Huku ndipo zilipofichwa ‘dhambi’ za wanawake kwenye simu zao

Sunday June 10 2018

 

Ukiondoa muziki, tamthilia, filamu na usengenyaji, starehe nyingine wanayoipenda wanawake ni kukagua simu zetu. Mwanamke akikamata simu yako ikiwa na chaji asilimia 100, anaweza akairudisha ikiwa na asilimia 15 na alichokuwa akifanya muda wote ikiwa ni kukagua tu.

Wana utaalamu katika sekta hiyo, wengine wana ujuzi huko kuzidi hata wanavyojua kucheza na sufuria jikoni, ni kama kipaji cha kuzaliwa.

Kuna wanaume pia wanajitahidi sana kujikita katika nyanja hii. Si dhambi, lakini asilimia kubwa hawajui kufanya ukaguzi.

Wengi wakishika simu wanaingia moja kwa moja kwenye sehemu ya ujumbe mfupi, ama kama ni simu janja wanakimbilia kwenye programu za meseji kama Whatsapp, Facebook, Instagram na zaidi.

Ni kweli, huko ndipo dhambi zinapofichwa kwenye simu za wanawake lakini ubaya ni kwamba wengi wanakosea, wanasoma mazungumzo ya wanawake zao na wanaume.

Yaani akikuta meseji imetoka kwa mwanamume au mke ameituma kwa mwanamume yeye ndiyo anacheza nayo hiyo, anatembea nayo taratibu, neno kwa neno, kuhakikisha kuna nini ndani.

Huko ni kujichosha, huwezi kukuta chochote kwenye majina ya wanaume na kama utakuta itakuwa ni bahati yako ila uwezekano ni mdogo sana.

Wanawake ni wajanja, wanawake wana kumbukumbu, hata siku moja si rahisi kusahau kutokufuta meseji ambazo zinatoka kwa wanaume na wanajua kwamba zinaweza kusababisha mizengwe ikiwa wewe utaziona, kwa hali hiyo usitegemee kuziona.

Sasa wapi kuna ‘madini’? Ukitaka kuyaona madini katika simu ya mama watoto wako, hakikisha unapita sehemu ambazo mazungumzo ni ya wanawake wenzake, hapo ndipo kwenyewe.

Ukiona meseji imetoka kwa Jackline, Halima, we zama nazo. Pitia humo. Ambazo zinaandikwa kwenye magrupu ya wanawake ndiyo kanisa. Ingia magroup yote, soma kila kitu, neno kwa neno, nukta kwa mkato.

Ujinga wote wa mkeo unapatikana katikati ya stori za mkeo na shoga zake. Huko ndiko wanakozungumza kuhusu michepuko, kuhusu majanga, kuhusu nyendo zao zote ambazo wewe hazikufurahishi.

Tena wataalamu wa hizi kazi wanakwambia kwamba hata ukitaka kujua kila kitu kuhusu mkeo we cheza tu na mashoga zake. Yaani unaweza kuchukua simu ya mkeo, ukawatumia meseji mashoga zake wanne, kwa mfano waandike tu ‘Shosti nna mimba.’

Kitakachofuatia baada ya meseji hiyo ni majibu ya kukuhakikishia kwamba mke wako anachepuka au laa.

Kuna watakaosema hongera, ukikuta ana hizi jua mke wako yu salama. Lakini kuna wengine wanakumbana na majibu ya ya kushtua kama vile, mimba ya nani? Ya Juma, ya Patrick au ya jamaa la Bandari?

Advertisement