Huenda watoto hawa wasisome

Magdallena Julius (14) na Hellena Julius(12), ni watoto waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza sekondari ya Serengeti wilayani Serengeti Mkoa wa Mara mwaka huu,hata hivyo hawajaanza masomo kutokana na ukata wa mzazi.

Wanaishi eneo la kijiji cha Burunga kata ya Uwanja wa ndege wilaya ya Serengeti, wana ndoto ya kuwa walimu, hata hivyo kama hakutatokea msamaria kuwasaidia, ndoto zao zitayeyuka.

Ukifika kwao wanajawa na matumaini wakiamini kuwa mgeni atakuwa mkombozi wao kwa kuwa baba yao ameishakata tamaa, kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili kiasi cha kushindwa kuwanunulia vifaa vya shule na michango mingine ya shule.

Magda kama walivyozoea kumwita akionyesha kukata tamaa anasema: ”Hali ya kiuchumi hapa nyumbani ni ngumu maana hata chakula chetu ni cha shida. Kwa hali ya baba si rahisi kumudu gharama za vifaa vyetu ikiwamo viti na meza,”anasema.

Anataja mahitaji yaliyowakwamisha yeye na mdogo wake kuwa ni sare, viatu, madaftari, begi mchango wa viti,meza na uji shuleni ambayo yanafika Sh 500,000 kwa wote wawili.

“Ugumu wa maisha yetu haukuanza leo, tumezaliwa tumekuta wazazi wetu wanaishi kwa shida hadi mama akaamua kukimbia. Baba yangu ni miongoni mwa watu waliohamishwa Nyamuma na mkuu wa wilaya,wakachomewa nyumba na kuporwa mali zao,”anasema huku akifuta machozi.

Baba alia hali ngumu

Nyangige Mataro(41) ambaye ni baba wa watoto hao, kwa utulivu anasema hana uwezo wa kupata vifaa vya watoto ili waweze kujiunga na kidato cha kwanza.

“Dada zao wawili wako vyuoni wanasoma,nimeuza maeneo hadi ya kilimo ili waweze kusoma mpaka yameisha,nao ilikuwa wasiendelee bali nasaidiwa ,sina namna kabisa ingawa naumia kuwaona wanangu nyumbani wakati wenzao wako shuleni,”anasema.

Anaomba msaada kwa watu mbalimbali ili kuwanusuru hao watoto akisema: ‘’Haya yote yanajitokeza sababu ya ugumu wa maisha, lakini nawapenda watoto wangu hasa wa kike.’’

Mataro mwenye watoto 12 anasema mke wake mkubwa alimkimbia kutokana na ugumu wa maisha.