Huyu hapa Wellu wa Steve Nyerere

Steven Mengere maarufu kwa jina la ‘Steve Nyerere’ ni kati ya wasanii wasiokauka midomoni mwa watu kutokana na namna ambavyo amekuwa akishiriki mambo mbalimbali hususani yanayohusu matatizo ya wasanii.

Kunapotokea misiba huwa mstari wa mbele kusimamia kamati mbalimbali za mazishi hadi kufika hatua ya watu kumpachika jina la mwenyekiti wa kamati ya rambirambi.

Amekuwa akishambuliwa mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii anapoandika lolote kadhalika hata anapotoa pole za misiba, huwa wakimtania kuwa ajiandae kukusanya rambirambi kitu ambacho anasema kwamba yote hayo hajali na zaidi anaona maneno hayo yanamjenga na kumuimarisha.

Wakati wengine wakimchukulia poa Steve, Wellu Sengo ambaye ni mama mtoto wake mmoja alipiga stori mbili tatu na mwandishi wa makala hii amezungumzia kwa undani kuwa Steve ni mtu wa aina gani tofauti wanavyomchukulia.

Kwa msiomjua Wellu ni msanii ambaye jina lake lilipata umaarufu kupitia tamthiliya ya Matilda na baada kuendelea kufanya filamu mbalimbali ikiwemo ‘I Know You’, ‘Bado Natafuta’, ‘Vagabond’ na sasa anaonekana kwenye tamthiliya ya Rebecca akiwa mhusika mkuu.

Akimuelezea Steve

Wellu anasema Steve ni mtu mwenye huruma, roho nzuri iliyopitiliza na hujitolea sana pasipo kujali anapata faida gani au anapoteza nini.

Pia, anasema ni mtu ambaye anapenda kusamehe, japokuwa hupenda kufanya maamuzi magumu pale anapoamua kufikia ukomo wa uvumilivu.

Akielezea namna anavyoshambuliwa kwenye mitandao, Wellu anasema hiyo ni hulka ya binadamu na huwezi kuwazuia.

Hata hivyo, anasema kama binadamu wakati mwingine huwa anaumia namna wanavyomshambulia baba watoto wake lakini anabainisha kuwa yote hiyo ni watu kujidai wanajua sana maisha ya watu wakati hawana wanalolijua.

“Wasanii huwa tunaongelewa mambo mengi sana, mwisho wa siku kikaongelewa ndivyo sivyo bila kujua namna gani inavyotuumiza kwenye mioyo yetu na hatuna sehemu nyingine ya kukanusha hivyo ndio maana wengine wanatumia mitandao hiyo hiyo kutoa ufafanuzi.

Je, huwa anamshauri?

Wellu anasema kama binadamu ambao wana uhusiano, masuala ya kushauriana mambo mbalimbali yapo.

Anaongeza kuwa hushauriana ikiwemo hilo la kwenye mitandao japokuwa sio kila anachofanya ni lazima amruhusu kwani kama binadamu ana uhuru wake.

Steve anamsaidia kwenye sanaa?

Kuhusu tetesi kuwa amejisogeza karibu kwa Steve ili kumsaidia kuendelea kudumu katika sanaa, anasema hilo halina ukweli wowote kwani ameanza mahusiano na Steve akiwa tayari ana jina.

Wellu anaeleza michongo aliyonayo Steve ni kwa faida yake wala haihusiani naye na kufafanua ameenda kwake kwa mapenzi na sio kitu kingine.

Kuhusu namna wazazi walivyompokea Steve kwa mara ya kwanza, anasema anashukuru walimpokea kwa mikono miwili japokuwa alikataa kuelezea wanaishi naye vipi kwani Steve tayari inaelezwa ana ndoa na mwanamke mwingine.