Huu ndio mkataba wa miaka kumi Barnaba na Vanessa Mdee

Saturday January 19 2019

 

By Nasra Abdallah,Mwananchi [email protected]

Huenda ukawa unajiuliza maswali mengi kwa nini Vanessa na Barnaba wamekuwa wakitoa nyimbo za pamoja.

Tayari sasa wasanii hao wanaofanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva wameshaachia nyimbo mbili kwa kushirikiana.

Walianza na wimbo ‘Siri’ waliouachia mwaka 2015 na mwaka jana waliachia wimbo ‘Chausiku’ ambavyo vyote vimeweza kufanya vizuri.

Katika mahojiano yake na Mwananchi Barnaba anatoboa siri ya kufanya kazi na Vanessa akisema mbali ya kuwa mtu wake wa karibu pia wameingia mkataba wa miaka kumi wa kufanya naye kazi.

Akifafanua kuhusu mkataba huo, Barnaba ambaye jina lake halisi ni Elias Barnaba, anasema moja ya makubaliano ni kutoa wimbo mmoja kila mwaka.

“Kwa mwaka huu mashabiki wetu watarajie kupata ngoma nyingine kutoka kwetu na kama kawaida yetu huwa hatubahatishi hivyo wasubirie kitu kizuri,” anasema.

Kuhusu mgawanyo wa gharama za kuandaa kazi, anasema mmoja atahusika katika uandaaji audio na mwingine video.

Vilevile kwenye kuweka wimbo Youtube ambapo kisheria hamuwezi kuuweka wote, anasema hili hupokezana, na kutolea mfano kwa wimbo wa Siri kuwa uliwekwa katika akaunti ya Vanessa na wa Chausiku aliuweka kwake.

Anasema kila senti inayopatikana katika kila wimbo wanaoutoa hugawanywa nusu kwa nusu na kuongeza kuwa wanafanya kazi kama familia moja hivyo hakuna litakaloshindikana kwenye mkataba huo.

Akimuongelea Vanessa, anasema ni mtu ambaye wanaendana katika kufanya biashara, pia ni msanii wa kike ambaye ameweza kutangaza muziki kimataifa kwa kuwa ameonyesha uthubutu.

Kuhusu mwaka 2018, Barnaba anasema pamoja na kukukumbana na changamoto mbalimbali anasema anashukuru kwa mwaka jana mambo yalikuwa mazuri kwake ikiwemo kufanikiwa kutoa nyimbo mbili.

Wakati kwa mwaka huu anasema anatarajia mambo yatakuwa mazuri zaidi kwake ukizingatia hivi karibuni anatarajia kuachia wimbo wake mpya alioupa jina la ‘Washa’.

Pia ndio kipindi anatarajia kutambulisha lebo yake ya muziki aliyoipa jina la ‘High Table’ na wasanii wake wanne huku akieleza moja ya kigezo alichotumia kuwapata ni pamoja na kuwa na nidhamu kama ambavyo yeye amekuwa.

Wito wake kwa mashabiki, anawaomba waendelee kumsapoti katika kununua kazi zake.

Advertisement