Jifunze kuishi na makundi manne ya wafanyakazi

Katika kazi kuna changamoto tofauti za kibinadamu. Tabia zetu, fikra zetu, haiba zetu, matarajio yetu yanatofautiana.

Unavyofikiri wewe; kwa mfano, sivyo wanachofikiri wengine. Unachoona ni cha muhimu, wengine wanaona hakina maana. Sababu tumeumbwa na kukuzwa tofauti.

Tofauti hizi tulizonazo ndizo hasa zinazotufanya tulazimike kujifunza namna ya kuishi na watu. Ukweli wa mambo ni kwamba usipojua namna ya kukaa na watu, hata kama hukubaliani nao, huwezi kufika mbali.

;Ukiamini siku zote kushirikiana na wale mnaofanana nao, wanaotazama mambo kama wewe, utashindwa kufanya mambo mengi.

Makala haya yanakusaidia kufahamu makundi makubwa ya watu kazini kwa kuzingatia uwezo wao na matarajio yao wanapokuwa kwenye eneo la kazi.

Ingawa makundi yako mengi, nimechagua haya matano kukidhi mukhtadha wa kazi.

Mjuzi

Huyu anaijua vizuri kazi yake. Uwepo wake kazini hautegemei fadhila wala upendeleo. Kazi zake na uwezo alionao vinatosha kumuumiza.

Unaweza kumchukia kwa sababu zako lakini huwezi kumpuuza. Utamhitaji tu kwa sababu anajua vizuri kile usichokijua.

Mara nyingi watu wenye ujuzi mkubwa kama hawa huwa hawana tabia ya kushindana na watu.

Ni watu wasiopenda kona kona sababu maisha yao ya kazi hayategemei njia za mkato.

Kutegemea na malezi, wana uwezekano mkubwa wa kuwa watu wenye roho safi. Hawa ni wale watu wanaoweza kukusaidia ukihitaji msaada pasipo kudai malipo.

Tabia hii, hata hivyo, inaweza kuwafanya wakawa wahanga wa watu wanaopenda sifa za haraka haraka kwa kutumia migongo ya watu. Hujikuta wakitumiwa na watu wenye malengo yaliyojificha pasipokujua. Wakati mwingine hugundua kwa kuchelewa na huumia.

Ikiwa kuna jina la mtu limepita kichwani kwako wakati unasoma maelezo haya, usikae nae mbali lakini pia utumie vibaya uhusiano wenu. Kumbuka kumtia moyo kwa kutambua kile alichokifanya.

Msanii

Huyu ni mtu wa maigizo. Hutumia muda mwingi kucheza na akili za watu kusudi ajijenge kibinafsi. Mara nyingi hujinasibu kuwa na uwezo asiokuwa nao. Huwatumia watu wenye ujuzi kama ngazi ya kufikia malengo yake.

Ni rahisi kumfahamu. Kwa mfano, katika vikao ni mtu atakayeongea basi tu aonekane hata kama anachoongea hakifahamu vyema. Shauku ya kujijengea sifa za haraka haraka humfanya apende kujionyesha kwa bosi kusudi ajenge taswira ya mtu mwenye bidii hata kama anajua hana bidii hiyo.

Shauri ya uwezo wake wa kucheza na matarajio ya watu, anaweza kuwa na tatizo la kupenda kuchonganisha watu anaowaona ni tishio kwake.

Pia, anaweza kuwa na tabia ya ulaghai mradi tu anachokitaka kitimie.

Kaa na mtu wa namna hii kwa tahadhari kubwa. Mengi anayozungumza hayaamini. Usidanganyike. Pia, tambua anashindana muda mwingi. Usimwingilie mipangilio yake ikiwa haikuathiri moja kwa moja. Ikiwa uko tayari kutumika kama ngazi fanya nae kazi.

Mlalamishi

Mtu wa kundi hili mara nyingi anakuwa amekata tamaa na kile anachokifanya. Kutokufikia matarajio yake ya kazi na yale ya maisha binafsi, humfanya awe na macho yanayoona tatizo kwa karibu kila kitu. Mazungumzo yake mengi hayana ufumbuzi zaidi ya kuonyesha ukubwa wa tatizo. Anapozungumzia matatizo anapata utoshelevu.

Huyu ni mtu anayeweza kukuaminisha kuwa kazini mnapofanya kazi hakufai lakini mwenyewe haachi kazi. Usipokuwa makini atakufanya uache kufanya kile unachojaribu kukifanya.

Ishi na mtu huyu kwa tahadhari. Kutegemea na vile ulivyo, waweza kumpa nafasi ya kutoa nyongo pasipo kuwa sehemu ya malalamiko yake. Ikiwa ni lazima kumsaidia, baada ya malalamiko yake mwuulize maswali yanayomfanya aone zaidi ya matatizo.

Mshindani

Kushindana ni ile hali ya kujilinganisha na mtu basi tu ujiridhishe kuwa wewe ni zaidi. Unapokuwa mshindani, kwa kawaida, inakuwa kama unaamini kufanikiwa kwako kunategemea kushindwa kwa wengine. Ukishakuwa mshindani, hutakuwa na mipaka. Utashindana kwa vitu vidogo kama mavazi, simu, gari unayoendesha, mpaka vitu vinavyogusa mambo ya kazi moja kwa moja.

Unapokuwa mshindani kazini, uwezekano ni mkubwa utapenda kueneza uzushi kwa lengo tu la kuwaharibia wengine. Mara nyingi utakuwa mtu wa kukuza mapungufu ya wengine na kukosoa watu kwa sababu unataka wengine waonekane wamekosea isipokuwa wewe.

Ukitaka kufanya kazi vizuri na mtu mshindani siku zote mfanye aamini anakuzidi. Ukiwa na muda mpe nafasi ajisifie. Ikiwa haiathiri kazi yako, usibishane naye hasa anapoonekana kuamini jambo kwa dhati. Ikiwa unaona ni lazima kumwonesha kosa lake, fanya hivyo kwa uangalifu kwa sababu ni mwepesi kutafsiri ushauri kama kudhalilishwa.

Mwandishi wa makala haya Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya