KILIMO BIASHARA : Mambo muhimu kuyajua kilimo cha alizeti

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa mtandao wa Mogriculture TZ, kawaida mmea wa alizeti una mizizi mirefu yenye urefu sawa au zaidi ya urefu wa shina kwenda juu.

Alizeti ni zao la mbegu za mafuta linalolimwa kwa wingi nchini. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO) mwaka 2015, uzalishaji wa alizeti nchini ulikadiriwa kufikia tani milioni moja mwaka 2013, ingawaje takwimu za Wizara ya Kilimo zilionyesha kiwango kikubwa zaidi.
Zao hilo limekuwa likilimwa kwa wingi katika mikoa ya Shinyanga, Singida, Dodoma, Iringa, Tabora, Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Arusha, Manyara, na Rukwa.  
Hata hivyo, kuna mikoa mingine inayoongezeka kwa ulimaji wa zao hilo kutokana na kuongezeka kwa soko.
Kwa mujibu wa mtandao wa Mogriculture TZ, kawaida mmea wa alizeti una mizizi mirefu yenye urefu sawa au zaidi ya urefu wa shina kwenda juu.
Urefu wa mizizi yake unaweza kufikia mita 1 hadi 2 kwenda chini ambapo hukoma kukua baada ya kutoka kwa ua.
Alizeti inalo ua kubwa ambalo ndani yake kuna maua ambayo hjuja kugeuka kuwa mbegu zilizojipanga ambazo ndiyo nukamuliwa ili kupata mafuta.
Ua hilo lina ukubwa kuanzia sentimeta 15 hadi 30 na linakadiriwa kuwa na maua madogo 800 hadi 3000 na kila ua dogo moja lina uwezo wa kutengeneza mbegu.
Mtandao huo pia unafafanua kuwa katika kichwa cha alizeti kuzunguka kombe kuna maua petali yenye rangi ya manjano iliyokolea ambayo kazi yake kubwa ni kuvutia wadudu wachavushaji kama vile nyuki na vipepeo.
Mbegu za alizeti huanza kutengenezwa katika kichwa kuanzia siku 10 hadi 15 tangu kutoka kwa maua.
Kichwa kikubwa cha alizeti kina uwezo mkubwa wa kutengeneza mbegu ukilinganisha na kichwa kidogo.
Kwa mfano kichwa chenye ukubwa wa sm 30 kinaweza kuzalisha gramu 19 hadi 20 za mbegu wakati kile chenye ukubwa wa sm 16 kinaweza kuzalisha hadi gramu 54. Itaendelea wiki ijayo