Jinsi Watanzania, ubalozi wa Cuba walivyouchambua mgogoro wa Venezuela

Saturday March 2 2019

 

By Khalifa Said, Mwananchi [email protected]

Katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni kukataa kufumbia macho mgogoro unaoendelea kurindima nchini Venezuela, baadhi ya wasomi na wanaharakati wa masuala ya kimataifa walikutana mjini hapa wiki iliyopita kwa lengo la kutafakari namna ambavyo wanaweza kusaidia kuepusha machafuko katika taifa hilo la kusini mwa bara la Amerika.

Kikao hicho kilifanyika siku tatu kabla ya kuibuka kwa purukushani Februari 23 katika mpaka wa Venezuela na Colombia baina ya wafuasi wa rais wa mpito aliyejitangazia ushindi, Juan Guaidó na wale wanaomuunga mkono rais wa sasa, Nicolás Maduro kuhusu uingizwaji wa ‘msaada wa kibinadamu’ kutoka Marekani. Wakati Guaidó anasisitiza kuwa msaada huo ni muhimu kwa Wavenezuela, Maduro ameuita kuwa ni njia ya Marekani kulivamia taifa hilo.

Washiriki wa kikao hicho, ambao walionekana kuwa na uelewa mpana si tu juu ya historia ya bara la Amerika Kusini, bali pia uhusiano wa muda mrefu wa Marekani na nchi za bara hilo, walitafakari njia wanazoweza kuzitumia katika kuimarisha vuguvugu na shinikizo la kimataifa linalolenga kuzuia serikali ya Marekani kubadili uongozi nchini Venezuela.

Kuepusha uvamizi

Wakikutana chini ya mwavuli wa ubalozi wa Cuba nchini, washiriki walitambua mchango ambao vuguvugu kutoka sehemu mbalimbali duniani linaweza kutoa katika kuishinikiza Marekani kubadili sera yake ya sasa.

Kwa pamoja waliazimia kuunda umoja wa “mashirika na taasisi za mrengo wa kushoto, zinazopinga ubeberu na zinazojali mshikamano wa kimataifa na kutoa kauli ya pamoja ya kulaani vikali vitisho vinavyotolewa na Marekani dhidi ya taifa huru la Venezuela.”

Mfano wa mashirika yanayokusudiwa ni kama vile Kamati ya Mshikamano Kati ya Cuba na Tanzania, Jukwaa la Wajamaa Tanzania, Vuguvugu la Mshikamano kwa ajili ya Palestina, Kamati ya Mshikamano na Watu wa Sahrawi pamoja na mengine ambayo yanaweza kuja pamoja na kusisitiza umuhimu wa “mazungumzo kama njia bora ya kutafuta suluhu ya kudumu ya hali ya tata inayoikabili Venezuela kwa sasa na kuirudisha nchi hiyo katika uimara wake.”

Kinacholengwa kufanikishwa ni “ushajihishaji wa vuguvugu la kimataifa kwa lengo la kulinda amani nchini Venezuela na katika bara lote la Amerika Kusini”. Lengo hili limejengwa na imani kwamba “vitisho dhidi ya taifa huru havijawahi kufanikiwa katika kudumisha uimara endelevu wa taifa husika na mara nyingi matokeo yake yamekuwa ni mabaya sana”.

“Kilicho hatarini kwa sasa ni uhuru wa Venezuela kama taifa na utu wa bara zima la Amerika Kusini na Caribbea na watu wa kusini mwa dunia kwa ujumla wao,” Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Profesa Lucas Polledo, alisema akiwakumbusha washiriki wa kikao hicho. “Swali ni kwamba je, uhalali wa serikali unatokana na ridhaa ya wananchi wa nchi husika au hutokana na serikali kutambuliwa na mataifa ya nje.”

Kikifanyika maelfu ya maili kutoka sehemu ambako mgogoro huo unaendelea, kikao hicho hata hivyo ni moja kati ya vingine kadhaa ambavyo vimekuwa vikifanyika katika sehemu mbalimbali za dunia tangu hali ya mambo ianze kuchafuka nchini Venezuela.

Ni nini kinaendelea Venezuela?

Taifa la Venezuela limegubikwa na mgogoro kwa kipindi kirefu sasa likiandamwa na machafuko ya kisiasa yaliyochochewa na mfumuko mkubwa wa bei, kukatika mara kwa mara kwa nishati ya umeme na uhaba wa vyakula na dawa. Zaidi ya watu wapatao milioni tatu wameripotiwa kuikimbia nchi hiyo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Katikati ya mzozo huu, mnamo Januari 23 mwaka huu, kiongozi wa Bunge la nchi hiyo, Juan Guaidó, aliutangazia umma kwamba atakuwa rais wa mpito wa taifa hilo hatua ambayo haikumfurahisha Rais Nicolás Maduro, ambaye ndiyo kwanza amekula kiapo cha kutumikia muhula wake wa pili wa miaka sita wiki mbili zilizopita baada ya kushinda uchaguzi ambao upinzani uliamua kuususia.

Rais wa Marekani, Donald Trump punde alimtambua Guaidó kama rais halali wa Venezuela dakika kadhaa tu baada ya Guaidó kujitangaza. Haikushangaza sana kwamba hatua ya Trump ilikumbana na mrejesho hasi kutoka kwa Rais Maduro ambaye kwa muda mwingi amekuwa akiishutumu Marekani kuwa nyuma ya juhudi za kumuondoa ofisini. Rais Maduro alivunja uhusiano na Marekani na kuwataka wanadiplomasia 72 wa nchi hiyo kuondoka Venezuela.

Wakati Guaidó ana uungwaji mkono kutoka Marekani, baadhi ya nchi za Amerika Kusini na viongozi wengine wa kimataifa, hata hivyo hana uungwaji mkono mkubwa ndani ya Venezuela. Idara ya usalama wa taifa na jeshi la nchi bado inaendelea kuwa mdau muhimu katika mzozo huu. Mpaka sasa, hata hivyo, idara zote mbili zimeendelea kubaki tiifu kwa Rais Maduro.

Huwezi kupuuza mgogoro huo Moja kati ya waliohudhuria kikao hicho cha majadiliano ni Salim Msoma, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Mshikamano Kati ya Cuba na Tanzania na ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Venezuela. Msoma anaamini kwamba inahitaji mtu mwenye moyo mzito sana kuweza kupuuzia kinachoendelea Venezuela.

“Kwa kweli huwezi kufumbia macho hali ambayo inaonesha taifa moja lenye nguvu linatishia kuivamia nchi nyengine dhaifu,” anaonya Msoma pembezoni mwa kikao hicho. “Sisi tuliopo Tanzania au Afrika kama bara tunaweza kufanya hivyo kwa madhara yetu wenyewe kwani kinachotokea Venezuela kinaweza pia kufanyika hapa ukizingatia kwamba mazingira ni yaleyale.”

Mazingira anayomaanisha Msoma ni uwepo wa rasilimali za mafuta na zinginezo nchini Venezuela, rasilimali ambazo hata Afrika zinapatikana ambazo Marekani inataka kuwa na uhuru usioingiliwa wa kuzidhibiti. “Ni rasilimali hizi ndiyo zinaifanya Marekani itake kuiadhibu na kuitesa Venezuela,” anasisitiza.

Alichobainisha Msoma si uvumi kwani hata Rais Trump mwenyewe amewahi kusema kitu hichohicho kwenye moja ya vikao vyake huko Ikulu ya Marekani. Kwa mujibu wa kitabu kilichoandikwa na aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa shirika la ujasusi (FBI), Andrew McCabe kilichopewa jina la Tishio, mwandishi anasimulia tukio lililotokea mwaka 2017: “Kisha Rais akaongolea kuhusu Venezuela. ‘Ile ni nchi ambayo ni lazima tuingie nayo kwenye vita,’ alisema. ‘Wana mafuta yote haya na wapo hapo kwenye mlango wetu wa nyuma.”

Hata hivyo, Msoma aliendelea kuonya, “tukiiachia Marekani iendelee na vitisho vyake kama inavyopenda dhidi ya Venezuela tutakuwa tunafanya uhalifu mkubwa wa kuiruhusu kufanya hivyo kwenye nchi zingine.

“Ndiyo maana ni muhimu sana kuishinikiza Marekani iachane na sera yake ya sasa na badala yake kuchagua majadiliano kama njia ya kutatua hali ya sintofahamu iliyopo Venezuela.”

Makosa makubwa yamefanyika

Lakini, Msoma si kwamba anamuondolea lawama Rais Maduro na serikali yake. Anasema kwamba malalamiko ya Wavenezuela ni ya msingi ambayo serikali inapaswa iyafanyie kazi. Wala hadhani kwamba kushindwa kwa Maduro kuboresha maisha ya wananchi wake kuna maanisha kushindwa kwa mradi wa kujenga ujamaa kama mbadala wa ubepari.

“Nafikiri serikali ilifanya makosa makubwa sana kwani wakati bei ya mafuta iko juu haikujisumbua kuwa na mpango wowote wa kupanua uchumi wake. Kwa kipindi chote hicho, kitu pekee serikali ilikuwa inajua ni kutumia tu. Sasa wakati bei ya mafuta iliposhuka kwa kasi, serikali haikuwa na namna bali kubana matumizi na hivyo ukinzani ukaanza kutokea,” anaelezea Msoma ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za kiserikali kabla ya kustaafu.

Nizar Visram ni mhadhiri na mwandishi wa habari mkongwe nchini ambaye ameandika makala kadhaa kuhusu kinachoendelea Venezuela. Visram anaukosoa “unafiki” wa Marekani wa kuonyesha kuwajali Wavenezuela kwa kuwapelekea msaada wa kibinadamu lakini haiko tayari kuondosha vikwazo vyake ilivyoviweka dhidi ya Venezuela.

“Sasa kwa vikwazo hivi, nchi inawezaje kuendelea na kuiwezesha serikali yake kuwapatia wananchi wake mahitaji yao ya msingi?” Anauliza Visram. “Vikwazo hivi vimeuharibu uchumi wa Venezuela. Hii haina maana kwamba hakuna aina fulani za ubadhirifu ndani ya serikali au sera za kijamaa ambazo Maduro anadai kutekeleza hazina mapungufu, lakini vikwazo vilivyowekwa vimeleta madhara makubwa kwa uchumi wa Venezuela.”

Advertisement