Isha Mashauzi: Ikibidi ataimba nyimbo za injili

Saturday February 9 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Kila binadamu anapozaliwa na kujitambua katika maisha yake huwa na ndoto za kuwa mtu fulani katika jamii.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa msanii wa muziki wa taarabu Isha Ramadhani maarufu kwa jina la Isha Mashauzi.

Isha ambaye alitamba na wimbo wa mama ‘Nipe Radhi’ anasema kabla ya kuingia kwenye taarabu ndoto zake zilikuwa kuja kuwa daktari.

Hata hivyo ndoto hizo zilishindikana kufikiwa baada ya baba yake kupata ajali na hivyo kushindwa kuendelea kumlipia ada.

Akipiga stori na mwandishi wa makala hii, Isha ambaye pia aliwahi kufanya kazi na bendi ya Jahazi na wimbo ‘Ya Wenzenu Midomoni’ anasema kutokana na kifo cha baba yake alijikuta akiishia kidato cha kwanza.

Baada ya kuacha shule aliamua kwenda kusoma kozi ya kingereza na baadaye unesi, na kuifanya kazi hiyo kwa muda mfupi.

Hivyo akaamua kugeukia kwenye biashara ambapo ndipo hasa alipojikuta akiingiwa na hamu ya kuwa mwimbaji na kuanza kufanya kazi na Jahazi.

Baada ya kuachana na Jahazi aliamua kuanzisha bendi ya Mashauzi Classic Modern Taarab ambayo yeye ndiye mkurugenzi kwa sasa.

Akiwa na bendi hiyo ameshaachia vibao mbalimbali mbali vikiwamo ‘Mama Nipe Radhi’ iliyobeba jina la albamu yao ya kwanza ipo Asiyekujua, Si Bure una Mapungufu, Viwavijeshi na nyinginezo.

Kwa nini anapenda udaktari?

Isha anayetamba na wimbo wa ‘Sudi Sudini’, anasema kwa muda mrefu amekuwa akipenda watoto na kazi za kuhudumia watu.

Hata hivyo, anasema ndoto hizo haziwezi kutimia kwa umri aliofikia pamoja na kuwa na majukumu ya kifamilia.

“Mimi nilishindwa kutokana na kukosa mtu wa kunisomesha, lakini kwa sasa ndoto hizo kwa wanafunzi zinawezekana ukizingatia kuna elimu bure iliyoletwa na Serikali ya awamu ya tano.

Pia alishauri jamii kuwa na tabia ya kuwasaidia wale ambao wanakwama kwenye kusoma kwa kuwa mtoto ni wa kila mzazi.

Matamanio yake katika muziki

Isha anasema matamanio yake kwenye muziki ni kuona anamfurahisha kila aliye shabiki wake.

“Kama mnavyoniona kuna wakati naacha taarabu naimba Bongo Fleva, au muziki wa dansi ilimradi tu nimfikie kila aliye shabiki yangu na siku msije mkashangaa kuniona nikaimba na muziki wa injili.

“Hilo nalishuhudia katika shughuli zangu za kusherehesha ambako nyimbo hizo zinapigwa kwa dini zote kikubwa wanachojali wasikilizaji ni ujumbe unaopatikana ndani yake jambo ambalo naamini naweza kulifanya,” anasema.

Advertisement