January ataja mbinu ya kuinua michezo nchini

Matokeo yasiyokuwa ya kuridhisha iliyopata timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), yamepokewa kwa hisia tofauti na wadau wa michezo nchini.

Hata hivyo, fainali hizo zilizomalizika jana, zimewapa fursa wachezaji wa timu hiyo kujitangaza ndani na nje kwa kuwa ziliwaleta mawakala mbalimbali kutoka Afrika na Ulaya.

Kwa mfano, tayari mshambuliaji Kelvin John anatupiwa jicho na klabu mbalimbali za Ulaya zikiwemo Ajax Amsterdam, Lille na Manchester City, ambazo zimeonyesha nia ya kutaka huduma yake baada ya kuvutiwa na kiwango chake.

Mbali na soka, Tanzania inaweza kunufaika kupitia vipaji vya wanamichezo wake endapo itawekeza vyema katika michezo mingine.

Katika michezo ya Olimpiki, tangu Uhuru mwaka 1961, Tanzania imewahi kutwaa medali mbili pekee za fedha mwaka 1980.

Kwa upande wa soka Tanzania ilisubiri kwa miaka 39 kufuzu mara ya pili fainali hizo ukiachana na michezo mingine.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba anasema tatizo la Tanzania kushindwa kupata mafanikio katika michezo linatokana na kutowekeza katika sekta hiyo.

“Ili tuwe na furaha endelevu katika sekta ya michezo, lazima tuwekeze tuwe na miundombinu ambayo itatuwezesha kutenda, kuandaa na kuendeleza vipaji hatupaswi kubahatisha katika michezo,” anasema January.

Ushauri

January ambaye ni mdau mkubwa wa soka anasema hakuna njia ya mkato kupata mafanikio endapo Watanzania hawatabadili fikra na kufanya michezo kuwa eneo muhimu la biashara.

‘Nchi zilizoendelea katika michezo zimewekeza kwa kuvumbua, kutambua, kuendeleza na kutumia vipaji, tunahitaji kuwekeza kuanzia shuleni aina ya walimu, muda wa kucheza, kuwekeza vyuoni, ligi za vijana na wakubwa,” anasema waziri huyo.

Afcon

Tanzania itanatarajiwa kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Aftika (Afcon) zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu nchini Misri. Taifa Stars imepangwa Kundi C na timu za Senegal, Kenya na Algeria.

“Safari bado ndefu lazima kufanya kazi vinginevyo furaha itakuwa ya muda mfupi, kama nilivyosema hamasa ni hatua ya mwisho na hamasa si ndoto,” anasema January.

Alitoa mfano kwa wachezaji wa Serengeti Boys kupewa hamasa kubwa tofauti na umri na uzoefu wao katika mashindano makubwa kama Afcon.

“Tulipaswa kuwaambia mlipatikana kwenye mechi za chandimu nendeni mkacheze kama mlivyokuwa mkicheza chandimu, lakini kwa umri wao unawambia nchi nzima inawatazama ninyi, mmebeba Bendera ya Taifa, pambaneni mwende Ulaya hii ilikuwa ni presha kwao kulinganisha na umri wao,” anasema January.

Bolt, Jordan

January anasema aliwahi kuzungumza na wakala ambaye kazi yake ni kusimamia masilahi ya wanamichezo maarufu aliyekutana naye Marekani.

“Nilipata mawasiliano naye kazi yake ya kwanza alifanya Morogoro wakati akitoka Chuo, huyu ni tajiri anawasimamia wanamichezo maarufu kama Michael Jordan (mcheza kikapu wa Marekani), Usain Bolt (mwanariadha bingwa wa dunia wa mbio fupi raia wa Jamaica) na wengine wengi.

“Nilimuuliza nchi yetu tunahangaika na michezo nini tufanye? aliniambia January ili mfanikiwe lazima mkubali kuifanya michezo kuwa biashara vinginevyo ni kazi bure.

Anasema wakala huyo alimwambia wakiweza kuifanya michezo kuwa biashara viwanja vitajaa mashabiki, haki za matangazo ya televisheni na mambo mengi, mtafanikiwa lakini hamuwezi kutegemea kiingilio ili muendeshe michezo.

“Nikamuuliza mbona sisi watu wanapenda michezo, lakini hatufanikiwi, akaniambia tafuteni ‘individual sports’, hii ya timu ni gharama pia tafuteni watu maarufu wa mchezo ambao mmechagua angalau wawili halafu muone.

Anasema wakala huyo alimwambia aliisadia Pakistani ambao mchezo wao mkubwa ni kriketi ambao si maarufu katika nchi nyingi.

“Aliwashauri kujifunza mchezo wa fencing (mchezo wa kuchomana) unachezwa kwenye Olimpiki, akawapelekea vifaa na kuanza kufundishwa kwenye jimbo moja kama Tanzania mchezo huo uchezwe Bumbuli.

“Watoto wakaanza kucheza ule mchezo na nchi ikaupokea na Pakistani nzima wakawa wanapenda ule mchezo, ukawa kama mchezo wao na kwenye Olimpiki medali za dhahabu wanachukua.

Anasema inawezekana pia hapa nchini sio lazima iwe kwenye soka, wanaweza kuangalia mchezo mwingine hata ngumi, wakatafuta mabondia wawili wanaofanya vizuri duniani, wakahamasisha na ukapokewa kuwa mchezo ambao utakuwa nembo ya nchi kimataifa.

Miaka ya 1970 hadi 1980 Tanzania ilifanya vizuri katika ngumi na riadha ambapo waliweza kuvuna medali katika mashindano ya dunia, Olimpiki, Afrika na Jumuiya ya Madola.

Usikose muendelezo wa mahojiano haya na January katika toleo lijalo.