Inawezekana kubeba ujauzito na miaka 67, lakini hatari-Madaktari

Friday November 1 2019

 

By Amana Nyembo, Mwananchi [email protected]

Gumzo kubwa wiki hii katika medani ya afya lilijikita katika taarifa ya mwanamke anayeitwa Tian, mwenye umri wa miaka 67, kujifungua mtoto baada ya kupata ujauzito kwa njia ya kawaida, lakini madaktari wameonya kuwa kuna athari kubwa kubeba ujauzito katika umri mkubwa.

Tian, ambaye ni daktari mstaafu alipata mimba kwa njia ya kawaida tofauti na wanawake wengine wenye umri mkubwa, baada ya kutumia ujuzi wake katika masuala ya tiba, kujisimamia ujauzito wake akitumia dawa asili za Kichina.

Lakini alijifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Zozhuang. Mumewe anaitwa Huang akiwa na miaka 68.

“Tuna bahati kutokana na ukweli kuwa alikuwa na ujauzito katika umri mkubwa na alikuwa na matatizo mengi,” alisema Liu Wencheng, daktari aliyesimamia upasuaji wa Tian.

Kwa mujibu wa kitabu cha rekodi za matukio makubwa duniani, Tian amevunja rekodi iliyowekwa Agosti 20, 1997 na Dawn Brooke wa Uingereza ambaye alijifungua kwa mkasi akiwa na miaka 59 baada ya kupata ujauzito bila ya kutarajia.

Hata hivyo, mwanamke aliyejifungua akiwa na umri mkubwa zaidi ni Erramatti Mangayamma. Alijifungua akiwa na umri wa miaka 73 na ndiye anayeshikilia rekodi ya mwanamke mwenye umri mkubwa duniani kujifungua, lakini alipata ujauzito kwa njia ya kupandikizwa mimba (IVF), njia ambayo wanasayansi wanasema inawezekana.

Advertisement

Mangayamma alijifungua Septemba mwaka huu watoto pacha wa kike kwa njia ya upasuaji, akiwa jimbo la kusini la Andhra Pradesh nchini India.

Lakini taarifa za kujifungua kwa Tian zilisisimua zaidi na zilienea kwa kasi duniani kote na kuibua mijadala kuhusu uwezekano wa mwanamke mwenye umri zaidi ya miaka 42 kubeba ujauzito kwa njia ya kawaida na kujifungua.

Nchini Tanzania, daktari wa magonjwa yanayoathiri wanawake wa Hospitali ya Mwananyamala, Daniel Nkungu anasema mimba katika umri mkubwa inaongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu na kifafa cha mimba, hivyo mtoto anaweza kukua kwa tabu tumboni (intra uterine growth restriction) au kufariki kabla hajakomaa.

Anasema kihalisia baada ya kukoma hedhi, mwanamke hawezi kushika ujauzito kwa njia ya asili kwa kuwa tayari kwenye vifuko vyake vya mayai kunakuwa hakuna mayai yaliyo hai (functional follicles).

Dk Nkungu anasema kuisha kwa mayai katika vifuko vyake (ovaries) ndiko kunaleta kukoma hedhi(Menopause).

“Kwa kawaida mwanamke anakoma hedhi kati ya umri wa miaka 45 mpaka 55, lakini kuna kina mama au wanawake ambao wanakoma hedhi mapema zaidi hata katika umri wa miaka 30. Hii tunaita ni premature ovarian insurficiency/failure,” anasema Dk Nkungu.

Aliyekoma hedhi na mimba

Suala la Tian linaibua mjadala wa kukoma hedhi na uwezekano wa kupata mimba.

“Ili mwanamke apate mimba baada ya kukoma hedhi, (mwanamke mwenye umri mkubwa) lazima atumie njia za kitaalamu za kupandikiza mayai ambayo anayapata kwa egg donor (mtoaji yai) na pia atatumia dawa za homoni ili kuhakikisha hiyo mimba inakuwa,” anasema Dk Nkungu.

“Kwa hapa Tanzania, hii teknolojia ndiyo inaingia na bado haijaanza kutumika kwa wanawake waliokoma. Inatumika kwa wanawake wenye umri wa kuzaa lakini wana changamoto za kupata watoto kwa sababu mbalimbali ambazo si ovarian failure.”

Hata hivyo, anasema kwa hapa nchini hajaona rekodi yoyote ya mwanamke ambaye amekoma siku zake na akafanikiwa kujifungua kwa njia ya asili, lakini wapo wanaojifungua kwa asili wakiwa na umri wa miaka mpaka 46.

“Siku mbili zilizopita hapa Mwananyamala tumezalisha mama ambaye ana miaka 42, na ameutafuta ujauzito huo kwa zaidi ya miaka 22. Miracles still happen (miujiza inaendelea),” anasema.

“Mtu anayeshika mimba katika umri mkubwa au baada ya kukoma hedhi, anakuwa katika risk (hatari) ya kupata shinikizo la juu la damu na kifafa cha mimba, lakini pia anakuwa na high chance (nafasi kubwa) ya kupata mtoto mwenye mtindio wa ubongo (hii ni kwa wale tu ambao wanapata naturally).

“Pia, uwezekano wa kujifungua kawaida ni mdogo kwa sababu unyumbulikaji wa nyonga unakuwa mdogo mno, hivyo wengi huishia kwenye upasuaji. Pia, anakuwa na risk ya kupata kisukari kinachosababishwa na ujauzito.

“Kama mama atalazimisha kuzaa kawaida anaweza kupoteza mtoto wakati wa kujifungua kutokana na nyonga kutonyumbulika.”

Alitoa mfano wa wanawake wawili katika Biblia waliopata mimba kwa njia za asili wakiwa tayari wameshakoma hedhi, yaani Sara aliyekuwa mke wa Ibrahim aliyepata mimba akiwa na miaka 90 na kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Huu ni muujiza na si natural methods, Mungu anajua alikoyatoa mayai na kumwekea ili ashike mimba kwa njia ya kawaida,” alisema.

Anasema wa pili ni Elizabeth mama yake Yohana Mbatizaji, alishika mimba uzeeni.

“Kwa njia ya asili kushika mimba ukiwa na miaka 67 haiwezekani lakini kwa muujiza vitu hivi vinawezekana,” anasema.

Maelezo ya Dk Nkungu, yanalingana na ya Dk Samweli Shita aliyesema ni nadra kwa wanawake wenye umri kama huo kushika ujauzito.

“Huyo (bibi wa China) alipata ujauzito kwa njia ya asili. Inawezekana mwili wake ulikuwa na afya njema na kutengeneza mayai katika kipindi hiki,” alisema Dk Shita.

“Au inawezekana alipata mshtuko wa homoni na akajikuta anatengeneza mayai na yalipokutana an mbegu ya kiume ikapandikizwa akapata ujauzito,” anasema Dk Shita.

“Binafsi kwa hapa nchini, sijawahi kuona rekodi zozote za mwanamke kujifungua akiwa na umri huo, lakini kwa uzoefu wangu katika huduma za afya kulikuwepo wanawake wanaojifungua na umri wa miaka 42 hadi 45.”

Tovuti ya livescience.com inaeleza kuwa kwa kawaida wanawake wenye umri mkubwa wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo wakibeba ujauzito kulinganisha na wasichana.”

“Lakini utafiti unaonyesha kuwa wanawake wenye umri zaidi ya miaka 50 ambao wanapata ujauzito kwa njia ya kupandikizwa, hufanya vizuri kama wasichana ili mradi tu wamechunguzwa afya yao vizuri kabla ya kupandikizwa,” inaandika tovuti hiyo.”

Kwa wanawake wazee, hofu kubwa ni kama moyo na mishipa ya damu inaweza kustahimili kiwango cha ziada cha damu kinachotembea mwilini mwake, inaandika tovuti hiyo.

Dk David Cohen wa Chuo Kikuu cha Chicago anakaririwa katika tovuti hiyo akiiambia ABC News kuwa kutokana na mishipa ya damu ya mwanamke mzee kusinyaa, hatari ya kupata shinikizo la damu wakati wa ujauzito ni kubwa kwa sababu damu inakuwa inapita kwa wingi na kwa nguvu.

“Kwa hiyo ni muhimu kwa wanawake wenye umri mkubwa kupimwa vizuri kabla hawajajaribu kubeba ujauzito,” anasema Dk Mark Sauer akikaririwa na livescience.com.

Advertisement