamond’.

Aanguka jukwaani Sumbawanga

Desemba 9, Diamond alizua gumzo jingine baada ya kuanguka jukwaani wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa. Tukio hilo la kuanguka lilitokea katika Uwanja wa Nelson Mandela, ikiwa ni mwendelezo wa Tamasha la Wasafi au Wasafi Festival kama lilivyozoeleka.

Akiwa amepanda jukwaani na kuimba wimbo wa ‘Zilipendwa’ na wasanii Rayvanny na Mbosso, ubao uliowekwa chini ulisogea na kujikuta anaanguka kwa kutumbukia chini ya jukwaa, jambo lililozua gumzo mitandaoni.

Gumzo la tukio hilo lilipozwa na Diamond mwenyewe baada ya kuandika kupitia ukurasa wake wa Instagram ‘Sumbawanga nimewashindwa’.

Atambulisha mpenzi mpya

Baada ya kuachwa na Zari, Diamond alikaa kimya, hakuna aliyejua anatoka na nani hadi alipovunja ukimya kwa kumtambulisha Tanasha Donna, mwanamitindo wa Kenya, alitambulishwa na Diamond wakati wa uzinduzi wa tamasha la Wasafi mkoani Mtwara na tangu hapo wameonekana wakijiachia maeneo mbalimbali ya starehe.

Diamond tayari katangaza ndoa na Tanasha ambaye pia ni mtangazaji wa Radio moja ya Mombasa, Kenya yapo madai huenda wakafunga ndoa Februari, 2019.

Vurumai na ATCL

Kama nilivyosema awali huku juu kwamba msanii huyu haishiwi matukio, Desemba 17 alijikuta akiingia katika msuguano na Shirika la Ndege Tanzania(ATCL).

Msuguano huo ulitokana na kukosa tiketi ya kusafiria kutoka Mwanza kwenda Dar, huku akidai ilikuwepo ikauzwa.

Hata hivyo ATCL waliibuka na kueleza kuwa Diamond ndiye alichelewa na kumruhusu kusafiri na ndege nyingine ya jioni.

Advertisement