Huyu haapa mtanzania anayemiliki akademi ya soka Ujerumani

Monday October 1 2018Jamal Barass

Jamal Barass 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Kuna juhudi za makusudi kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka ambazo wamekuwa wakizifanya kuhakikisha Tanzania inakuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya licha ya ugumu uliopo.

Ugumu uliopo kwa wachezaji wengi wa Tanzania kupata nafasi ya kucheza soka Ulaya ni kutokuwa kwenye nafasi za juu za viwango vya soka duniani ambavyo hutolewa na Shirikisho la Kimataifa la Soka, Fifa.

Mawakala wengi wa soka duniani wanaamini kuwa taifa linalofanya vizuri kama ilivyo kwa mataifa ya Afrika Magharibi, Nigeria,Ghana, Ivory Coast, Cameroon na Misri ndipo ambako wanakoweza kupata vipaji vya soka na kuvisimamia.

Pamoja na uwepo wa mazingira hayo ambayo amekutana nayo, Jamal Barass alipokuwa akijaribu kutafuta nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi hakukata tama na mwishowe alichukua uamuzi wa kusaidia vijana wengine wa Tanzania ili watimize ndoto zao.

Kufeli kwake haikuwa sababu ya kumfanya aachane na soka aliamua kujikita zaidi ili kuondoa changanmoto ambayo Watanzania wengine ingewakwamisha.

Spoti Mikiki ilimnasa Barass na kumweka kwenye kundi la miongoni mwa wadau wa soka la Tanzania ambao wanapenda kuona maendeleo yakipatikana licha ya uwepo wa changamoto kadhaa za soka letu.

MAMBO YALIVYOKUWA

Barass ambaye anatarajia kurejea nchini akitokea Ujerumani amezungumza na jarida hili kiundani namna alivyogeukia masomo ya ukocha nchini Denmark na kusimamia wachezaji ili kutimiza ndoto zao.

“Binafsi nilicheza mpira japo sikufika mbali kutokana na changamoto kadhaa ambazo zilinifanya nisifikie malengo. Muda huo sikuwa na mawazo ya kuanzisha kampuni ya kusimamia wachezaji, nilikuwa nikiwaza kucheza soka Ulaya.

“Lakini nilivyoona ndoto zangu haziwezi kutimia nikajikita kwenye biashara na baadaye nikaamua kwenda kusoma Ulaya ambako niliamini ninaweza kupata elimu yenye kiwango kikubwa inayohusu ukocha,” anasema.

Mdau huyo ambaye kampuni yake inaitwa BASMALI (Barass Sports Management Limited) anadai hakuwa anapata sapoti kwingine zaidi ya kusomea ukocha kupitia biashara ambazo alikuwa akifanya.

Barass anasema alisomea ukocha na kupata leseni ya UEFA ya Shirikisho la Soka Denmark ambalo linafahamika kama DBU, baadaye akasomea inshu za kusimamia wachezaji pamoja na ujuzi wa kutambua vipaji vya wachezaji ‘scouting’.

KUFUNGUA KAMPUNI

Wakati ameanza kusomea ukocha, Barass anasema hakuwa na wazo la kufungua kampuni ya kusimamia wachezaji lakini akiwa chuo ambako alikutana na watu tofauti akajikuta anaingiwa na hayo mawazo.

Barass anasema kabla ya hata kuanza kusomea mambo ya mpira alitambua baada ya kumaliza atawatumikia Watanzania kufanikisha ndoto zao lakini hakuwa na mawazo ya kuwa na kampuni ya kusimamia wachezaji.

“Nilikuwa na uwezo wa kuja nyumbani Tanzania na kuwa kocha mkubwa tu kutokana na vyeti nilivyonavyo, lakini nikawaza nitakuwa kocha je nitakuwa nimemaliza tatizo lililonitatiza ndoto zangu, nikajijibu kuwa ndiyo lakini siyo kwa kiwango kikubwa. “Natambua kuwa Tanzania ina makocha wengi ambao wanaweza kutambua vipaji vya wachezaji na kuviendeleza ila namna ya kuwafanya wachezaji hao kutimiza ndoto zao ni kikwazo kikubwa hakuna taasisi nyingi nchini zinazoweza kuwasimamia,” anasema.

Barass anadai ndipo akafanya uamuzi, 2016 wa kufungua kampuni yake hiyo ili kuchukua nafasi ya kama daraja la kuwavusha wachezaji wa Kitanzania kutoka nchini na kwenda Ulaya ambako wamejitengenezea mizizi ya mahusiano mazuri na klabu kadhaa.

MALENGO YA KAMPUNI

Barass ambaye ndiye mkurugenzi mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya BASMALI (Barass Sports Management Limited), anasema malengo yaliyopo ni kuongeza idadi ya wachezaji wanaocheza mpira wa kulipwa nje ya nchi.

Mkurugenzi huyo anasema vijana wengi Kitanzania wanatamani kucheza soka Ulaya na sio kwamba hawana uwezo wanao ila tatizo kubwa ni kuinganishi kwao na huko ambako wanatakak kwenda.

“Hii kampuni ya usimamizi wa wachezaji lakini pia kampuni inamiliki kituo cha Barass Sports Centre kilichopo Magu Mwanza chenye lengo la kuendeleza vijana kupitia michezo na Elimu,” anasema.

WIGO WA KAMPUNI

Barass anasema kampuni yake inawigo mpana kwenye mataifa mbalimbali kwa kuweka wawakilishi wao.

Miongoni mwa mataifa ambayo wanawawakilishi ni Tanzania, Kenya, Nigeria, Denmark na Ujerumani.

“Kampuni ina miaka miwili kwa hiyo bado ni kampuni changa lakini tunaendelea kuipanua kadri tutakavyoweza,” anasema.

KUWEKEZA TANZANIA

Barass anasema wana mpango wa kuwekeza nchini kwenye kituo chao kilichopo Mwanza, anadai kituo hicho bado hakina miundombinu kwa maana ya vifaa vya kisasa na mengineyo muhimu ambayo huwa yanahitaji kwenye vituo mbalimbali vya soka.

“Tupo kwenye mchakato wa kuandaa bajeti kwa ajili ya uwekezaji mkubwa, hizi ni mikakati juu ya mkakati naamini tutafika,” anasema Barass.

CHANGAMOTO

Upande wa vikwazo ambavyo amekutana navyo, Barass anasema ni vingi lakini miongoni mwanzo ni gharama kubwa ya kutengeneza uhusiano.

Pili anasema ni ukubwa wa gharama za kumsafirisha mchezaji na akatoa mfano kutoka Tanzania hadi Denmark ambako wana mawasiliano makubwa na klabu nyingi za nchini humo.

“Kufikia uhusiano mzuri na klabu yoyote ni gharama ila cha kushukuru Mungu haijawahi kutokea pamoja na mazingira hayo na mengineyo mengi nikawa na mawazo ya kuachana na usimamizi wa wachezaji,” anasema.

MATUNDA YA KAMPUNI

Ndani ya miaka miwili, Barass anasema kampuni yake imefanikisha madili kwa Watanzania wawili ambao ni Elisha Nehemia na Ally Athuman ambao kwa sasa wako kwenye klabu ya FC Helsingør.

FC Helsingør ni timu ya daraja la kwanza Denmark ‘NordicBet Liga’ ambayo imetoa nafasi kwa nyota hao wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 18 kuwa nao kwenye timu za vijana.

WALIPO JIKITA

Barass anasema kampuni yake imejikita kwenye kusimamia zaidi vijana wadogo wenye umri chini ya miaka 20.

“Wenzetu wanapenda zaidi soka la vijana kwa sababu huko ndipo walipotengenezwa nyota wanaofanya vizuri. Kama kusingekuwa na maandalizi mazuri kwao ni ngumu kuona ubora ambao wamekuwa wakiuonyesha.

“Sana sana tunatoa kipaumbele cha kumsimamia mchezaji mwenye miaka 16 na 17 ni wachache ambao tunawasimamia wakiwa na miaka 20,” anasema.

Barass anasema wepesi uliopo kwa kijana mdogo ni kwenye kufundishika, wanaweza kumwombea sehemu nafasi na akachukuliwa moja kwa moja kutokana na udogo wake.

MTANDAO WAO

Kuhusu ukubwa wa mtandao wao kwa maana ya mahusiano na klabu mbalimbali, Barass anasema wamefanikiwa kupata ukaribu na FC Helsingør, Hornbak IF za Denmark na kituo cha Snekkersteen IF ambako hupeleka wachezaji wao kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Upande wa Ujerumani, Barass anasema wapo kwenye mazungumzo na klabu za Bundesliga, SV Werder Bremen na 1. FSV Mainz 05 ili kufanya nao kazi kupitia kwa Harkebrügge SV.

WANAKOPATA SOMO

Mkurugenzi huyo wa ufundi wa BASMALI, anasema wamekuwa wakijifunza vitu vingi kutoka kwa makapuni mkubwa ya usimamizi wa wachezaji kama vile Player Transfer & Management, TSH Talentschmiede GmbH & Co KG, 100&10 Percent Global Sportsmanagement.

Nyingine ni 100&10 Percent Global Sportsmanagement, Spielerberaterkanzlei Agirman, 90m GmbH, Hanse Sports GmbH, LPM Sports GmbH & Co. KG, 100&10 Percent Global Sportsmanagement na YA Fussball - Sag JA zu Fußball.

UJIO WAKE BONGO

Mkurugenzi huyo wa ufundi huenda akatua nchini wakati wowote kwa ajili ya kufanikisha moja ya usimamizi mkubwa wa mchezaji wa Kitanzania.

“Nina dili kubwa hilo. Huyu mchezaji ambaye nakuja kumchukua hatoki kwenye kituo changu kule Mwanza, anamilikiwa na watu wengine hapa ni baina ya kampuni yangu kwa ajili ya kumsimamia,” anasema

Advertisement