Jinsi Uganda, Rwanda zinavyosaka pumzi kwa jirani zao

Muktasari:

Kama hiyo haitoshi, Rwanda inadai Uganda inaendesha njama za kuihujumu kiuchumi lakini Uganda imekanusha.

Kama wanasemavyo watoto wa mjini mambo ni mengi muda ni mfupi. Hivyo ndiyo hali halisi ya mgogoro baina ya Rwanda na Uganda unaoendelea kutikisa. Rwanda inasema ina ushahidi unaothibitisha tuhuma zake dhidi ya Uganda lakini nchi hiyo imekanusha vikali.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame anadai utawala wa Rais Yoweri Museveni unaunga mkono kundi la (Rwanda National Congress (RNC).

Kagame ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anadai kundi hilo linatumiwa na Uganda kuwanyanyasa raia wa Rwanda wanaotembelea maeneo ya mipakani au wanaoishi nchini Uganda.

Kama hiyo haitoshi, Rwanda inadai Uganda inaendesha njama za kuihujumu kiuchumi lakini Uganda imekanusha.

Hata hivyo, katika mtazamo wa haraka mataifa hayo yako kwenye mfarakano. Yanashindana na kuchuana. Yanaendelea kupigana vikumbo yakizuru nchi jirani katika kile kinachoonekana kama jitihada za kusaka uwanja wa kupumulia.

Rais Kagame ambaye tangu kuzuka kwa mvutano huo amekutana na viongozi wa zaidi ya nchi tatu amekuwa akiikosoa waziwazi Uganda.

Mathalani, hivi karibuni wakati akifafanua mgogoro huo, Kagame alirejelea kitabu kinachoitwa ‘From Genocied to continental War’ kilichoandikwa na Gerard Prunier, mwandishi wa vitabu wa siku nyingi kutoka Ufaransa.

Anasema mwandishi huyo aliandika kwamba alikutana na waziri wa zamani wa mambo ya ndani, marehemu Seth Sendashonga mwaka 1998 pamoja na maofisa wakuu wa jeshi la Uganda na kuzungumzia mipango ya kumsaidia Sendashonga ili kuangusha utawala wa Kagame. Mwandishi huyo katika kitabu chake kulingana na maelezo ya Rais Kagame, Uganda ilikuwa imeahidi kumsaidia kijeshi.

“Sababu ya mimi kurejelea kuzungumza haya nimetaka kuwaonyesha mfululizo jinsi mambo yalivyokwenda mnamo miaka 20 iliyopita. Tulijaribu kufanya mikutano ya hapa na pale ili kutafuta suluhu lakini matatizo hayo hayaishi. Ukweli ni kwamba Seth Sendashonga alifariki dunia kwa kuwa alivuka mstari mwekundu. Sifurahii kusema hivyo lakini pia sijutii kifo chake.’’

Sendashonga aliuawa katika mazingira ya kutatanisha mwaka 1998 mjini Nairobi alipokuwa uhamishoni baada ya kutofautiana na utawala wa Rwanda.

Rais Kagame anasema mgogoro huo ulishika kasi hivi karibuni kufuatia wananchi wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda na kufanya kazi nchini humo kukamatwa na akuteswa.

Kagame pia anaushutumu utawala wa Uganda kutoa nafasi ya ushirikiano kwa kundi la RNC linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda, Jenerali Kayumba Nyamwasa.

“RNC wanafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya Uganda. Wanachokifanya ni kunyanyasa Wanyarwanda ambao hawataki kuungana nao huku wakisingizia kwamba wametumwa na utawala wa Kigali kuhujumu usalama wa Uganda na kuua upinzani. Ni madai yasiyo na msingi lakini yanaonyesha tuhuma za ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Uganda na kundi la RNC.’’

Wakati wote Uganda imekuwa ikijiweka kando na shutuma hizo na kuwakikishia wananchi wake juu ya kile kinachoendelea na jirani yake.

Rais Museveni anasema nchi yake iko tayari kukabiliana na kushinda uvamizi wowote.

Akizungumza katika Mkoa wa Rwenzor uliopo karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mseveni aliwataka wananchi wake wasiogope.

“Hakuna mtu atakayevuruga amani nchini Uganda. Amani itahifadhiwa. ADF iko Congo na vita vitaendelea pale. Yeyote anayetaka kusababisha mgongano huko Kasese, hawezi kusimama.”

Uganda imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwatuma majasusi na kuifanyia vitendo vya ujasusi kwenye ardhi yake, shutuma ambazo Rwanda imekanusha.

Rais Kagame amesisitiza kwamba mara kadhaa mwenyewe aliwasilisha malalamiko hayo kwa mwenzake Museveni na kwamba hakuonyesha utashi wowote wa kuyatatua.

Hivi karibuni Rwanda ilizuia wananchi wake kwenda nchini Uganda na kusababisha mkwamo wa kibiashara.

Wakati hali ikiwa hivyo, Rwanda imeanza kuwa karibu na baadhi ya mataifa jirani na wachambuzi wa mambo wanahisi huenda hatua hiyo ni ishara ya kutaka kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa hayo.

Hali kama hiyo pia imeshuhudiwa kwa Uganda ambayo imekuwa ikikutana na viongozi mbalimbali katika eneo la Afrika Mashariki huku kiini cha majadiliano yao kikiendelea kuwa mioyoni mwao.

Kagame awali alikutana na Rais Uhuru Kenyatta wa nchi ya Kenya na wote walionekana wakiwa katika hali ya furaha na kila mmoja akielezea namna anavyomhitaji mwenzake.

Kenyatta aliwaambia wajumbe katika mkutano wa uongozi wa kitaifa kuwa “wakati changamoto zinajitokeza, kwa nia njema na nzuri, zinaweza kutatuliwa”.

Aidha, akiwa nchini Angola Rais Kagame alikutana na mwenyeji wake Joao Lourenco ambako pia walikuwa na majadiliano ya faragha.

Ziara hiyo ya Kagame imefanyika siku chache baada ya kuzuru nchini na kukutana na mwenyeji wake, Rais John Magufuli.

Wawili hao walikuwa na mazungumzo ya faragha yaliyofanyika ikulu na baadaye kiongozi huyo alirejea tena nyumbani.

Pia, amekuwa na ziara nchini Afrika Kusini ingawa hakukuwa na taarifa ya kina iliyoelezea kile kilichojadiliwa wakati alipokutana na mwenyeji wake Rais Cyril Ramaphosa.

Kama ilivyo kwa mwenzie, Rais Museveni naye amejishughulisha kwa mfumo huo huo.

Amekuwa na majadiliano ya kina wakati alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake, William Ruto waliozuru Uganda kwa nyakati tofauti hivi karibuni. Aidha, Rais Museveni hajaiweka kando Tanzania, ambako hivi karibuni alimtuma waziri wake wa mambo ya nje, Sam Kutesa alikuja na ujumbe maalumu wa Rais Magufuli.

Ingawa mazungumzo baina ya wakubwa hao ni ya faragha, ni dhari kila moja anajitahidi kunyoosha maelezo ili aweze kueleweka katika mataifa hayo rafiki.