Jukata yataka terehe uchaguzi serikali za mitaa

Dar es Salaam. Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limeitaka serikali kutangaza mapema tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu ili kutoa fursa kwa vyama vya siasa kujiandaa.

Suala hilo ni miongoni mwa mapendekezo saba ya Jukata kuhusu mabadiliko ya kikatiba na kisheria yanayopaswa kufanyiwa kazi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Mambo mengine ni kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi, kuruhusu mgombea binafsi, vyama vya siasa kuruhusiwa kuungana na kusimamisha mgombea mmoja.

Pia wanataka mtu yoyote mwenye ushahidi aruhusiwe kupinga matokeo ya urais mahakamani na Tamisemi isisimamie chaguzi ndogo.

Mapendekezo hayo yalisomwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba wakati akifunga warsha ya siku mbili iliyowakutanisha viongozi wa vyama vya upinzani.

Alisema kitendo cha serikali kuchelewa kutangaza tarehe ya uchaguzi wa serikali za mitaa kinaminya mwanya kwa vyama vya upinzani kujiandaa kikamilifu na kujikuta wakipoteza kura katika sehemu nyingi.

“Tarehe hii iwekwe wazi kama ilivyo uchaguzi mkuu kila mtu anajua ni lini na anajiandaaje lakini pia ipo haja ya kubadilisha mambo yanayohusiana na uchaguzi ili uwe wa huru na haki,” alisema.

“Baada ya kuwepo kwa Tume Huru, Tamisemi isihusike katika kusimamia chaguzi zozote kwa sababu iko chini ya Rais na chama chake ni miongoni mwa vinavyoshiriki uchaguzi,” alisema na kuongeza: “Mbona nchi za wenzetu hili jambo (la kupinga matokeo) lipo, sisi tunaogopa nini ?”